000-Swahiyh Twibbin-Nabawiy: Utangulizi Wa Mwandishi

 Swahiyh Twibbin-Nabawiy

 

 

000-Utangulizi:

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

Kwa hakika Himdi Anastahiki Allaah, tunamhimidi tunamtaka msaada, tunamuomba maghfirah, na tunajikinga kwa Allaah kutokana na shari za nafsi zetu, na kutokana na uovu wa matendo yetu.  Mwenye kuhidiwa na Allaah hakuna wa kumpotoa, na aliyeachwa kupotea hakuna wa kumhidi.

 

Na nashuhudia kuwa hapana muabudiwa wa haki ila Allaah Peke Yake Hana mshirika. Na nashuhudia kuwa Muhammad ni mja Wake na Rasuli Wake.

 

Ama baada ya utangulizi huo:  Mtazamo wa Uislamu kwenye Tiba Una pande mbili.

 

Kwanza: Mtazamo wa Uislamu kwa mwana Aadam; Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amejaalia kuwa mwana Aadam ni Khalifa katika ardhi.[1]

 

 

وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي جَاعِلٌ فِي الْأَرْضِ خَلِيفَةً ۖ قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ وَنَحْنُ نُسَبِّحُ بِحَمْدِكَ وَنُقَدِّسُ لَكَ ۖ قَالَ إِنِّي أَعْلَمُ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٣٠﴾

Na pindi Rabb wako Alipowaambia Malaika: “Hakika Mimi Nitaweka katika ardhi khalifa.” [Al-Baqarah: 30]

 

Na kadhalika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemtukuza mwana Aadam. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

  

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا ﴿٧٠﴾

Na kwa yakini Tumewakirimu wana wa Aadam, na Tukawabeba katika nchi kavu na baharini, na Tukawaruzuku katika vizuri na Tukawafadhilisha juu ya wengi miongoni mwa Tuliowaumba kwa ufadhilisho mkubwa. [Al-Israa: 70]

 

 

Na Amemdhalilishia vilivyomo duniani ili aiamarishe kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika Suwrat Al-Baqarah:

 

هُوَ الَّذِي خَلَقَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا 

Yeye Ndiye Ambaye Amekuumbieni vyote vilivyomo ardhini [Al-Baqarah: 29]

 

Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَلَمْ تَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَأَسْبَغَ عَلَيْكُمْ نِعَمَهُ ظَاهِرَةً وَبَاطِنَةً ۗ وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلَا هُدًى وَلَا كِتَابٍ مُّنِيرٍ ﴿٢٠﴾

Je, hamuoni kwamba Allaah Amekuitishieni vile vilivyomo mbinguni na vile vilivyomo ardhini, na Akakutimizieni kitimilifu neema Zake kwa dhahiri na siri?  Na miongoni mwa watu wako wanaobishana kuhusu Allaah bila ya elimu yoyote ile, na bila ya mwongozo wowote ule, na bila ya kitabu chochote kile chenye nuru.  [Luqmaan: 20]

 

Na kauli yake Allaah (Ta’aalaa):  

 

اللَّـهُ الَّذِي سَخَّرَ لَكُمُ الْبَحْرَ لِتَجْرِيَ الْفُلْكُ فِيهِ بِأَمْرِهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴿١٢﴾

Allaah Ambaye Amekutiishieni bahari ili zipite merikebu humo kwa amri Yake, na ili mtafute katika fadhila Zake na ili mpate kushukuru.

 

وَسَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مِّنْهُ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴿١٣﴾

Na Amekutiishieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini vyote humo. Hakika katika hayo bila shaka kuna Aayaat (hoja, dalili, ishara) kwa watu wanaotafakari. [Al-Jaathiyah 12-13]

 

 

Thamani hii kubwa ya mwana Aadam, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameizungushia funiko madhubuti la dhamana na vizuizi vya kutendewa uadui isipokuwa kwa haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Amefanya lile kosa la kumfanyia uadui mwana Aadam kama kwamba ni sawa na kufanya uadui kwa wana Aadam wote kama tusomavyo katika Suwrah Al-Maidah:

 

مِنْ أَجْلِ ذَٰلِكَ كَتَبْنَا عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنَّهُ مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا ۚ  

Kwa ajili ya hivyo, Tukawaandikia shariy’ah wana wa Israaiyl kwamba; atakayeiua nafsi bila ya nafsi (kuua), au kufanya ufisadi katika ardhi; basi ni kama ameua watu wote. Na atakayeiokoa kuihuisha, basi ni kama amewaokoa watu wote.  [Al-Maaidah: 32]

 

 

Na dhamana hizi, zimeelezwa na wanazuoni kuwa ni (Dharura Tano) na Ummah wote umeafikiana kuwa Shariy’ah imewekwa kwa ajili ya kuhifadhi mambo haya matano.

