Waislamu wenye hasira waandamana Bangladesh wakitaka bidhaa za Ufaransa zisusiwe

Makumi ya maelfu ya Waislamu wa Bangladesh wamefanya maandamano katika mji mkuu Dhaka, kulaani hatua ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ya kuunga mkono kitendo cha kifidhuli cha jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.


Huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kutaka kususiwa bidhaa za Ufaransa, waandamanaji hao waliokuwa na ghadhabu wamechoma moto picha za Macron na bendera za nchi hiyo ya Ulaya.


Kadhalika waandamanaji hao wametoa mwito wa kuwajibishwa Rais Macron, kutokana na matamshi na misimamo yake ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.


Jeshi la Polisi la Bangladesha linakadiria kuwa, watu elfu 40 walishiriki maandamano hayo ya jana Jumanne mjini Dhaka, yaliyoitishwa na chama cha Kiislamu nchini humo cha Islami Andolan Bangladesh (IAB).


Maandamano hayo yalianzia katika Msikiti wa Jamia wa Baitul Mukarram jijini Dhaka, na kuishia karibu na ofisi za Ubalozi wa Ufaransa nchini humo, ambapo waandamanaji wamekabidhi waraka wa kukosoa matamshi ya Macron dhidi ya Waislamu na hatua ya rais huyo wa Ufaransa ya kuufungamanisha ugaidi na Uislamu.


Hatua hiyo ya Macron imelaaniwa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu, huku kampeni ya kususia bidhaa za Ufaransa katika mataifa hayo ya Kiislamu ikishika kasi.

0 Comments