Historia Fupi Ya Imaam Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله)

 

Jina Lake:

 

Ahmad bin ‘Aliy bin Muhammad, bin Muhammad, bin ‘Aliy, bin Mahmuwd, bin Ahmad, bin Ahmad bin Al-Kinaaniy Al-‘Asqalaaniy. Umaarufu wake ni Ibn Hajar ‘Asqalaaniy.

 

 

Babu zake waliishi Asqalaan ambapo walifika huko katika mwaka wa 583H. Jiji la Asqalaan liko Palestina huko Gaza. Neno Hajar ni jina la mmoja wa babu zake. Kun-ya yake ni Abul-Fadhwl na Laqab yake ni Shihaabuddiyn.

 

 

Kuzaliwa Kwake:

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alizaliwa tarehe 12 mwezi wa Sha'baan, 773H. Inasemekana pia amezaliwa tarehe 10 Sha’baan.  Alizaliwa Misri karibu na  ufukoni wa mto wa Nile alikulia huko huko.    

 

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alikuwa yatima. Baba yake ambaye alikuwa Mwanazuoni mkubwa na mfanya biashara alifariki katika mwaka wa 777H akimwacha Ibn Hajar (رحمه الله) akiwa na miaka minne tu. Mama yake alifariki kabla ya hapo na kwa hivyo alikuwa yatima kutoka kwa wazazi wake wote wawili.

 

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) amekulia katika familia yenye maadili mema na wazazi wenye ‘ilmu na wenye kushajishana katika kutafuta ‘ilmu.

 

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alikuwa ana kaka mkubwa ambaye alikuwa ni ‘Aalim, lakini alifariki kabla ya Ibn Hajar,  na kwa sababu hii, baba yake alikuwa na majonzi makubwa na huzuni mno.  Mmoja wa Swaalihiyna Shaykh Yahyaa Asw-Swaanifiriy aliota ndoto akambashiria baba yake Ibn Hajar akamwambia kwamba atarithiwa (‘ilmu yake) na mtu ambaye atakuwa bora kuliko yeye, atakayekuwa na maisha marefu na kwamba atatoka katika mgongo wake ‘Aalim atakayejaza dunia kwa ‘ilmu.  Ibn Hajar   ‘Asqalaaniy (رحمه الله) mwenyewe kisha akasema:  "Nilizaliwa kisha Allaah (سبحانه وتعالى Akanifungulia mikono.” Kwa maana: Allaah Amemjaalia nuru ya 'ilmu kubwa na akili nzuri ya busara.

 

 

Ibn Hajar  ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alilelewa na Zaakiy Al-Kharuwbiy ambaye alikuwa tajiri mfanya biashara maarufu.  

 

 

Ibn Hajar  ‘Asqalaaniy (رحمه الله) anahesabiwa kuwa ni mmoja wa watu adimu katika Historia ya Kiislamu. Imaam Al-Albaaniy (رحمه الله) alisema: "Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله alikuwa miongoni mwa ‘Ulamaa wakubwa kabisa, ambaye alihifadhi   Hadiyth kwa usahihi kabisa wa hali ya juu.”

 

 

Elimu Yake:

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alianza madrasa akiwa na umri wa miaka mitano, akahifadhi Qur-aan akiwa na umri wa miaka tisa. Alikuwa na akili nzuri mno ya kuhifadhi; aliweza kuhifahdi Suwrah Maryam kwa siku moja tu.

 

 

Mlezi wake; Zaakiy Al-Kharuwbiy alikwenda naye Hajj, akabakia huko na alipofika umri wa miaka kumi na mbili aliimamisha Waislamu Swalaah za Taraawiyh katika Masjid Al-Haram Makkah. Alikuwa ni mtoto tofuati na wenzake kutokana na upeo wa ‘ilmu yake na kuhifadhi kwake Qur-aan na kuweza kuimamisha watu katika umri mdogo kama huo. Hapakuweko na mtoto ambaye aliyelingana sawa naye katika ‘ilmu. Alipokuwa Makkah alihudhuria duruws za ‘Ulamaa waliokuwa wakifundisha huko.

