Dhana ya Uhuru katika Uislamu

 

Uislamu ni dini inayojulikana kwa wepesi wake. Ni dini inayohimiza kusameheana siyo tu miongoni mwa wafuasi wake, bali wanadamu kwa jumla. Uislamu umempa mwanadamu haki ya kujiamulia na kuchagua dini anayotaka kuifuata na itikadi anayotaka kuishikilia.


Uhuru wa itikadi ni msingi muhimu miongoni mwa misingi ya dini hii adhimu kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:


“Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uongofu umekwisha pambanuka dhidi ya upotofu. Basi anayemkataa Shetani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.” [Qur’an, 2:256].


Kulingana na misingi ya Uislamu na mafunzo yake; kutofautiana kikabila, kiitikadi, kilugha, kitabia kunakubalika katika Uislamu.


Ushahidi wa hili ni kauli yake Mwenyezi Mungu Aliyetukuka aliyesema katika kitabu chake kitakatifu:


“Na Mola wako Mlezi angelipenda angewafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana. Isipokuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu; na kwa hiyo ndiyo Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako Mlezi, ‘Kweli kweli nitaijaza Jahannam kwa majini na watu pamoja.’” [Qur’an, 11:118-119].


Pia, Uislamu uliwapa watu uhuru wa kuchagua dini na kufuata sheria ambayo wataridhika nayo kwani masuala ya itikadi yanafungamana na uelewa wa mtu mwenyewe na imani yake.


Mwenyezi Mungu anasema: “Na sema, ‘Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae.” [Qur’an, 18:29].


Katika aya hiyo tuliyoinukuu, Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie) kwamba hana mamlaka ya kuwalazimisha watu kuamini ujumbe wake kwani jukumu lake linaishia katika kuwalingania na kuwaita kwenye njia ya Mwenyezi Mungu.


Kama wanaolinganiwa watakubali, ni vema. Ama wakikataa, basi hakuna mamlaka ya kuwalazimisha kufuata Uislamu.


Ufafanuzi zaidi wa jambo hili unapatikana katika kauli ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:


“Angelitaka Mola wako Mlezi wangeliamini wote waliomo katika ardhi. Je, wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe Waumini?” [Qur’an, 10:99]; na katika kauli yake nyingine: “Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji. Wewe si mwenye kuwatawalia.” [Qu’ran, 88:21-22].


Zaidi ya hayo, Mtume aliamrishwa katika Qur’an aachane na wale waliotangaza kukufuru. Amri hiyo imerudiwarudiwa mara kadhaa, ikiwemo katika Suratul Kafiruun.


Katika Sura hiyo, Mwenyezi Mungu anasema: “Sema: Enyi makafiri!. Siabudu mnachokiabudu. Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Wala Sitaabudu mnachoabudu. Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu.” [Qur’an, 109: 1-6].


Kwa kweli kutofautiana kidini na kiitikadi siyo sababu ya kumzuia Muislamu kuishi na kuamiliana na wengine wasio Waislamu kwa wema na amani. Mwenyezi Mungu amewahimiza Waislamu kuamiliana na watu wote kwa wema na hisani madamu hawakuwafanyia Waislamu uadui wala bughudha. Mwenyezi Mungu anasema:


“Wala kuwachukia watu kwa kuwa walikuzuilieni kufika Msikiti Mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na uchamungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.” [Qur’an, 5:2].


Qur’an Tutufu kupitia aya kadha wa kadha imesisitiza kuwa Waislamu wanatakiwa kuwa na mahusiano mazuri na watu wa dini na itikadi mbalimbali kwani kuna mambo ya pamoja yanayostahiki kuchungwa na wote, Waislamu na wasio Waislamu kwa msingi wa kushirikiana na kukamilishana kwa ajili ya manufaa ya ulimwengu wote.


Kwa kweli Uislamu ulikuja ili kuimarisha mahusiano baina ya watu siyo kuyakata mahusiano hayo.


Jambo la kusisitiza ni lile alilolifanya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) katika Suluhu ya Al-Hudaibiya ambapo alifunga mkataba wa amani wa kwanza kabisa baina ya Waislamu na washirikina kwa msingi wa kuheshimiana na kuamiliana kwa wema ili kuwe na amani na utulivu kwa manufaa ya jamii na ili kuilinda nchi.


Ingawa masharti ya mkataba huo yalionekana yanawadhulumu Waislamu na kupendeleza washirikina, Mwenyezi Mungu aliuita mkataba kuwa ni wa ushindi kama ilivyokuja katika kauli yake Aliyetukuka:


“Hakika tumekufungulia Ushindi wa dhahiri. Ili Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako yaliyotangulia na yajayo, na akutimizie neema zake, na akuongoe katika Njia iliyonyooka. Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu.” [Qur’an, 48: 1-3].


Mkataba wa Hudaibiya unathibitisha kuwa Uislamu ndiyo dini ya amani na utulivu; na Uislamu kamwe siyo dini ya ugaidi na vurugu.


Ikumbukwe kuwa, baada ya suluhu ya Hudaibiya, ilitokea vita vya Khaybar baina ya Waislamu na Mayahudi; na Mtume aliingia katika makubaliano mengine na Wayahudi kwa ajili ya kuzilinda nafsi na damu za pande mbili.


Si hivyo tu, kuanzia mwaka wa saba baada ya Hijra ya Mtume, misafara ya mabalozi wa Waislamu waliokuwa wanatumwa na Mtume huku na huku ili kueneza ujumbe wa amani na kuanzisha mahusiano na mataifa mbalimbali kwa lengo la kuthibitisha kuwa dini hiyo ni dini ya amani na upendo.


Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikubali zawadi alizozipata kutoka kwa wafalme wa mataifa mengine kama vile Najash, aliyekuwa Mfalme wa Uhabashi.


Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwafanyia wajumbe wa Mfalme Najash ukarimu mkubwa akisema:


“Hakika watu hawa waliwafanyia Maswahaba zetu ukarimu mkubwa.”


Inatajwa pia kwamba Uislamu unawahimiza Waumini kuhifadhi mahusiano yao wenyewe kwa wenyewe na kuwafananisha na mwili mmoja kama ilivyokuja katika Hadith ya Mtume:


“Kwa kweli mfano wa Waumini katika upendo na huruma baina ya wao wenyewe kwa wenyewe ni kama mwili mmoja. Kama kiungo kimoja kinauma, basi mwili mzima huumwa na kutaabika.”


0 Comments