 

Al-Imaam Al-Shaatwiby (Rahimahu Allaah) amesema: “Kwa hakika Ummah umewafikiana, bali hata watu wa dini nyingine kuwa Shariy’ah imewekwa kwa lengo la kuhifadhi mambo hayo matano ‘Adh-Dhwaruriyyaat Al-Khamsah’ ambayo ni Dini, nafsi, kizazi, mali na akili, na ni lazima yajulikane kwa ummah wote kuwa ni mambo ya msingi…” [Al-Muwafaqaat (1/31)]

 

 

Na elimu ya Tiba ni katika njia kuu za kuhami nafsi, uzao, akili, na kulinda vitu hivyo ni haki ya kiwiliwili iliyo juu ya mtu. Kama walivyofahamu As-Salaf As-Swaalih (wema waliotangulia)

 

 

Imepokewa kutoka kwa Abuu Jahiyfah Wahab Ibn Abdillaah amesema:

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliunga udugu kati ya Salmaan Al-Farsiy na Abuu Dardaai. Siku moja Salmaan akamtembelea Abuu Dardaai akamkuta Ummu Dardaai na mavazi yasio maridadi (kama vile nguo za mfanyakazi). Salmaan akamuuliza: “Una nini”? (Ummu Dardaai) akasema: “Ndugu yako, huyu Abuu Dardaai hana haja na dunia.” (hamkurubii).  Alipokuja Abuu Dardaai akamtengenezea chakula Salmaan na akamwambia: “Kula, mimi nimefunga.” Salmaan akajibu: “Mimi sitokula mpaka wewe ule.” Basi akala, ilipokuwa usiku Abuu Dardaai akawa anasimama kufanya ‘ibaadah. Salmaan akamwambi: “Lala.” Akalala, kisha akawa anasimama tena kutaka kufanya ‘ibaadah, akamwambia: “Lala.”  Ilipokuwa mwishoni mwa usiku Salmaan alimwambia: “Sasa simama.” Wakaswali wote pamoja, Salmaan akamwambia Abuu Dardaai: “Rabb wako ana haki juu yako, na nafsi yako ina haki juu yako na mkeo ana haki juu yako, basi mpe kila mwenye haki haki yake”. Akamwendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na akamsimulia hayo,  kisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akasema: “Amesema kweli Salmaan”  [Al-Bukhaariy 1968]

 

Waislamu wametambua umuhimu wa Tiba na thamani yake ukilinganisha na elimu mbali mbali; hivyo wakaiwekea umuhimu, wakasisitiza umuhimu wake, na ulazima wa kuifundisha na kujifundisha.

 

Imepokewa kutoka kwa ‘Urwah bin Az-Zubayr; kwamba alikuwa akimwambia Ummul-Muuminiyn ‘Aaishah bint As-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhaa). “Ee Mama yangu![2] Sishangai ufahamu wako; nasema: Mke wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na bint wa Abuu Bakr na sioni ajabu kutokana na ujuzi wako wa mashairi na masiku za watu; nasema: Bint wa Abuu Bakr na alikuwa katika wajuzi mno wa watu, lakini nastaajabu kutokana na elimu yako ya Tiba, vipi elimu hiyo, wapi umeipata?”

 

Kisha akasema huku akampiga kwenye mabega yake: “Ee ‘’Uryah!”[3]  “Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaugua mwishoni mwa umri wake ikawa makundi ya Waarabu kutoka pande mbali mbali yakimjia na kumpa aina mbalimbali za dawa, na nikawa ninamtibu kwa dawa hizo, basi ni kutokana na kisa hicho (ndipo nikajua Tiba)” [Hadiyth Hassan, imepokewa na Ahmad (6/67), na kutoka kwa Abuu Nu’aym katika ‘Al-Hilyah’ (2/50) na Adh-Dhahabi katika kitabu chake ‘As-Siyar’ (2/182) kwa isnaad yenye udhaifu ndani yake]

 

Ameeleza vema Imaam Al-Muttwalibiy Muhammad bin Idriys Ash-Shaafi’iy (Rahimahu Allaah) mlango huu wa Tiba, kwa namna ambayo imekuja kuwapa tabu sana waliokuja baada yake kwani Imaam Ash-Shaafi’iy alikuwa anajua vema elimu ya Tiba.

