Misikiti yafunguliwa tena Algeria baada ya kufungwa kwa miezi mitano

Kwa mujibu wa taarifa, mbali na misikiti serikali ya Algeria pia imeruhusu kufunguliwa migahawa, maeneo ya fukwe za baharini na mabustani lakini sheria ya kutotoka nje inaendelea kutekelezwa katika zaidi nusu ya Algeria. Halikadhalika watu wote watatakiwa kuvaa barakoa wakiwa nje ili kupunguza maambukizi ya corona.

Idadi kubwa ya watu walimiminika katika fukwe za bahari Jumamosi katika mji mkuu wa Algeria, Algiers na kuchukua fursa hiyo kuogelea katika Bahari ya Mediterranea wakati huu wa msimu wa joto. 

Pamoja na kuwa misikiti imefunguliwa lakini watoto, wanawake na watu wazee hawataruhusiwa kutumia maeneo hayo ya ibada. Aidha kwa sasa sala za Ijumaa zitaendelea kuwa marufuku misikitini nchini humo ili kuzuia msongamano mkubwa wa watu. Halikadhalika wanaofika msikitini wanatakiwa kuvaa barakoa, kubeba mkeka au zulia binafsi la kuswali na kuzingatia sheria ya kutokaribian. Waziri wa Masuala ya Kidini Algeria Mohamad Belmahdi amesema kila mtu anapaswa kuwa na nidhamu ili kuzuia kuenea corona. Amesema serikali inaweza kuamua kufunga tena misikiti iwapo watu watapuuza sheria za kuzua maambukizi ya corona.

Hadi kufikia Ijumaa, Algeria ilikuwa na kesi 37,000 za maambukizi ya corona huku waliofariki wakiwa ni 1,350 na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa ya tatu iliyoathiriwa vibaya na corona Afrika baada ya Afrika Kusini na Misri.

0 Comments