October 8, 2020

HRW: Waislamu Warohingya wanaishi kwenye 'jela ya wazi' na katika "unyonge na udhalili"

 


Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema, Waislamu wapatao 130,000 wa jamii ya Rohingya waliosalia kwenye kambi za wakimbizi zilizoko kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar wanaishi katika mazingira ya unyonge na udhalili. Human Rights Watch imeihimiza serikali ya nchi hiyo ikomeshe haraka uwekaji kizuizini huo wa kiholela na usio na mwisho wa watu hao.


Katika ripoti liliyotoa leo, shirika hilo la kuteeta haki za binadamu limesema, mazingira wanayoishi Waislamu hao waliowekwa kizuizini kwa umati ni mithili ya "jela ya wazi".


Mwandishi wa ripoti hiyo, Shayna Bahchner amesema, "serikali ya Myanmar imewafungia kwa muda wa miaka minane Warohingya 130,000 katika mazingira yasiyo ya kiutu na kuwatenganisha na makazi, ardhi na maisha yao, huku kukiwa na matumaini madogo ya hali waliyonayo kuboreka."


Ripoti hiyo ya kurasa 160 iliyotolewa na Human Rights Watch imeeleza kuwa, makumi ya maelfu ya Waislamu wa Rohingya wanaoishi kwenye kambi za wakimbizi wa ndani na kwenye maeneo mithili ya kambi, wanawekewa vizuizi vya kupindukia katika harakati na shughuli zao za maisha.


Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limetoa mwito kwa jamii ya kimataifa wa kuitaka itoe mashinikizo zaidi kwa serikali ya Myanmar na kuwawajibisha viongozi wa serikali hiyo waliohusika na uhalifu dhidi ya Waislamu hao.

"Maisha makambini ni ya kuhuzunisha sana... Hakuna fursa ya kutembea kwa uhuru, hatuna kitu kinachoitwa uhuru", ameeleza Muislamu mmoja wa jamii ya Rohingya kama alivyonukuliwa katika ripoti ya Human Rights Watch.


Kati ya Warohingya zaidi ya 250,000 waliosalia nchini Myanmar, kwa uchache laki moja miongoni mwao wamekuwa wakiishi kwenye kambi za ndani tangu walipopoteza makazi yao wakati wa wimbi la machafuko ya mwaka 2012.


Serikali ya Myanmar inaamiliana na Waislamu Warohingya kama watu wasio na uraia na haiko tayari kuwapatia wananchi hao haki yao hiyo. Mauaji ya halaiki yaliyofanywa na jeshi la Myanmar na mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka dhidi ya Warohingya yamewalazimisha Waislamu wengi wa jamii hiyo kuhama eneo la makazi yao ya asili la Rakhine na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.../

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only