 

Imaam Adh-Dhahaby (Rahimahu Allaah) amesema, “Katika baadhi ya fani za Imaam huyu ni fani ya Tiba, kwani aliielewa vema’ [As-Siyar (10/56)]

 

Imaam Ash-Shaafi’iy (Rahimahu Allaah) alikuwa akisema: “Elimu ni aina mbili, elimu ya Fiqh kwa mambo ya Dini na elimu ya Tiba kwa ajili ya kiwiliwili. Na yasiyokuwa hayo ni ufasaha wa baraza” [Manaaqib Ash-Shafi’iy ya Al-Bayhaqiy (2/114)]

 

Na amesema: “Usikae kwenye mji usiokuwa na mwanazuoni anayeweza kufutu maswali ya Dini yako wala tabibu anayekuelimisha kuhusu mwili wako.” [Aadaab Ash-Shaafi’iy wa-Manaaqibihi cha Ibn Abiy Haatim (Uk. 323) na Manaaqib Ash-Shaafi’y (2/115)]

 

 

Na kwa ajili hii, Imaam Ash-Shaafi’iy aliwakosoa Waislamu wengi kwa kupuuzia elimu hii yenye manufaa.

 

Imepokewa kutoka kwa Harmalah, amesema nimemsikia Ash-Shaafi’iy akisema: “Mambo mawili wameghafilika nayo watu, elimu ya Tiba na Lugha ya Kiarabu.” [Manaaqib Ash-Shaafiy’ (2/116)]

 

Akasema tena: Ash-Shaafi’iy alikuwa anasikitikia Tiba walioipoteza Waislamu akisema, “Wamepoteza theluthi ya elimu, na wakaitelekeza kwa Mayahudi na Manaswara.” [Rejea iliyotangulia (2/116)]

 

Hivyo basi Tiba kwa Waislamu ni dharura ya ki mwana Aadam na hitajio la msingi na sio anasa ya kimawazo au jambo la ziada.

 

Imaam Ash-Shaafi’iy (Rahimahu Allaah) amesema: “Sijui elimu yeyote iliyo bora baada ya elimu ya halaal na haraam kuliko ta’aluma ya Tiba, isipokuwa watu wa kitabu wametushinda katika hilo.” [As-Siyar’ (10/57)]

 

Mwisho: Uislamu unatofautiana na dini zingine; Uislamu ni kwa ajili ya Aakhirah na dunia. Hivyo basi Uislamu haukuishia kuwafundisha watu yatakayowafaa na kuwaokoa wao Aakhirah tu, bali umewafundisha yatakayowafaa katika maisha yao ya dunia, pia ili kusimamisha jamii iliyo kamili duniani. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akateremsha elimu zote katika nyanja mbali mbali; kuna mfumo wa utawala na siasa, kuna mfumo wa kijamii na mfumo wa kiuchumi na mfumo wa siha na kadhalika.

 

Na atakayezingatia mwongozo wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ataukuta ni mwongozo ulio bora kuliko yote na uliokamilika katika kuhifadhi siha. Kwani kulinda siha kunategemea katika kuzingatia vyema vinywaji, vyakula, mavazi, makazi, hewa, malazi, kuamka, harakati, na utulivu. Haya yakipatikana kwa namna iliyolingana sawa, inayoendana na mwili, basi hupelekea kuwa na afya ya kudumu na kuweza kuhifadhika.

 

Ilipokuwa daraja ya elimu ya Tiba ni kubwa katika Uislamu na ndio kauli sahihi ya kweli mno kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani msamiati ya Tiba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) iko juu kileleni kabisa, ina sifa za pekee kuliko Tiba ya ki mwana Aadam kwani inatokana na chanzo cha Wahyi.  

