Uswisi yaitisha kura ya waoni kuhusu nikabu ya wanawake Waislamu

Uswisi imeitisha kura ya maoni kuhusu marufuku ya vazi la nikabu (niqabu) au burqa linalotumiwa na wanawake Waislamu kufunika uso kikamilifu.


Kura hiyo ya maoni imepangwa kufanyika Machi 7 mwaka huu. Kwa mujibu wa katiba ya Uswisi mabadiliko yoyote ya sheria ya kikatiba huelekea katika kura ya maoni iwapo watu zaidi ya 100,000 watatia saini pendekezo la kutaka kura hiyo ya maoni.


Mwaka 2009 wapiga kura Uswisi walishiriki katika kura ya maoni na kuunga mkono pendekezo la kupinga ujenzi wa minara mipya katika misikiti nchini humo.


Tayari majimbo ya St. Gallen na Ticino nchini Uswisi yameshapiga marufuku nikabu baada ya wapiga kura wa maeneo hayo kuidhinisha uamuzi huo. Hatahivyo serikali ya Uswisi imetangaza kupinga pendekezo la kura ya maoni ya kupiga marufuku vazi la nikabu nchini humo na kusema hatua kama hiyo itaathiri vibaya utalii nchini humo. Katika taarifa serikali ya Uswisi inasema ni watu wachahce sana wanaovaa nikabu nchini humo na hivyo marufuku ya nikabu itavuruga utalii na itakiuka haki za baadhi ya wanawake. Taarifa hiyo imeongeza kuwa aghalabu ya wanawake wanaovaa nikabu ni watalii ambao hutembelea nchi hiyo kwa muda mfupi.


Maeneo ya Montreux, Ziwa Geneva na Interlaken huwavutia watalii Waislamu ambao aghalabu ni kutoka nchi tajiri za Ghuba ya Uajemi na hivyo serikali ya Uswisi haitaki kupoteza pato kubwa litokanalo na watalii hao.


Wakuu wa Uswisi wanasema badala ya kupiga marufuku nikabu, kunapaswa kuwa na sheria ya kuwashurutisha wanawake wanaovaa vazi hilo kuonyesha uso wanapotakiwa na maafisa wa usalama au wanapotumia usafiri wa umma.


Waislamu ni asilimia 5 ya watu wote milioni 8.6 nchini Uswisi.

0 Comments