September 19, 2020

Hatari ya kuwanyonyesha watoto maziwa ya kopo


 Mwaka 1991, Shirikisho la Dunia la Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama (World Alliance of Breast feeding Action (WABA) lilianzisha Maadhimisho ya Wiki ya Kunyonyesha Maziwa ya Mama Duniani (World Breastfeeding Week). Kuwekwa kwa wiki hiyo inayoadhimishwa kuanzia Agosti Mosi mpaka 7 kila mwaka katika nchi zaidi ya 120 inaonesha umuhimu wa maziwa ya mama kwa afya na ustawi wa mtoto. Kwamba, ni Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ndiyo wasimamizi wa wiki hii ni jambo jingine linaloonesha uzito unaopewa suala la unyonyeshaji wa maziwa ya mama

Mashirika hayo mawili, kwa pamoja, yaliazimia kulinda, kuboresha na kuendeleza utamaduni wa kunyonyesha watoto maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya kwanza tangu mtoto kuzaliwa. Duniani kote, Serikali zinahimiza watoto wanyonyeshwe maziwa ya mama pekee kwa muda wa miezi sita ya mwanzo.

Katika miezi hiyo sita, serikali zinahimiza mtoto asipewe maji, vinywaji au vyakula vingine kwa kuwa tafiti zinaonyesha kuwa mtoto anapokunywa maziwa ya mama pekee katika miezi hiyo sita, hupunguza vifo vya watoto. Baada ya mtoto kufikia umri wa miezi sita, aendelee kunyonyeshwa maziwa ya mama mpaka miaka miwili na huku pia akipewa vyakula vingine.

Licha ya himizo hilo la serikali, akinamama wengi katika baadhi ya nchi hawajakubali kurudi katika utamaduni wa kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama. Jambo linalosikitisha zaidi ni kuwa wanawake Waislamu nao wanadharau kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama hali ya kuwa kwao kufanya hivyo ni wajibu wa kidini.

Qur’an na kunyonyesha

Suala la kunyonyesha limezungumzwa kwa upana katika Qur’an. Hata muda wa kunyonyesha pia umetajwa.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kaamili kwa anaye taka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada…” [Qur’an, 2: 233].

“Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia), ‘Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio.’” [Qur’an, 31:14].

Vilevile, Mwenyezi Mungu anaendelea kuhimiza kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama kwa kusema:

“Na tumemuusia mwanadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini…” [Qur’an, 46:15].

Hapa Tanzania, kuna makosa kadhaa yanayofanywa na wanawake, ikiwemo kuanza kuwapa watoto vyakula vingine ndani ya miezi sita ya awali, kuwakatisha watoto nyonyo kabla ya miaka miwili.

Wapo baadhi ya wakinamama wana udhuru unaokubalika kisheria wa kushindwa kunyonyesha. Kuna changamoto ya baadhi ya kinamama kufanya kazi zinazowanyima fursa ya kunyonyesha. Wengine, maziwa hayatoki kwa sababu mbalimbali za kiafya bila kusahau udhuru kama ugonjwa, safari, kifo na kadhalika.

Ukiacha hao wenye udhuru, wapo baadhi ya kinamama wasiotaka tu kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama kwa kuwa wanaona hiyo ni kero inawanyima muda na uhuru wa ‘kustarehe’ kama vile kwenda matembezi au katika vilabu vya pombe na muziki.

Sio hivyo tu, wakinamama wengine wanaamini kuwa kunyonyesha kuna wazeesha mapema, na pia wataonekana hawajasoma na kuwa hawaendi na wakati. Mitazamo ya aina hii ni mbaya kwa sababu inaathiri afya, ustawi na makuzi ya mtoto.

Wakinamama, mtoto anatakiwa apewe maziwa ya kopo iwapo tu kuna sababu maalumu; na kwa kushauriana na daktari. La sivyo, ni vizuri mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama ili apate virutubisho na kinga mwilini vitakavyomwepusha na maradhi.

Usitumie maziwa ya kopo, ya wanyama bila udhuru

Mara nyingi watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya kopo au wanyama hupata maambukizi ya maradhi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa maziwa ya kopo hayana kinga (antibodies). Kinga hii ipo katika maziwa ya mama na hasa yale maziwa ya kwanza anayoyatoa mama baada ya kujifungua. Pia, maziwa ya kopo hayana virutubisho vyote muhimu anavyovihitaji mtoto mchanga ili aweze kukua vizuri.

Zaidi ya hayo, mtoto anayenyonyeshwa maziwa ya kopo anaweza kupata maambukizi ya maradhi kama maziwa yataandaliwa kwa kutumia maji yasiyokuwa safi wala salama. Tukumbuke pia kuwa, chupa na chuchu za kumnyonyeshea mtoto huwa tabu sana kusafishika kwa hiyo zinaweza kuwa chanzo cha maradhi kwa mtoto anayenyonyeshwa maziwa kwa kutumia chupa.

Vilevile, maziwa ya kopo ni gharama kubwa na familia nyingi hazimudu na matokeo yake yanaongezwa maji mengi ili mtoto ashibe. Kwa mfano, mtoto wa miezi mitatu anahitaji maziwa ya kopo kilo moja kila wiki, jambo ambalo watu wachache sana wanamudu.

Watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya kopo au ya wanyama wanaweza kupata matatizo ya kiafya kama uzito na unene kupita kiasi, kisukari, kuharisha, tundu la hewa, pumu, kifua kisichosikia dawa na mzio (allergies).

Pia, maziwa ya kopo yakiwa yamewekwa kwa muda mrefu katika hali ya joto na vijidudu vya maradhi huzaliana na hivyo vijidudu hivyo vinaingia tumboni kwa mtoto atakaponyweshwa maziwa hayo.

Ni vema pia watu wafahamu kuwa maziwa ya wanyama kama ng’ombe nayo hayafai kuwapa watoto wenye umri chini ya miezi sita kwa sababu utumbo na mwili wa watoto hao hauwezi kuyatumia maziwa hayo kwa ukamilifu.

Mtoto anahitaji kufikisha angalau mwaka mmoja aweze kutumia maziwa hayo bila ya shida. Ikumbukwe kuwa, fumula ya virutubisho vya maziwa ya ng’ombe ni kwa ajili ya kumkuza ndama ambaye mahitaji yake si sawa na yale ya mtoto wa binadamu.

Kwa hiyo, tunawanasihi wakinamama kama hawana udhuru wa kisheria rudini katika utamaduni wa kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama ili kuwanusuru wapate makuzi mema.

Faida kwa mama

Faida za kunyonyesha haziishii kwa mtoto pekee bali huenda hadi kwa mama anayenyonyesha, Wataalamu wanasema, kunyonyesha husaidia kupunguza uzito kwa mama hasa baada ya kujifungua

Pia, kunyonyesha husaidia kutolewa kwa kichochezi kiitwacho ‘Oxytocin’ ambacho husaidia kurudisha mfuko wa kizazi katika size yake ya zamani kabla ya ujauzito. Vilevile, kunyonyesha husaidia kupunguza hatari ya saratani za matiti na pia hupunguza hatari za matatizo ya mifupa.

Kubwa zaidi kuliko yote, kunyonyesha husaidia kutengeneza ukaribu kati ya mtoto na mama, yaani tunaita ‘bonding.’ Ikumbukwe mama anaponyonyesha humpa mtoto huduma ambayo hawezi kuipata kwa mtu mwingine yoyote, hivyo hutengeneza ukaribu maalumu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only