Maandamano ya Kimya Kimya' ya Waislamu Warohingya wakikumbuka kufurushwa makwao


Zaidi ya wakimbizi Warohingya milioni moja wanaishi katika makazi makubwa zaidi ya wakimbizi duniani kusini mwa Bangladesh huku wakiwa na matumaini machache mno ya kurejea Myanmar, nchi ambayo imewanyima haki za uraia na haki zingine za kimsingi.

Wakimbizi wamesema janga la COVID-19 limewazuia  kuandaa maandamano makubwa ya kuadhimisha siku hii ambayo wanaiita 'Siku ya Makumbusho." Inkadiriwa kuwa watu 88 wameambukizwa COVID-19 katika kambi hiyo kubwa ya wakimbizi ambapo sita miongoni mwao wameaga dunia.

Miaka mitatu iliyopita, yaani Agosti 2017, inadaiwa kuwa wanamgambo walishambulia vituo vya polisi na kituo cha kijeshi katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar ambapo maafisa 12 wa usalama waliuawa.

Jeshi la Myanmar lilitumia kisingizio hicho kuanzisha oparesheni kubwa ya maangamizi ya umati dhidi ya Waislamu Warohingya ambao kwa muda mrefu walikuwa wanakandamizwa na kubaguliwa. Tukio hilo lilipelekea Warohingya 730,000 kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh na kujiunga na wenzao laki mbili ambao katika miaka ya nyuma walikuwa wameikimbia nchi yao.

Umoja wa Mataifa umesema ukandamizaji wa Waislamu nchini Myanmar ambao unatekelezwa na jeshi la nchi hiyo una lengo la maangamizi ya kimbari.

Utawala wa Myanmar unakanusha kufuatilia malengo ya mauaji ya kimbari na kudai kuwa kampeni iliyopita ni ya usalama dhidi ya wangamabo Warohinga.

Warohingya wanasema wamekuwa wakikabiliwa na mauaji ya kimbari kwa miongo kadhaa nchini Myanmar na wametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na taasisi zingine za kimataifa kutangaza kuwa kile kilichojiri nchini humo mwaka 2017 dhidi ya Waislamu ni mauaji ya kimbari.

0 Comments