January 24, 2021

Baraza la Kiislamu Marekani lampongeza Biden kwa kuondoa marufuku ya wasafiri Waislamu

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) imepongeza hatua ya rais mpya wa nchi hiyo, Joe Biden, kuondoa marufuku ya kusafiri na kuhajiri kuelekea Marekani raia wa nchi za Kiislamu.


Mara baada ya kuapishwa kuwa rais wa 46 wa Marekani, Joe Biden amesaini amri 17 za utekelezaji ambazo zimetengeua maamuzi yaliyopitishwa na mtangulizi wake Donald Trump.


Katika siku ya mwanzo baada ya kuingia Ikulu ya White House rais mpya wa Marekani amesaini amri 17 za utekelezaji kwa lengo la kubatilisha hatua kadhaa zilizochukuliwa na Trump.


Kuondoa marufuku ya kusafiri na kuhajiri kuelekea Marekani raia wa nchi za Kiislamu, kuirejesha Marekani kwenye Makubaliano ya Paris ya tabianchi, kusimamisha mchakato wa kujitoa nchi hiyo katika Shirika la Afya Duniani WHO, kulazimisha watu wote kuvaa barakoa katika maeneo ya umma na kuhitimisha hali ya hatari katika mpaka wa pamoja wa Marekani na Mexico ni miongoni mwa amri za utekelezaji zilizosainiwa na Biden mapema jana.


Kati ya nchi ambazo raia wao watafaidika na hatua hiyo mpya ya Biden ni Iran na Tanzania.


Katika taarifa, Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limekaribisha hatua ya Biden kuondoa marufuku ya kuingia nchini humo raia wa baadhi ya nchi za Kiislamu na Kiafrika na kusema hiyo ni hatua ya kwanza ya kutupilia mbali sera dhidi ya Waislamu na wahajiri zilizokuwa zikitekelezwa na utawala wa Trump.


CAIR pia imemtaka Biden awateue Waislamu katika nyadhifa mbali mbali serikalini.


Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only