September 19, 2020

Tuunge mkono JAI katika kuuguza wagonjwa


 Mara nyingi tunapozungumzia masuala ya afya, upande wa wahudumu tunawataja zaidi madaktari, manesi, wakunga, na watawala wa idara hizo ambao wanapanga mipango ya namna ya kufikisha huduma.

Lakini kuna kundi jingine huwa linasahaulika sana. Bahati mbaya, kundi hili ni muhimu sana. Hili ni kundi la wahudumu wa kujitolea wanaofanya kazi nyingi mbalimbali. Kama kundi hili la watu wa kujitolea lisingekuwepo na kufanya kazi wanazozifanya; basi mazingira ya kazi ya ya wahudumu rasmi wa afya walioajiriwa madaktari, manesi na kadhalika yangekuwa magumu mno.

Leo katika safu hii ya afya nimeona niwaadhimisha watu hawa ambao wametoa mchango mkubwa katika kufanya matendo ya kiutu hapa nchini kwetu. Kama tutataja taasisi na vikundi vinavyofanya kazi hizo za kujitolea katika sekta ya afya, sitashangaa iwapo ya kwanza katika orodha itakuwa ni Jumuiyyatul Akhlaaqul Islam (JAI).

JAI ni taasisi yenye matawi nchi nzima ambayo inahuisha tabia za Kiislamu kwa wanachama wake kutekeleza yale aliyoyaelekeza Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) katika kutoa sadaka, kukirimu watu na kuwasadia wenye shida, hususan wagonjwa.

Tumeandika sana kuhusu shughuli za JAI katika gazeti letu la Imaan na katika makala hii nitatumia taarifa mbalimbali tulizowahi kuzichapa kuielezea kwa ufupi taasisi hii na mchango wake katika kusaidia hospitali, wagonjwa na hata serikali.

Kazi za JAI

Kazi kubwa ya JAI ni kutembelea wagonjwa hospitalini, kuwapa faraja na kuwahudumia kwa mahitaji mbalimbali kama chakula na mengineyo katika miongoni mwa mahitaji ambayo mgonjwa anayategemea kutoka kwa ndugu na jamaa zake.

Kuna wagonjwa ambao hawana ndugu. Kuna wagonjwa ambao wamesuswa na ndugu zao. Kuna wagonjwa ambao wana ndugu lakini ndugu hao hawana uwezo wa kuwahudumia ipasavyo. Hawa wote wamepata faraja kutoka JAI, tena bila ya kujali dini, jinsia au maakabila yao.

Na jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa wanachama wa JAI siyo tu hawalipwi lakini pia hawategemei mfadhili fulani mmoja kuwawezesha kufanya shughuli hizi bali huchangia kutoka mifukoni mwao.

Kutokana na fedha hizo zinazochangwa na wanachama, taasisi ya JAI imeweza kununulia wagonjwa wenye uhitaji vitu muhimu ikiwemo chakula na dawa.

Wanachama wa JAI wameweza kwa kiasi kikubwa kuwapunguzia mzigo wa kazi wauguzi, ambao tayari wameelemewa na kazi. Wanachama wa JAI hufanya usafi siyo tu wa hospitalini bali pia wa wagonjwa wasiojiweza. Kwa kutengeneza mazingira haya mazuri, hata kazi ya madaktari huwa rahisi.

Ukiacha jukumu hilo la kuhudumia wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali, JAI pia wanashughulika na uokozi kipindi cha majanga, uchangiaji damu, usafi na kutunza mazingira. Kazi nyingine ni kusaidia shughuli za mazishi ya watu wasio na ndugu.

Kiasi cha damu amnbayo wanachama wa JAI wamechangia ni nyingi mno, naamini inaweza kufikia hadi chupa laki moja kama tutahesabu yote iliyochangwa tangu taasisi hii ianze kazi zake katika mikoa karibu yote hapa nchini.

Katika kazi ya uokoaji iliyowapa sifa kubwa taasisi ya JAI ni katika ajali ya moto mjini Morogoro iliyosababisha vifo vya karibu watu 100 na majeruhi wengi baada ya lori la mafuta kupinduka, kisha kulipuka. Katika ajali ile, JAI walishiriki kikamilifu katika kusaida waathirika.

Siku ile ya ajali, JAI walifanya mambo mengi ikiwemo kushiriki kubeba maiti na majeruhi na kuwapeleka hospitali, tena kwa kutumia rasilimali zao wenyewe. JAI pia walishiriki kikamilifu katika kuwafariji wafiwa na ndugu wa majeruhi sambamba na kuwanasihi wawe na subira.

Katika mazishi ya pamoja ya kitaifa yaliyofanyika siku ya Eid – al Adh’haa yaliyohudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo viongozi waandamizi wa serikali; ni taasisi hii ya JAI ndiyo ilibeba jukumu la kugawa chakula.

Ingawa siku ile ya ajali ya moto hawakutoa damu, kwa hakika ni damu za wanachama wa JAI zilizotumika kuhudumia wagonjwa kwani wao huwa na utaratibu wa kuchangia damu kila baada ya miezi minne. Kwa kuwa kipindi hicho kilikuwa hakijatimia walishindwa kuchangia kipindi kile.

Mafanikio

Gazeti la Imaan media liliwahi kumhoji Mratibu Mkuu wa Jumuiyyatul Akhlaaqul Islam (JAI) Taifa, Othman Said Massanga ambaye alisema taasisi yao inajivunia mafanikio lukuki.

