October 24, 2020

Qur'ani tukufu yavunjiwa heshima tena nchini Sweden


Vijana kadhaa wa Sweden wenye misimamo ya kufurutu mpaka wamefanya kitendo cha kishenzi cha kuivunjia heshima Qur'ani tukufu kwa kuchukua msahafu na kuuchoma moto mbele ya jengo la bunge la nchi hiyo.


Mwanaharakati mmoja mwanamke wa Kiislamu amesambaza mkanda wa video kwenye mitandao ya kijamii unaoonyesha kitendo hicho cha kishenzi na akawatolea mwito Waislamu kuilinda Qur'ani takatifu na dini yao tukufu ya Uislamu.


Katika mkanda huo wa video, askari polisi wa Sweden, ambao huwepo muda wote mbele ya jengo la bunge la nchi hiyo, hawaonekani kuchukua hatua yoyote ya kuwazuia vijana hao wasiivunjie heshima Qur'ani tukufu.


Kitambo si kirefu nyuma, mwanachama mmoja wa chama chenye misimamo ya kufurutu ada nchini Denmark naye pia alifanya kitendo cha kishenzi cha kuivunjia heshima Qur'ani kwa kuuchoma moto msahafu katika eneo la watu wenye misimamo ya ubaguzi wa rangi la Rinkeby, katika mji mkuu wa Sweden, Stockholm.


Msahafu mwengine ulichomwa moto katika maandamano haramu na yasiyo na kibali yaliyofanywa na makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo ya kufurutu mpaka katika mji wa Malmo nchini Sweden mnamo Agosti 28 mwaka huu.


Kitendo hicho kililaaniwa vikali katika nchi za Kiislamu.


Katika miezi ya karibuni Sweden imeshuhudia matukio kadhaa ya hujuma na mashambulio dhidi ya Waislamu, maeneo yao matakatifu na kuvunjiwa heshima pia kitabu kitukufu cha Qur'ani.../

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only