October 16, 2020

Hakika umeniamrisha jambo jema, nami nitakutii

 


Ibnu Abdil–barri (Allah amrehemu) amesema: “Niliwasikia masheikh zangu wakisema kuwa Alghaazi bin Qays (Allah amrehemu) alisafiri kwenda Madina kujifunza hadithi kwa Imam Malik (Allah amrehemu).

Akiwa huko alikutana na Naafi’u, mmoja wa wanazuoni wa Qirati za Qur’an ambaye alimfundisha Qur’an Tukufu. Muda mfupi baada ya Alghaazi kuingia ndani ya msikiti wa Mtume (Madina), alitokea Ibnu Abi Dhuayb, kisha akaketi pasina kuswali (rakaa mbili za Tahiyyatul Masjid).”

Alghaazi akamwambia: “Simama uswali rakaa mbili kwani kukaa kabla ya kuswali Tahiyyatul Masjid ni ujinga.”

Ibn Abi Dhuayb akanyanyuka ghafla na kuswali rakaa mbili. Alipomaliza kusali aliketi chini na kuegemeza mgongo wake ukutani huku watu wakiwa wamemzunguka wakisubiri kuanza kwa darasa mduara (halqa).

Alghaazi alipoona hali hiyo akauliza: “Ni nani huyu?” akaambiwa: “Huyo ni Ibn Abi Dhuayb, mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Fiqh wanaoheshimika sana katika mji wa Madina.”

Baada ya kusikia hivyo, Alghaazi alisimama na kumuomba msamaha Ibn Abi Dhuayb. Abi Dhuayb akamwambia:

“Ewe ndugu yangu, hakuna lawama yoyote juu yako kwani umeniamrisha jambo jema nami nitakutii.” [Ibnu Abdil barri – Tamhiid, uk. 106/20].

Mafunzo ya tukio

Unyenyekevu Unyenyekevu ni hali ya kujishusha mbele ya wengine, hasa watu wakubwa au wale wanaostahiliheshima ya pekee. Kwa maneno mengine, unyenyekevu ni tabia inayodhihirisha usafi wa nafsi na kuleta amani, upendo na mafungamano ya kindugu miongoni mwa watu.

Mtu mnyenyekevu hajikwezi wala kujitenga na watu na mara zote huwa tayari kuwasaidia watu bila kujali tofauti ya dini zao, makabila yao, rangi zao au maeneo watokako.

Kiburi ni kinyume cha unyenyekevu

Kiburi, maana yake ni kupenda ufahari, kuwa na dharau na kujiona bora kuliko wengine. Mtu mwenye kiburi hupenda kujikweza hata kwa sifa asizokuwa nazo.

Unyenyekevu ni sifa ya wanazuoni

Miongoni mwa tabia ambazo kila Muislamu anapaswa kujipamba nazo ni unyenyekevu. Historia inaonesha kuwa, Maswahaba wa Mtume (Allah awaridhie wote) walipewa hadhi ya kuwa watu bora baada ya Mtume kutokana na unyenyekevu wao mkubwa waliouonesha mbele ya Allah Aliyetukuka na Mtume wake.

Mwanazuoni mnyenyekevu hutambua kuwa wakati wowote anaweza kusahau, pia hujiona ana elimu ndogo hata kama amefikia elimu ya chuo kikuu. Allah Mtukufu anasema:

“Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.” [Qur’an 17:85].

Imam Malik ni miongoni mwa wanazuoni wa kupigiwa mfano katika hili. Imeelezwa kuwa Abu Ja’afar Al–mansuur (Khalifa wa pili katika dola ya Abbasiyya) alikwenda Makka kwa ajili ya ibada ya hijja akakutana na Imam Malik (Allah amrehemu) na kumwambia:

“Nimedh a m i r i a kutoa nakala nyingi za kitabu cha Al– Muwatta na kuvip e l e k a katika kila mji ili watu wafanyie kazi yaliyomo ndani yake na wasishughulike na mambo mengine, kwani mimi naonelea kuwa asili ya elimu ni riwaya ya watu wa Madina.”