Jambo kubwa wanalojivunia ni kule kujitoa kwao kutekeleza jambo ambalo ni la kiibada ili tu kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kufuata mafundisho ya Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie).

Sambamba na hilo, JAI imefanikiwa pia kujitanua na kwa kufungua matawi katika mikoa mingi ya Tanzania bara na visiwani, ingawa hamu na mipango yao ni kuona JAI inaenea katika mikoa yote nchini.

JAI kwa sasa inatambulika sana na kuheshimiwa. JAI inaenziwa zaidi na taasisi inazofanya nazo kazi, hususan hospitali. Mara kadhaa JAI imepokea maombi maalumu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuchangia damu, hususan pale madaktari kutoka nje ya nchi wanapowasili kwa ajili ya kufanya upasuaji maalumu.

Pia, katika mafanikio ya JAI, wameokoa maisha ya watu wengi kwa kujitolea damu katika Mpango wa Taifa wa Damu Salama. JAI, hakika, ni mchangiaji mkubwa wa akiba hiyo. Hospitali na Mpango wa Damu Salama wanajua na kutambua mchango huo.

Tuwaunge mkono

Jambo wanalolifanya JAI ni kubwa mno na lina fadhila kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na lina faida kwa jamii, kwa hiyo ni muhimu kuwaunga mkono.

Sisi kama jamii ya Kiislamu na Watanzania kwa ujumla tujitahidi kuongeza upendo tukitambua kuwa binadamu wanategemeana. Pia, tukumbuke kuwa, sote ni wagonjwa watarajiwa kwa hiyo tuwe tayari kujitolea damu ili kuokoa maisha ya wenzetu kwani ipo siku na sisi tutahitaji msaada.

Taasisi ya JAI ni moja tu ya njia za kusaidia watu. Unaweza kujiunga nao, lakini pia unaweza kujiunga na vikundi/taasisi nyingine. Unaweza kufanya wewe binafsi, peke yako. Hata hivyo, kilicho bora ni kujiunga na wengine kwani umoja ni nguvu na msaada wa Mungu upo pamoja na wengi.

Shime Waislamu na Watanzania, tusikubali kushughulishwa na mambo hadi tukasahau wajibu huu kwani hata wanachamna wa JAI nao wana harakati zao nyingine za kimaisha lakini wanatenga muda kutafuta radhi za Muumba wao.

Kuanzishwa kwa Jai

Jumuiya ya JAI, kwa mujibu wa Mratibu Mkuu Massanga, ilianzishwa takriban miaka 13 iliyopita kutekeleza jambo la kidini na kiutu. Jumuiya hii ikitokana na Waumini wa Msikiti wa Taqwa uliopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Waumini hao wa msikiti huo walienda kumtembelea ndugu yao katika Imani waliyekuwa wakisali naye ambaye aliugua na kulazwa katika Hospitali ya Mwananyamala.

Wakiwa hospitalini hapo wakizungumza na ndugu yao, waliona mgonjwa wa jirani kazungukwa na watu wanazungumza naye. Katika kusikiliza, waligundua kuwa wale waliomzunguka ni Wakristo waliokuwa wakijaribu kumritadisha mgonjwa yule ambaye awali alikuwa ni Muislamu.

Pia, waligundua kuwa mgonjwa yule Muislamu hakuwa na ndugu anayemtembelea pale hospitalini na aliishi kwa shida sana, hususan kwa upande wa mahitaji yake kama chakula. Wale waliokuwa wakimshawishi kuritadi walitumia udhaifu wake huu kutaka kumkufurisha kwani ni wao ambao ndiyo waliokuwa wakimtembelea na kumpa zawadi za hapa na pale afuate dini yao.

Baada ya kumlainisha kidogo kidogo kwa zawadi za hapa na pale kwa muda mrefu, siku hiyo ilikuwa ndiyo kilele kwani walifanikiwa kumritadisha na wakaanza kumuombea.

Jambo la kusikitisha ni kuwa punde tu baada ya kuritadishwa na huku wakiwa katikati ya maombi, mgonjwa yule alizidiwa, akaanza kutetemeka, kisha akatulia. Kumbe ndiyo kashakata roho!

Waliomritadisha walipogundua hilo, waliondoka na kumuacha pale. Kwa kuwa Waislamu hawa walikuwa kitanda cha jirani, walisogea kumuangalia na wakagundua kuwa alishakufa. Wakamfuata muuguzi, ambaye naye alimleta daktari kuthibitisha kuwa mgonjwa yule alishafariki.

Katika kutaka kufahamu zaidi, Waislamu wale kutoka Msikiti wa Taqwa walimuuliza yule muuguzi kuhusu taarifa za yule marehemu ambapo aliwathibitishia kuwa tangu aende pale hospitalini hakuwahi kutembelewa na ndugu yoyote.

Tukio hili ndilo lililopelekea Waumini wale kupeleke taarifa msikitini kwao (Taqwa). Viongozi walifuatilia uhakika wa taarifa hizo na ilipothibitika ndipo msikiti ukaadhimia kuanzia siku iliyofuata kutembelea wagonjwa hospitalini na kuwahudumia wale wasiokuwa na uwezo.

Katika kutekeleza hilo, waliazimia kuwa kila mtu ajitoe kwa hali na mali yake, kadri alivyojaaliwa ili kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Misikiti mingine ilivutiwa na harakati zilikuwa za msikiti huu wa Taqwa, na kuamua nao kujiunga na wenzao. Mwaka 2008 walipata usajili rasmi kwa jina la JAI.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only