 

 

Mnamo mwaka wa 786H Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alihama kutoka Makkah kurudi Misr ambako alihifadhi vitabu kadhaa vya mukhtasari  mfano: ‘Umdatul-Ahkaam cha Al-Maqdisiyy na Al-Haawiy ambacho ni cha  Fiqh ya Ash-Shaafi’iy na pia  Al-Mukhtasar Al-Haajib ambacho ni cha Usuwl Al-Fiqh, na vitabu vingine vya sarufi ya lugha ya Kiarabu.

 

 

Alipofika umri wa miaka kumi na tisa aliisoma Qur-aan yote kwa Tajwiyd mbele ya Shihaab Al-Khayuwtwiy na alizisoma Hadiyth za Swahiyh Al-Bukhaariy mbele ya Mashaykh mbali mbali .

 

 

 

Akazidi kutafuta ‘ilmu katika sayansi mbalimbali, kama Tafsiyr na Qiraa-ah.  Alikuwa akipenda sana kusoma Historia. Na alipenda sana kusoma fasihi ya lugha ya Kiarabu. Mmoja wa ‘Ulamaa   Al-Badr Al-Bushtakiy alimhimiza kusoma Al-Ghaaniy, ambayo ni vitabu vikubwa vilivyoandikwa katika fasihi ya Kiarabu. Vitabu hivyo vilikuwa ni mjeledi  takriban ishirini mpaka thelathini na Ibn Hajar (رحمه الله) alivisoma vyote kwa umakinifu hadi akawa, pindi akisikia shairi aliweza kutambua mtunzi wake na kufahamu kwa kina shairi hilo.  Alipokaribia kufikia umri wa miaka ishirini na tano alikuwa ameshachuma na kukusanya ‘ilmu ambayo hapakuweko mtu aliyeweza kukusanya ‘ilmu kama yeye.  

 

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) aliandika mashairi mwenyewe. Akaanza kusoma zaidi Sayansi ya Hadiyth na Allaah (سبحانه وتعالى) Akamjaalia mapenzi ya Hadiyth yakamsukuma kujifunza Sayansi ya Hadiyth kuzihifadhi moyoni mwake.   

 

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) akazidi kupatwa  shauku kubwa na bidii ya kuzidi kutafuta elimu. Aliweza kujifunza elimu kubwa na alibarikiwa na Allaah (سبحانه وتعالى) katika fani hiyo. Alikuwa akitembea sana masafa na safari  za asubuhi na jioni kutafuta ‘ilmu kutoka kwa ‘Ulamaa wa zama zake.

 

 

Alisafiri kwenda Hijaz Sham, Syria, Misri akifika mpaka Alexandria, na sehemu zingine pia, ambapo aliweza kuchuma faida tele ya ‘ilmu na pia akanufaisha watu kwa ‘ilmu.

 

Alisafiri pia kwenda Yemen ambako alikutana na  baadhi ya ‘Ulamaa  kama Fayruwz Aabaadiy  ambaye ni ‘Aalim bingwa mkubwa wa sarufi ya Kiarabu ambaye aliandika moja ya kamusi ya Lugha ya Kiarabu inayojulikana kama Qamuws Al-Muhiytw. 

 

 

Pindi Ibn Hajar  ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alipokuwa na umri wa miaka sitini na kipindi hiki alikuwa tayari ni ‘Aalim mkubwa,  lakini hii haikumzuia kusafiri kwa ajili ya  kutafuta ‘ilmu.  Hii inaonyesha  jinsi gani Imaam huyu mkubwa alivyokuwa na shauku na kuthibitika kwake kutafuta ‘ilmu kutoka kwa ‘Ulamaa wengineo. 

 

 

Daraja Yake ‘Ilmu Na Hadhi Yake:

 

‘Ulamaa wa zama zake walimpa  Ibn Hajar  ‘Asqalaaniy (رحمه الله) kipaumbele na walimheshimu na akaheshimika katika zama zake na zama za baada yake. 

 

Al-Buqaa'iy alisema kumhusu Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) kwamba: “Yeye ni Imaam wa Waislaam.”  

 

Ash-Shawkaaniy amesema: “Yeye ni Al-Haafidhw Maarufu mwenye upeo wa ‘ilmu ya Hadiyth.”

 

Basi ilikuwa anapotajwa mtu kwa “Al-Haafidhw” ilijulikana moja kwa moja kuwa ni Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله).

