Msikiti mkubwa zaidi Afrika kufunguliwa Novemba

Kwa mujibu wa taarifa msikiti huo ulio katika mji mkuu wa Algeria ulianza kujengwa miaka minane iliyopita na sasa uko tayari kwa ajili ya ufunguzi rasmi.

Sherehe za ufunguzi huo zitafanyika mapema Novemba, sambamba na maadhimisho yam waka wa 66 wa Mapinduzi ya Algeria, amesema Rais Abdelmadjid Tebboun wakati alioputembelea msikiti huo.

Ilikuwa imepangwa kuwa msikiti huo ufunguliwe katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu lakini ufunguzi huo uliakhirishwa kutokana na janga la corona.

Msikiti huo una mnara mrefu zaidi duniani na ni mkubwa zaidi Afrika huku ukiwa wa tatu kwa ukubwa duniani.

Ujenzi wa msikiti huo ulianza Agosti 2012 na serikali ya Algeria ndiyo iliyofadhili ujenzi wake uliogharimu dola bilioni 1.

Msikiti huo una eneo lenye ukubwa wa mita mraba laki nne katika pwani ya Bahari ya Mediterrania. Ukumbi wa swala wa msikiti huo una uwezo wa kubeba waumini 37,000 na uwanja wa msikiti huo na una uwezo wa kubeba waumini 120,000. Aidha msikiti huo una nafasi ya kuegesha magari elfu saba. Halikadhalika jengo la msikiti huo linajumuisha madrassah ya Qur'ani, bustani, maktaba, nyumba za wafanyakazi , kituo cha wazimamoto, jengo la makumbusho la sanaa za Kiislamu na kituo cha utafiti.

Mnara wa msikiti huo una urefu wa mita 265 na hivyo kuufanya kuwa jengo refu zaidi barani Afrika

0 Comments