January 11, 2021

Sri Lanka yatakiwa kuacha kuchoma maiti za Waislamu

 Jumuiya 16 zisizo za kiserikali nchini Australia zimetoa wito wa kushinikizwa serikali ya Sri Lanka ili isitishe kuchoma moto maiti za Waislamu wanaoaga dunia kutokana na virusi vya corona nchini Sri Lanka.


Wito huo umetolewa katika barua iliyotumwa na mkuu wa muungano wa AAGGSL, Dr Lionel Bopage, kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Muungano huo unawakilisha mashirika na jumuiya za Waislamu, Wakristo, Wahindu, Mabudha na kadhalika.Sehemu moja ya barua hiyo imesema kuchoma moto kwa lazima maiti za watu wanaoaga dunia kutokana na virusi vya corona ni ukiukaji wa haki za binadamu na kwamba nchi zenye idadi kubwa ya wahanga wa corona kama Marekani, India, Mexico na italia hazichomi moto maiti za wahanga wa corona kama inavyofanyika nchini Sri Lanka.


Barua hiyo imesema mwenendo huo unaokiuka maadili na unaokera wa serikali ya Sri Lanka unasababisha wasiwasi na machafuko nchini.


Dr Lionel Bopage amesema katika barua hiyo iliyotumwa kwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba serikali ya Sri Lanka inakiuka haki za Waislamu na Wakristo kwa kuchoma moto maiti za watu wanaofariki dunia kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19.


Wakati huo huo Mwenyekiti wa Baraza la Kiislamu katika jimbo la Victoria nchini Australia amesema madai yanayotolewa na serikali ya Sri Lanka kuhalalisha kitendo hicho akisema kuwa kuzika maiti za wahanga wa corona kunasababisha maradhi na kuchafua maji, hayana msingi wowote.


Mohammad Muhyiddeen amesema uamuzi wa kuchoma moto maiti za Waislamu nchini Sri Lanka unatokana na sababu za kibaguzi. Ameongeza kuwa Waislamu wanaounda asilimia 10 ya jamii ya watu wa Sri Lanka wamekuwa wakisumbuliwa na ukatili katika miaka iliyopita hususan kutokwa kwa baadhi ya wanasiasa na makuhani wa Kibudha.


Alkhamisi iliyopita serikali ya Sri Lanka ilisisitiza kuwa itaendelea kuchoma moto maiti zote za watu wanaofariki dunia kutokana na virusi vya corona licha ya kuendelea malalamiko ya Waislamu kote duniani wanaotaka kukomeshwa zoezi hilo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only