Imam Malik akamwambia Ja’afar: “Usifanye hivyo ewe Amir, kwani watu wameshatanguliwa na kauli mbalimbali na wameshasikia hadithi nyingi za Mtume, na wameshashika yale yaliyotangulia kuwafikia na kuyaandika, zikiwemo kauli za Maswahaba. Waache watu wabaki na yale waliyoyachagua wenyewe katika miji yao.”

Imam Malik akasema: “Naapa k u w a kama ungenitii basi ningeamrisha jambo hilo.” Ibnu AbdilBarri ambaye ni mpokezi wa kisa hiki amesema: “Huu ni upeo wa juu kabisa wa uadilifu.” [Ibnu Abdulbarri – Tamhiid].

Njia ya kupata radhi za Allah

Unyenyekevu ni njia bora zaidi ya kupata radhi za Allah. Mwenyezi Mungu amea – hidi kuwanyanyua wale wenye kunyenyekea kwake na kuwadhalilisha wanaojikweza.

Tunasoma katika Qur’an Tukufu kuwa, mja mwema wa Allah, Luqman alimuusia mwanae kwa kumwambia:

“Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi mwenye kujivuna na kujifahirisha.” [Qur’ an, 31:18].

Na katika hadithi, Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) amesema: “Kutoa sadaka hakupunguzi mali. Allah humzidishia mja ‘izzah’ (utukufu) kwa ajili ya kusamehe kwake. Na yeyote anayenyenyekea kwa ajili ya Allah, Allah Aliyetukuka atampandisha daraja (atamtukuza).” [Sahihul jaami’I, uk. 5809].

Kadiri mtu anavyotoa sadaka, Allah humlipa malipo mema kama anavyosema:

“Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amrudishie maradufu na apate malipo ya ukarimu.” [Qur’an, 57:11].

Kwa ushahidi huo, ni wazi kuwa, Allah humnyanyua na kumpa heshima, hadhi na utukufu mtu anayenyenyekea kwake na kutoa sadaka.

Sifa ya Mitume na waja wema

Allah ‘Azza Wajallah’ ametaja sifa nyingi miongoni mwa sifa za waja wema kwa kusema:

“Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanaotembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu, ‘Salama!’” [Qur’an, 25:63].

Allah amewasifu watu hawa baada ya kujitakasa na tabia mbaya ya kujikweza na kuwadharau wengine. Allah anasema:

“Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.” [Qur’ an, 17:37].

Unyenyekevu ni sifa muhimu ya kiutendaji ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuwa nayo ili imsogeze karibu na wanadamu wenzake. Ni muhali kabisa mtu kuwa mnyenyekevu ikiwa moyo wake hauna chembe ya huruma, kwani hisia za huruma ndizo zinazomfanya mtu kuwa mpole na mnyenyekevu kwa watu.

Ni bayana kwamba palipotawaliwa na chuki na visasi, hapana huruma na pasipo na huruma, hapana unyenyekevu. Hii ndiyo sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu ametukataza kuwatukana washirikina na makafiri ili wasimtukane Mwenyezi Mungu.

Maisha ya nyumbani

Mama wa Waumini, Aisha (Allah amridhie) alipoulizwa kuhusu mwenendo wa Mtume pindi awapo nyumbani alisema:

“(Mtume) alikuwa mtu wa kawaida, anafua nguo zake na kukamua mbuzi wake maziwa.”

Kisha Mtume akasema kuwaambia Maswahaba zake: “Hakika Mwenyezi Mungu ameniteremshia wahyi ya kwamba muwe wanyenyekevu ili asijifaharishe mmoja wenu juu ya mwingine na kumfanyia uovu mwenzake.” [Taz: ‘Sahihul – adabul mufrad,’ uk. 420].

Upole katika kulingania

Upole humfanya mtu kuwa mnyenyekevu katika kulingania. Katika tukio hili, tumeshuhudia Imam Alghaazi Ibnu Qays (Allah amrehemu) akitamka maneno mazito kwa Ibnu Abi Dhuayb pasina kutambua kuwa Abi Dhuayb ni mwanachuoni mkubwa katika mji wa Madina. Hatimaye, Alghaazi alisimama na kumuomba Ibnu Abi Dhuayb msamaha.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only