Baraza la Maulamaa India lataka aliyemvunjia heshima Bwana Mtume Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam achukuliwe hatua

Baraza la Maulamaa wa Kiislamu wa India limeitaka serikali iwachukulie hatua kali na ya haraka waliomvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW.

Maulana Sayyid Muhammad Othman, Mkuu wa Baraza la Maulamaa wa Kiislamu wa India ametaka watu waliomvunjia heshima Bwana Mtume SAW wapewe adhabu na akaongeza kuwa, hiyo ndio njia pekee itakayoweza kupoza hisia zilizotiwa machungu za Waislamu na kudhamini amani ya nchi.

Maulana Sayyid Othman amebainisha kuwa, Bwana Mtume Muhammad SAW anaheshimiwa na jamii yote ya Waislamu; na kumvunjia heshima yeye ni sawa na kuwatusi na kuwavunjia heshima Waislamu milioni 200 wa India.

Kiongozi huyo wa Baraza la Maulamaa wa Kiislamu wa India ameeleza kwamba, serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi inapaswa kuzuia vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu; vyenginevyo, vitendo vya aina hiyo vitasababisha mpasuko mkubwa zaidi wa tofauti ndani ya nchi hiyo.

Hivi karibuni, mpwa wa mbunge mmoja wa chama tawala cha BJP alituma maelezo katika mtandao wa kijamii wa Facebook ya kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW.

Waislamu wa India walioghadhibishwa na kitendo hicho kichafu walifanya maandamano ya kukipinga, lakini ukandamizaji uliofanywa na polisi ulipelekea Waislamu watatu kuuawa.

Serikali inayotawala hivi sasa nchini India ambayo inafuata fikra za Uhindu wa misimamo mikali, katika mwaka mmoja uliopita imechukua maamuzi kadhaa dhidi ya jamii za kidini za walio wachache hasa Waislamu na kuzusha hofu na wasiwasi mkubwa kwa wananchi hao.

0 Comments