 

 

Kufundisha Kwake:

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alifundisha Sayansi tofauti za Kiislam kama Tafsiyr ya Qur-aan, Qiraa-ah, Hadiyth, Fiqh (Shariy’ah) na kadhaalika. Alikuwa Mufti pia, hivyo alitowa Fatawa kwa watu.  Alijishughulisha sana kuendeleza ‘ilmu  ya Hadiyth,  akiifundisha na akiiandika. Alitoa mawaidha mahali pengi kama Al-Azhar, Jami’ ‘Amr, na penginepo. Pia alikuwa akifundisha wanafunzi wake kwa imla kutoka katika hifdhw yake. ‘Ulamaa wengineo, Qadhi na Mufti walikuwa wakisafiri kwenda kwake kuchota elimu yake.  

 

 

Walimu Wake Wengineo:

 

Miongoni mwa ‘Ulamaa  mashuhuri ambao alijifunza kutoka kwao alikuwa Al-Hafidhw Al-Iraqi na Ibn Al-Mulaqqin, ambao walikuwa ‘Ulamaa wawili mashuhuri wa Hadiyth na alijifunza kutoka kwa ‘Ulamaa hawa  wawili na ‘Ulamaa wengine kama wao.  Aliishi pamoja na Az-Zayn Al-Iraqi kwa miaka kumi. Pia alisomeshwa na Al-Balqini, Ibn Al-Mulaqqin,   Alijifunza Kiarabu kutoka kwa Al-‘Amari, alijifunza ufasaha wa lugha na mashairi kutoka kwa Al-Badr Al-Mushtaki, na alijifunza uandishi utoka kwa baadhi ya ‘Ulamaa. Pia alikuwa akiisoma Qur-aan katika Viraa vyote saba kutokwa kwa At-Tanuwkhiy.

 

 

Kazi Zake:

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) aliandika vitabu vingi vinavyopindukia mia moja na khamsini; vingi kati ya hivyo vilikuwa ni fani ya Hadiyth.   Wafalme na wana wafalme wakawa wanapeana zawadi ya vitabu vyake.

 

Kitabu chake maarufu ni Fat-h Al-Baariy ambacho ni Sharh ya Swahiyh Al-Bukhaariy.  Kitabu hiki hakika kilihesabika kuwa ni Kamusi ya Sunnah, bali ni Kamusi ya Sayansi za Kiislaam. 

 

Kitabu hiki kilihesabiwa kuwa na faida kubwa kwa kuwa ilikuwa inapoulizwa maswali, basi Ibn Hajar (رحمه اللهalitoa majibu kutokana na Kitabu hiki na kuwafanya waulizaji wapate fahamu kamili ya maswali yao. 

 

Pia katika kazi zake nyenginezo ni Tahdhiyb At-Tahdhiyb, Taqriyb At-Tahdhiyb, Lisaan Al-Miyzaan, Al-Iyswaabah fiy Tamyiyz Asw-Swahaabah, na Buluwgh Al-Maraam Min Adillat Al-Ahkaam.

 

Pia kazi zake (Vitabu) vingi mno mbalimbali vya Sayansi za Hadiyth, Tafsiyr, Uluwmul-Qur-aan.

 

 

Wadhifa:

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alikuwa Ustaadh, Mwandishi, Mufti na Qadhi wa Misri, kisha Sham, ikaongezewa kwenye eneo la madaraka yake, ambayo aliyashikilia kwa zaidi ya miaka ishirini. Mara ya kwanza, alikataa kukalia kiti cha Uqadhi, mpaka pale Sultani alipompelekea shauri moja makhsusi. Kisha akakubali kumwakilisha Al-Balqini alipomuomba sana awe Qadhi. Tena akashika wadhifa kwa ajili ya watu wengine mpaka alipoteuliwa akalie kiti cha Uqadhi Mkuu. Kisha akaondoka, lakini akalazimika kushika wadhifa wa Uqadhi mara saba, hadi alipoacha karibu na mwaka wa kufariki kwake

 

 

Khulqa (Tabia) Zake:

 

Kuhusu khulqa zake, Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alikuwa mnyenyekevu mno hadi kwamba alipoulizwa: “Je umepata kukutana au kumjua mtu kama wewe?” Alijibu:

 

فَلَا تُزَكُّوا أَنفُسَكُمْ ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اتَّقَىٰ ﴿٣٢﴾

Basi msizitakase nafsi zenu. Yeye Anamjua zaidi aliyekuwa na taqwa. [An-Najm: 32]

 

Na baadhi ya Swahibu zake walimuuliza: “Je wewe umehifadhi zaidi au Adh-Dhahabiy?” Alinyamaza kimya bila kujibu lolote.

