Msikiti wa Jamia mjini Nairobi wafunguliwa baada ya miezi mitano

Tangazo la kufunguliwa msikiti huo limeeneza furaha miongoni mwa Waislamu mjini Nairobi ambao kwa kawaida humiminika kwa malefu  katika swala za jamaa misikitni hapo.

Kutokana na kanuni mpya za kuzuia kuenea corona, msikiti huo ambao una uwezo wa kubeba waumini 10,000 utaruhusiwa kuwa na waumini 1,350 wakati wa swala.

Kila muumini anayefika msikiti ametakiwa abebe mkeka au zulia binafsi kwa ajili ya swala na kushika wudhuu kabla ya kuingia msikitini. Aidha sharti la kuingia msikitini hapo ni kuvaa barakoa na kupimwa kiwango cha joto mwilini. Halikadhalika wote wanaoingia msikitini wanatakiwa kunawa mikono kwa sabuni na kufuata maagizo ya wafanyakazi wa msikiti.

Ndani ya msikiti kila muumini anapaswa kuswali katika eneo ambalo limewekwa alama maalumu ambapo umbali wa kila muumini na mwenzake ni mita 1.5.

Wasimamizi wa msikiti wanasema wataendelea kufunga choo na eneo la wudhuu msikitini ili kulinda afya ya waumini katika amzingira ya sasa.


Msikiti wa Jamia mjini Nairobi ulifungwa Machi 18 ili kuzuia kuene ugonjwa wa corona. Mwezi uliopita rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alitangaza maeneo ya ibada yatafunguliwa lakini kwa kuzingatia kanuni maalumu za kiafya ili kuzuia kuenea corona.

0 Comments