November 23, 2020

Uhalisia wa maisha ya Muislamu

 


Allah ‘Azza Wajallah’ ametupigia mfano mzuri katika suala la kumcha Yeye pale aliposema: “Je, huoni vipi Allah amepiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara na matawi yake yanafika mbinguni (ni marefu mno). Unatoa mazao yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Allah anapiga mifano kwa watu ili wapate kukumbuka.” [Qur’an, 14:24–25].


Mti uliopigiwa mfano katika aya hii, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ameuelezea kuwa ni mtende. Na imepokewa kutoka kwa Abdullahi bin Umar (Allah amridhie) akisema, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alituambia:


“Hakika miongoni mwa miti, kuna mti mmoja ambao majani yake hayaanguki wakati wa joto wala baridi, na hutoa matunda yake kila mara kwa idhini ya Mola wake. Kwa hakika mti huo ni kama alivyo Muislamu. Nitajieni jina la mti huo. Watu wakataja miti mbalimbali ya mashambani.”


Ibn Umar akasema: “Niliufikiria kuwa ni mtende, lakini niliona aibu kujibu kutokana na hadhi ya Maswahaba wakubwa (Abubakr na Umar) waliokuwepo katika kikao kile.” Maswahaba wakamwambia Mtume: “Tufahamishe ni mti gani huo ewe Mjumbe wa Allah?” Mtume akasema: “Ni mtende.” [Bukhari na Muslim].


Katika hadith hii, Mtume amebainisha wazi kuwa mti madhubuti ambao una manufaa ya kudumu ni mtende na akaufananisha na Muislamu. Hivyo ndivyo alivyopiga mfano Mtume kuhusu mti wa mtende.


Mtende una manufaa makubwa

Mtende ni mti mzuri ambao mizizi yake ni imara na madhubuti sana. Hivyo ndivyo alivyo Muislamu mwenye imani thabiti, madhubuti na imara. Pamoja na kuwa ni tunda lenye ladha tamu na nzuri mdomoni, mti wa mtende una faida nyingine nyingi, ikiwamo ya matunda mazuri na matamu, kivuli cha kudumu, pia kokwa zake ni chakula cha ngamia.


Tende huliwa kipindi cha baridi na joto zikiwa mbichi au zimeiva. Pia tende husindikwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ameufananisha mtende na Muislamu katika manufaa haya.


Na kama tujuavyo, kitu kinachopigiwa mfano huwa na taathira kubwa kuliko kile kinachofananishwa. Kwa hivyo, Muislamu anapaswa kuwa na manufaa zaidi kwa watu kuliko mtende, ndio maana mtende ukafananishwa naye.


Manufaa ya Muislamu ni ya kudumu ukilinganisha na mtende ambao majani yake hudondoka. Muislamu anapaswa kuvaa vazi la uchamungu na kutoa huduma kwa jamii popote alipo.


Muislamu ni kama nyuki katika utendaji wake

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amemfananisha Muislamu na nyuki kwa kusema: “Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu ipo mikononi mwake, mfano wa Muumini ni kama mfano wa nyuki, anakula kilicho kizuri na anazaliasha kizuri, na akitua havunji wala hafanyi uharibifu, anatua kwenye matawi na maua havunji wala kuharibu.” [Ahmad]


Na katika riwaya nyingine Mtume amesema, mfano wa Muumini ni kama nyuki, hazalishi isipokuwa kizuri. Nyuki huzalisha kinywaji chenye manufaa makubwa kwa watu.


Allah anasema: “Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki: Jitengenezee nyumba yako katika milima na katika miti na katika wanayojenga watu. Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizofanywa nyepesi kuzipita. Na katika matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbalimbali. Ndani yake kina matibabu kwa wanadamu. Hakika katika haya ipo ishara kwa watu wanaofikiri.” [Qur’an, 16:68–69].


Haya ni manufaa makubwa yanayopatikana kutokana na mdudu huyu (nyuki). Muislamu amefananishwa na nyuki ili awanufaishe watu na kuwaepushia madhara katika maisha yao.


Chumo la Muislamu ni la halali

Mtume anatufahamisha kuwa nyuki huzalisha asali nzuri na hatui isipokuwa katika mmea mzuri au kwenye maua. Mfano huu unapaswa kuchukuliwa na kila mmoja wetu kama mfano wa jinsi Muislamu anavyotakiwa awe. Muislamu anatakiwa ahakikishe chumo lake ni la halali na hazalishi isipokuwa vya halali ambavyo vinamnufaisha yeye pamoja na watu wengine.


Kama tulivyoeleza awali, nyuki hufanya kazi yake kwa ufanisi wa hali ya juu na ushirikiano wenye manufaa makubwa kwake na kwa viumbe wengine. Kwa kutumia mfano huo, Muislamu anatakiwa asimamie majukumu yake kwa ukamilifu na afanye kazi yake kwa ufanisi wa hali ya juu ili iwe na tija kwake na kwa watu wengine.


Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu anapenda mmoja wenu anapofanya jambo, alifanye kwa ufanisi.” [Sahihul Jaami’ I].


Kazi yoyote inayomuingizia muislamu kipato cha halali huzingatiwa kuwa ni ibada yenye malipo makubwa, hivyo inapaswa kufanywa kwa weledi, ufanisi na umakini mkubwa. Mtume amesema:


“Hakuna Muislamu atakayepanda mazao au mimea kisha ndege, binadamu au mnyama akala sehemu ya mazao hayo, isipokuwa itakuwa ni sadaka kwake.” [ Bukhari].


Allah ametuwajibisha kufanya wema katika kila jambo. Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kufanya mambo ya kheri na kujitenga na mabaya, katika hali ya siri na uwazi. Vishawishi vinavyoweza kumtoa mtu katika uongofu ni vingi. Miongoni mwa vishawishi hivyo ni kukithirisha maasi, kufuata matamanio ya nafsi, na kadhalika.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only