Siku Ambayo Kila Mmoja Atakayomkimbia Mwenzake

 Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa):   

فَإِذَا جَاءَتِ الصَّاخَّةُ ﴿٣٣﴾ يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ ﴿٣٤﴾ وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ ﴿٣٥﴾ وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ ﴿٣٦﴾ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ ﴿٣٧﴾

Basi utakapokuja ukelele mkali wa kugofya (baragumu la Qiyaamah)Siku mtu atakapomkimbia ndugu yake. Na mama yake na baba yake. Na mkewe na wanawe. Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na hali ya kumtosheleza. ['Abasa: 33-37]

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema kuwa "As-Saakh-khah ni moja wapo wa jina la siku ya Qiyaamah, siku ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Amewaonya waja Wake". [At-Twabariy 23:229]

Ibn Jariyr amesema: "Labda ni jina la kupigwa baragumu" [At-Twabariy 23:231] 

Al-Baghaawiy amesema: "As-Saakh-khah ina maana ukelele wa mngurumo wa siku ya Qiyaamah. Umeitwa hivyo kwa sababu utawazibua watu masikio. Hii ina maana kwamba utapenya katika masikio hadi kwamba utayazibua”. [At-Twabariy 24:449]

Siku hiyo kila mmoja atamkimbia mwenzake kutokana na kiwewe cha hali ya juu kitakachowasibu watu Siku hiyo. Hakuna mmoja atakayetaka kumsaidia mwenziwe. Hata Rasuli hawataweza kumsaidia mfuasi wake Siku hiyo, kila mmoja atasema "nafsiy nafsiy" (nafsi yangu, nafsi yangu). Hata 'Iysa mwana wa Maryam atasema: "Sitomuomba (Allaah) kuhusu yeyote ila nafsi yangu. Situmuomba hata Maryam ambaye amenizaa. [Muslim]. 

Atakayetuombea pekee ni Nabiy Muhammad  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Hali itakavyokuwa Siku hiyo imetajwa pia katika Hadiyth ifuatayo:

 عَنْ عائِشَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْها أَنَّ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّمَ قالَ:  ((يُبْعَثُ النّاسُ يَوْمَ القِيامَةِ حُفاةً عُراةً غُرْلاً)) فَقالَتْ عائِشَةُ:  فَكَيْفَ بِالعَوْراتِ قالَ  (لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ)

Kutoka kwa ‘Aaishah Radhwiya Allaahu ‘anhaa  kwamba Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam amesema: ((Watu watafufuliwa siku ya Qiyaamah bila ya viatu, uchi na bila ya kutahiriwa)) Akasema  ‘Aaishah: Vipi watakuwa uchi? Akasema: ((Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na hali ya kumtosheleza)) [An-Nasaiy] 

0 Comments