 

Kwa hiyo, hakuwa mwenye kujigamba kutokana na ‘ilmu yake wala daraja yake katika jamii.

 

Alikuwa pia mvumilivu, na mwenye subira na ustahamilivu mkubwa sana, mwenye zuhd (kuipa mgongo dunia). Ilisemwa kuwa alikuwa mcheshi, mwaminifu, mwerevu, mtu anaejinyima anasa, asiyejiweka mbele mbele, mkarimu, mtoa swadaqah, na aliyedumu katika Swalaah na Swiyaam za faradhi na za Sunnah. Hakuwacha kamwe Swalaah za jamaa wala hakupata kuacha kuamka kuswali usiku hadi alipofika kupata maradhi yake aliyofia.  Imesemekana kwamba alikuwa akifunga Swiyaam siku moja na ya pili yake akila.

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alikuwa akila chakuka kidogo tu. Alikuwa mwangalifu katika kula chakula cha watu wengine, hakuwa na makuu, na alipokuwa safarini alikuwa akila chochote anachokipata. Pindi alipoishiwa na pesa za kununulia chakula, alikuwa akila chakula duni;  chakula ambacho  watu wa kawaida hawangeweza kula.   Alikuwa anatahadhari na kukhofia sana kula chakula cha watu kutokana na chumo la haraam.      

 

Alipenda kutoa vichekesho kidogo, na alikuwa na khulqa na desturi nzuri ya kuwasiliana na Imaam, wawe ni wa daraja la juu au watu duni kabisa, na akitaamuli vizuri na watu alioishi nao, wawe wazee au vijana, maskini na mafakiri.

 

Kwa ujumla Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alikuwa na akhlaaq njema za kila aina, akhlaaq ambazo apasavyo kuwa nazo Muumini wa kweli. As-Sakhaawiy aliandika mlango mzima kuhusu akhlaaq za Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله)

 

 

Kufariki Kwake:

 

 

Ibn Hajar ‘Asqalaaniy (رحمه الله) alianza kuumwa katika mwezi wa Dhul-Qa’dah mwaka 852H lakini hakuacha kufundisha wala kuacha kazi zake nyenginezo za kunufaisha Waislamu katika mambo ya dunia yao na Aakhirah yao, wala  hakuacha Swalaah ya jamaa. Kisha maradhi yakamzidi katika mwezi wa Dhul-Hijjah akashindwa kuhudhuria Swalaah ya ‘Iydul-Adhwhaa, ila aliswali Swaaah ya jamaa usiku wa kabla yake. Kisha ilipofika Jumanne tarehe 14 Dhul-Hijjah akazidiwa mno na maradhi hadi kufika Jumamosi tarehe 18 Dhul-Hijjah akafariki baada ya Swalaah ya ‘Ishaa.

 

 

Inasemekana kuwa aliswaliwa Swalaah ya Janaazah na Khaliyfah wa Al-‘Aabasiyy au Qaadhi  mkuu al-Baqlaaniy. Mazishi yake Misr yalihudhuria na umati wa Waislamu akiwemo   Sultan, pamoja na viongovi wengineo wa Kiislamu na ‘Ulamaa wakubwa na watu wengi mno walihudhuria hadi ilisemekana kwamba idadi ya watu waliohudhuria walifikia maelfu.  Na akaswaliwa pia Swalaatul-ghayb (Swalaah ya ghaibu) sehemu kadhaa za Kiislamu ikiwemo Makkah, Sham, na miji mingineyo ya  Kisalaam. Siku ya kufariki kwake ilikuwa siku adhimu ya huzuni kubwa kwa Waislamu.

 

Allaah Amrehemu Alimpe malipo mema ya Jannatul-Firdaws kwa juhudi zake katika Uislaam na kunufaisha kwake Waislamu.

 

 

0 Comments