 

Kwa kuwa Tiba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haijatiliwa mkazo, nikaamua kuhudumia maandiko ya ‘Ulamaa wetu, waliotangulia katika somo hili. Na nikaanza kuangalia kwa makini katika elimu waliyoiacha, na kuikuta katika kitabu bora kabisa; ‘Atw-twib An-Nabawiy’ (Tiba ya Nabiy)  cha Imaam  Ar-Rabbaany Shaykh Al-Islaam wa pili Ibn Al-Qayyim Al-Jawziyah (Rahimahu Allaah) ameng’ara katika misamiati ya Tiba ya Nabiy na kuitetea, na kuwajibu walioikana na kuipinga au kuona haina umuhimu mkubwa, kwa namna isiyo na kifani katika historia ya mwana Aadam, nikaanza kuiboresha na kuirekebisha na kuzihusisha mada zake nyingi na elimu ya “Tiba ya Kisasa” kwani pamoja na fadhila za Imaam Ibn Al-Qayyim Al-Jawziyah kama niliyotangulia kubainisha na pamoja na jitihada zake zote, alikuwa hakuvuka maarifa ya Tiba ya zama zake, ambapo tutaanzia hapo na kuendelea, na tutafanya marejeo kwake, na kinachojulikana haswa ni kuwa: Elimu hizi za Tiba hazina uwezo wa kuhifadhika kwa Tiba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  wala ulinzi wake!

 

Hivyo basi hapana budi kusoma upya Milango ya Tiba za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam); usomaji unaotegemea taarifa za kitaalamu za kisasa ili kuweza kuelewa vema Tiba na maana yake mbali mbali, malengo, na kupangilia kwa utaratibu kutokea hatua ya awali hadi tamati yake. Lakini kwa kuchunga kiini na maneno aliyotumia Imaam Ar-Rabbaaniy pamoja na nususi za ki-Tiba za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ikawa kwa tawfiyq ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na fadhila zake. Ni chuo cha Tiba, na mambo ya kujivunia kisayansi ya Tiba na taaluma ya madawa ya Kinabii.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa Majina Yake Mazuri na Sifa Zake Zilotukuka anitakabalie kwa kuinusuru Dini Yake, na kwa kuhudumia Sunnah ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwanusuru ndugu zangu Waislamu, aniwekee akiba thawabu ya amali yote hii hadi siku ya kukutana Naye, siku mali haitafaa kitu wala watoto ila atakayemjia Allaah kwa moyo salama.

 

 

Mwandishi:

Saliym bin ‘Iyd El–Hilaaly Al-Athariy As-Salafy – Abuu Usaamah.

Asubuhi siku ya Jumamosi Tarehe 11 Rabiy’ul-Aakhir 1423 A.H.  ‘Ammaan, Al-Balqaa ‘Aaswimat Jundul-Jordan min Bilaad Ash-Shaam Al-Mahruwsah.

 

 

 

 

 

 

[1] Yaani: Wana Aadam wanafuatana baadhi yao kwa wao ardhini; kama ilivyo katika kauli ya Allaah (Ta’alaa):

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَكُمْ خَلَائِفَ الْأَرْضِ  

Naye (Allaah) Ndiye Aliyekufanyeni makhalifa wa duniani [Al-An’aam: 165]

 

Na kauli Yake:

ثُمَّ جَعَلْنَاكُمْ خَلَائِفَ فِي الْأَرْضِ مِن بَعْدِهِمْ لِنَنظُرَ كَيْفَ تَعْمَلُونَ﴿١٤﴾

Kisha Tukakufanyeni warithi katika ardhi baada yao, ili Tutazame vipi mtatenda. [Yuwnus: 14]

 

Na kauli Yake:

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ ۗ  

Au nani Anayemuitika mwenye dhiki mno anapomwomba, na Akamuondoshea ouvu na Akakufanyeni makhalifa wa ardhi?  [An-Naml: 62]

 

 

Wametofautiana katika ukweli wa msemo: “Mwana Aadam ni ni khalifa wa Allaah katika ardhi yake” kwa rai tatu: Wengine wamejuzisha, wamekataa na tafsili. Na kilicho sahihi kwangu: ni kile alichokichagua Imaam Ibn Qayyim Al-Jawziyyah (Rahimahu Allaah) katika ‘Miftah Daar As-Sa’aadah’ (1/472): “Nimesema: Kilichokusudiwa ni ziada kwa Allaah: Yeye ni khalifa Wake; na sahihi ni: Kauli ya waliokataa. Na kama imekusudiwa ni idhwaafah kuwa: Allaah kuwa Amemwakilisha (khalifa) kuliko wengine waliokuwa kabla yake; hili halikatazi ziada, na ukweli wake: Khalifa wa Allaah ambaye amemjaalia mwakilishi kwa wengine.”

 

[2] Alikuwa ni shangazi yake na shangazi anachukua nafasi ya mama, na anakuwa vile vile kuwa ni mama yake kwani mke wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa watu ni mama zao “Na wake zake ni mama zao” [Al-Ahzaab: 6]

 

[3] Kulidekeza jina au utukuzo wa jina Urwah.0 Comments