Enyi ndugu zangu! Jiandaeni na jambo hili

 

Albarau bin Azib (Allah amridhie) amehadithia kuwa, siku moja wakiwa na Mjumbe wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) waliona kundi kubwa la watu.


Mtume akawauliza: “Ni jambo gani limewakusanya hapa?” Maswahaba wakajibu: “Wamekusanyika kwa ajili ya kuchimba kaburi.” Mtume alipatwa na hofu kubwa baada ya kusikia maneno hayo, akaondoka na kuelekea upande yalipo makaburi kisha akapiga magoti.


Ibnu Azib, ambaye alikuwa amesimama karibu na Mtume amesema:


“Nilimuelekea Mtume na kutazama anachokifanya. Nilipomuangalia usoni nikamuona analia kwa uchungu mpaka akalowesha mchanga kwa machozi yake. Kisha Mtume akatuelekea na kutuambia: “Enyi ndugu zangu! Jiandaeni na jambo hili.” [Ahmad].


Katika tukio hili yapo mengi ya kujifunza. Hapa tutaja baadhi ya mambo muhimu ya kujifunza.


Kujiandaa na kifo

Umauti au kifo ni jambo zito lisiloepukika katika maisha ya mwanadamu. Hakuna ajuae siku wala saa ambayo kifo kitamkumba.


Allah ‘Azza Wajallah’ anasema: “Hakika kuijua saa (ya Kiyama) kuko kwa Allah. Na Yeye ndiye anayeiteremsha mvua. Na anavijua vilivyomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yeyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yeyote haijui itafia nchi gani. Hakika Allah ndiye Mwenye kujua, Mwenye habari.” [Qur’an, 31:34].


Uzito wa kilio cha Mtume

Tukio la Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kutoa machozi (kulia) lina athari kubwa na halipaswi kupuuzwa. Hili ni tukio linalotupa taswira ya uzito wa kifo na misukosuko yake. Kaburi, ambalo watu wengi wameghafilika nalo lilimfanya Mtume wa Allah alie kwa uchungu mpaka akalowesha mchanga kwa machozi yake.


Mtume alilia sana kwa sababu alijua uzito wa maisha ya kaburini kwa yule ambaye hakufanya amali (matendo) mema katika maisha ya Dunia. Kaburi ni kituo ambacho mtu anaweza kuishi maisha ya raha au ya tabu.


Imepokewa na Uthman bin Affan (Allah amridhie) kwamba Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kila aliposimama kwenye kaburi alikuwa akisema:


“Hakika kaburi ni mashukio (nyumba) ya kwanza katika nyumba za Akhera. Atakayeokoka hapo, basi yaliyo baada ya hapo ni mepesi zaidi. Ama yule asiyeokoka hapo (kaburini), basi yatakayotokea baada ya hapo ni magumu zaidi.” [Ahmad].


Madhara ya kutojiandaa na kifo

Maisha ya kaburini ni kile kipindi anachokaa mtu baada ya kufa kwake mpaka kufufuliwa kwake. Ni kipindi kati ya parapanda la kwanza ambalo ni amri ya kufa viumbe wote na para – pand a l a pili ambalo ni amri ya kufufuliwa viumbe vyote vitakavyotakiwa vifufuke. Katika maisha ya kaburini, roho za watu wema hukaa mahali pazuri kungojea malipo yao ya peponi. Ama roho za watu waovu huwekwa mahabusu kungojea siku ya hukumu yao.


Allah anatuuliza swali la kutuzindua juu ya uzito tulionao katika kujianda na maisha ya Akhera.


“Enyi mlio amini! Zisikusahaulisheni mali zenu wala watoto wenu kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndiyo waliopata hasara. Na toeni katika tulichokupeni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, tena h a p o aseme, ‘Mola wangu Mlezi! Huniahirishii muda kidogo nipate kutoa sadaka ili (nami) niwe katika watu wema?’” [Qur’an, 63:9–11].


Katika aya nyingine, Allah anasema: “Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: ‘Mola wangu Mlezi! Nirudishe. Ili nitende mema badala ya yale niliyoyaacha.’ Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi m p a k a siku watapofufuliwa.” [Qur’an, 23:99].


Kifo hakiepukiki

Allah ‘Azza Wajallah’ anasema: “Hakika hayo mauti mnayoyakimbia bila ya shaka yatakukuteni. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kuyajua yaliyofichikana na yanayoonekana. Hapo atakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.” [Qur’an, 62:8].


Kutoka kwa Ibn Umar (Allah amridhie yeye na baba yake) amesema: “Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alinishika bega na kuniambia: ‘Ishi duniani kama vile mgeni au mpita njia.’” [Sahih Al–jaami’I].


Pia, Ibn Umar (Allah amridhie) alikuwa akisema: “Utakapofika jioni usingojee (usitegemee kuishi mpaka) asubuhi, na utakapofika asubuhi usingojee jioni. Na chukua siha (afya) yako kabla ya maradhi yako, na uhai wako kabla ya kufa kwako.” [Bukhari].


Kutumia wakati vizuri

Kitendo cha Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kupiga magoti na kulia mbele ya kaburi kinathibitisha kuwa umauti ni jambo zito ambalo kila kiumbe litamfika. Hivyo, ni muhimu kwa Muislamu kujitathmini ili kuweza kuacha vitendo visivyompendeza Allah Ta’ala.


Mtume amesema: “Chukua faida ya mambo matano (5) kabla ya matano (5); Ujana wako kabla ya uzee wako, afya yako kabla ya maradhi yako, mali yako kabla ya ufukara wako, faragha kabla ya kushughulishwa kwako, na uhai wako kabla ya kifo chako.” [Bukhari].


Kuandika usia

Ni vema kila Muislamu ahakikishe anaandika usia wa mali yake kwa wazazi wake na jamaa zake, yakiwemo madeni anayodai au anayodaiwa. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:


“Si haki kwa Muislamu ambaye ana jambo la kuusia, zikampita siku mbili isipokuwa ahakikishe kuwa usia wake umeshaandikwa.” [Bukhari].


Kudumisha uchamungu

Kumcha Allah ndiyo njia bora ya kujiandaa na umauti. Allah anatuambia:


“Na jitengezeeni zawadi. Na hakika bora ya zawadi ni uchamungu. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili!” [Qur’an, 2:197].


Kukumbuka umauti

Kuzuru makaburi ni jambo linaloruhusiwa kisheria. Hili ni jambo linalowafanya watu wakikumbuke kifo. Imepokewa hadith kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema:


“Nilikuwa nimewakataza kwanza kuzuru makaburi lakini kuanzia sasa yatembeleeni kwani hakika (makaburi) yanawakumbusheni Akhera.” [Sahihi Al–jaami’I].


Na katika riwaya nyingine, Mtume amesema: “Kwani huko kuzuru makaburu huwakumbusha Akhera.” [Ahmad].


Toba

Watu wengi humuomba Allah msamaha kutokana na makosa wanayoyafanya, lakini wanaotubia kikwelikweli ni wachache. Watu wengi hujikuta wanatubu lakini hawatimizi masharti ya toba.


Kujiandaa na umauti kunahitaji toba ya kweli kama anavyobainisha Mwenyezi Mungu:


“Enyi mlioamini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika pepo zipitazo mito kati yake.” [Qur’an, 66:8].

0 Comments