Kukata Kucha Ni Lazima Siku Ya Ijumaa Au Inafaa Kukata Siku Nyenginezo?

 SWALI:

 

Why did Mtume Muhamad Salla Allaahu alayhi wa sallam used to cut his nails on Friday. What was the reason for cutting his nails on Fridays. Please advise

 

 

JIBU

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kujisafisha siku ya Ijumaa kwa kukoga (Ghuslu), kukata kucha, kuvaa nguo iliyo nzuri kabisa na kujitia manukato (kwa wanaume) ni katika kuiadhimisha siku hii tukufu ya Ijumaa kwani kufanya hivyo ni kufuata amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  katika Qur-aan Anavyosema:

 

 ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ حُرُمَاتِ اللَّـهِ فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ عِندَ رَبِّهِ  

Ndio hivyo iwe na yeyote anayeadhimisha vitukufu vya Allaah basi hivyo ni khayr kwake mbele ya Rabb wake. [Al-Hajj: 30]

 

 Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾

Ndivyo hivyo, na yeyote anayeadhimisha Ishara za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo. [Al-Hajj: 32]

 


Ama Swali kuhusu sababu hasa inayohusu kukata kucha, ni kwamba ni mojawapo ya Sunnah ya Fitwrah (Maumbile ya asili 'Pure Nature of Creation') kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) 

 

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚ

Basi elekeza uso wako kwenye Dini yenye kujiengua na upotofu inayoelemea haki. Umbile la asili la kumpwekesha Allaah Aliyowaumbia watu. [Ar-Ruwm: 30]

  

 

Na Sunnah kuhusu Fitwtrah hii  imesisitizwa katika Hadiyth mbali mbali.  Sunnah ambayo inapotimizwa huleta maslaha pande mbili ambazo ni:

 

 

i-Siha ya mwana-Aadam

 

ii-Kutimiza amri za Dini

 

Kutokana na pande zote mbili hizo, faida zinazopatikana ni:

  • Kuepukana na maradhi.
  • Kudhihirisha uzuri na usafi.
  • Kuitukuza na kuiridhisha nafsi (kuwa imetimiza Sunnah).
  • Kutimiza Twahara ya wudhuu vizuri.
  • Kuukirimu ubinaadamu. 

 

Hadiyth ifuatayo inatufundisha vitu vya kufanya katika mwili wetu kupatikana Fitwrah:

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه، عن النبي  قال: (( الفطرة خمسة، أو خمس من الفطرة. الختان، والاستحداد، وتقليم الأظفار، ونتف الإبط، وقص الشارب))  متفق عليه

 Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Fitwrah ni tano, au (vitu) vitano miongoni ni mwa Fitwrah, Kutahiri (Circumcision), kunyoa (au kupunguza) nywele za sehemu ya siri (pubic hair), kukata kucha, kunyofoa (au kunyoa) nywele za kwapani, na kupunguza mashurubu))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

   

Na kufanya hayo tumewekewa muda wa siku Arubaini tusipitize bila kukamilisha Fitwrah hiyo.

 

عن أنس بن مالك رضي الله عنه، قال. "وقت لنا  وفي رواية، قال: وقت لنا رسول الله   في قص الشارب وتقليم الأظافر ونتف الإبط وحلق العانة. أن لا نترك أكثر من أربعين ليلة. أخرجه أبو داود والترمذي ومسلم والنسائي.

Imetoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituwekea muda wa kupunguza masharubu, kukata kucha, kunyofoa (au kunyoa) nywele za kwapa, na kunyoa (au kupunguza) nywele za sehemu za siri (pubic hair), kwamba tusiziache zaidi ya siku Arubaini)) [Muslim, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy]

 

 

Kuhusu kukata kucha Ijumaa kumependezewa kwa sababu Muislam anatakiwa siku ya Ijumaa ajisafishe na kujipamba wakati anakwenda Msikitini, na hivyo basi kukata kucha ni jambo moja katika usafi huo.

 

 

Vile vile kukata kucha siku ya Ijumaa pamoja na kupunguza masharubu na kunyoa au kupunguza nywele za sehemu za siri (pubic hair), kunyofoa au kunyoa nywele za kwapa, na pia kujipaka manukato kwa mwanaume, kupaka mafuta nywele na ndevu zake na kuzichana, ni jambo lenye kupendeza kwa Muislam.

 

Vile vile, kucha zinapokuwa ndefu, wudhuu wa Swalaah huwa ni vigumu kutekelezeka kikamilifu kwa uwezekano wa maji kutofika sehemu za ndani ya kucha. Vilevile kama mtu hajakuwa makini kwa usafi, kucha ndefu huhifadhi uchafu mara kwa mara.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments