November 2, 2020

Kukosolewa mwenendo wa sera za chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa


Kushadidi utendaji ulio dhidi ya Uislamu barani Ulaya hususan nchini Ufaransa katika majuma ya hivi karibuni siyo tu kwamba, kumewakasirisha Waislamu ulimwenguni kote, bali hata viongozi na wanasiasa wa nchi hiyo wameonyesha radiamali zao kwa hatua hiyo.


Ukosoaji wa chuki dhidi ya Uislamu umeshadidi kufuatia hatua ya jarida la Charlie Hebdo la kuchapisha tena vikatuni vinavyomvunjia heshima Bwana Mtume SAW na hatua ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo ya kutetea kitendo hicho kichafu, Kuhusiana na jambo hilo, Francois Hollande Rais wa zamani wa Ufaransa ametahadharisha kuwa, magaidi hawapaswi kuchanganywa na Waislamu na kwamba, magaidi wanafuatilia suala la kuanzisha vita vya kidini.


Kufanywa mashambulio ya kigaidi na kushambuliwa maeneo ya kidini kama makanisa, kumekuwa kisingizio cha viongozi wa Ufaransa cha kushadidisha misimamo yao ya chuki dhidi ya Uislamu na kuzifanyia dhihaka itikadi za Waislamu barani Ulaya hususan nchini Ufaransa sambamba na kuongeza mashinikizo dhidi ya Waislamu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo ya kufurutu ada.


Hii ni katika hali ambayo, uchunguzi wa kimahakama umethibitisha katika matukio mengi juu ya kutokuwa na ukweli wowote madai hayo. Kama ambavyo shambulio la kigaidi katika mji wa Avignon kusini mashariki mwa Ufaransa ambapo polisi mmoja aliuawa imefahamika kuwa, lilitekelezwa na Harakati ya Mrengo wa Kulia wa Kutetea Ulaya'. Mshambuliaji akiwa na silaha baridi sambamba na kumtishia mfanyabiashara mmoja wa Kimorocco na maafisa wa polisi katika barabara moja mjini Avignon aliwashambulia pia.


Katika hali ambayo, viongozi wa Ufaransa hususan Rais Emmanuel Macron wamechukua misimamo dhidi ya Waislamu na wamo mbioni kukuza chuki dhidi ya Uislamu, makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo mikali barani Ulaya hususan Ufaransa, yakipinga utendaji wa viongozi pamoja na anga ya kisiasa na kiuchumi inayotawala hivi sasa barani humo yamejiimarisha na hivi sasa yanatumia uwepo wa Waislamu kama kisingizio cha kuhalalisha mapungufu na matatizo ya sasa ya viongozi wa Paris.

Masoud Shajareh, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu (IHRC) nchini Uingereza anasema: Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameamua kuushambulia waziwazi Uislamu kwa kusema, Uislamu uko katika mgogoro katika hali ambayo, ukweli wa mambo ni kuwa, sera za Ufaransa na wanasiasa wa Ulaya wenye mtazamo sawa na wake, ndio ambao wamo katika mgogoro. Kutokana na ufisadi huu, Macron hana budi kuelekeza nguvu zake kuliko wakati mwingine wowote katika suala la ubaguzi wa rangi na  chuki dhdi ya Uislamu, ili kwa njia hiyo aweze kujipatia kura za makundi na watu wa mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu ada.


Msimamo wa Rais Macron na serikali yake unaendelea katika hali ambayo, kushadidi misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu na kuendelea kutusiwa na kuvunjiwa heshima Uislamu na Waislamu hususan Bwana Mtume SAW, kivitendo hilo limepelekea kuongezeka ukosefu wa amani na uchochezi dhidi ya makundi ya kufuruta ada na kuyasukuma yatekelekeze vitendo vya ugaidi.

Ahmad Tayyib, Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar cha Misri ameitaka jamii ya kimataifa ipasishe sheria ambayo itatambua kuwa, chuki dhidi ya Uislamu na kueneza chuki baina yao na dhidi ya wengine ni kosa na uhalifu na watakaokiuka sheria hiyo waadhibiwe. Aidha amewataka Waislamu kufungamana na mbinu na mikakati ya amani na njia za kisheria katika kutetea dini na Mtume wao SAW.


Ukweli wa mambo ni kuwa, Ufaransa badala ya kukubali kubeba dhima ya yaliyopelekea kutokea anga hii kutokana na kusaidia kueneza ugaidi Asia Magharibi, kushiriki katika vita na kuleta ukosefu wa amani katika eneo na vilevile katika eneo la Sahel Afrika, filihali wamo mbioni kukuza misimamo ya kufurutu ada kwa kutumia visingizio visivyo na msingi wowote na kuchukua hatua kama za kuwafukuza Waislamu na kufunga misikiti.


Licha ya kushadidi chuki dhidi ya Uislamu na kutetea vitendo vichafu vya kumvunjia heshima Bwana Mtume SAW kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa maoni kunakofanywa na viongozi wa Ufaransa na baadhi ya viongozi wa Ulaya, lakini inaonekana kuwa, mbinu hii siyo tu kwamba haikubaliwi na shakhsia na watu huru ulimwenguni, bali ukweli ni kuwa, utendaji huu unafanyika kwa minajili ya kufunika na kuficha mambo na kujaribu kuhalalisha hatua na siasa zisizo na busara za Wamagharibi.


Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only