Qur-aaniyyuwn: Wanaopinga Hadiyth Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 


Alhamdulillaah wasw-Swalaatu was-Salaam 'alaa Rasuwlihil Kariym wa 'alaa aaalihi wa-Aswhaabihi Ajma'iyn. Wa ba'ad,

 

 

 

Yapo makundi mengi yanayojinasibisha na Uislam na kila siku yanaongezeka, lakini utakapoingia ndani yao na kuyajua au utakapoyasoma vizuri, itakubainikia ukweli halisi wa mambo, na hapo ndipo yale maneno ya Mtukufu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapo juu yatakapoonekana maana na ukweli wake halisi.

 

 

Katika miaka ya nyuma kumejitokeza  kundi linalojiita Waislam na kujipa jina la 'Al-Qur-aaniyyuwn' au 'Ahlul-Qur-aan' au 'The Submitters' au 'Khalifites (19ers)' n.k. Wote hao mwelekeo wao ni mmoja, nao ni kufuata Qur-aan tu pekee na kutohitaji Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wanapinga Hadiyth za Rasuli wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakidai zimejaa uongo na uzushi na hivyo hazifai kufuatwa! Na kwamba zimeandikwa na watu na kuwa watu hao (kina Imam Al-Bukhaariy) walikuja miaka mingi baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki. Na kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataa Hadiyth zisiandikwe!

 

 

Mmoja wa waanzilishi wake wa miaka ya karibuni ni mtu aliyekuwa akiitwa Rashad Khalifa, huyu alikuwa ni Mmisri aliyezaliwa mwaka 1935 na akafa kwa kuuliwa mwaka 1990 huko Tucson, Arizona. Alihamia Marekani kama mwanafunzi wa biochemistry na kupata uraia huko. Alianzisha kundi aliloliita 'United Submitters International' na ambalo katika imani yake ni kukataa na kupinga Hadiyth na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ni moja ya vyanzo au kanuni ya shari'ah ya Dini. Kwa miaka mingi alikuwa ni Imam wa msikiti huko Tucson, Arizona.

 

 

Kuanzia mwaka 1969, Rashad Khalifa alianza kutumia Computer kufanya uchangunuzi wa idadi ya marudio wa herufi na maneno ya Qur-aan. Alichapisha takwimu zake za mwanzo miaka michache baadaye kuhusu utafiti wake huo. Hata hivyo, mnamo mwaka 1974 alidai kuwa kagundua mpangilio au muundo wa kutatanisha kuhusiana na tarakimu katika maandishi ya Qur-aan yenye kuhusiana na namba 19 ambayo imetajwa katika suwrah ya Al-Muddathir kuanzia aya ya 30. Muundo huo unahusiana na ulinganishi wa tarakimu na herufi. Alichapisha vitabu mbalimbali kuhusiana na somo hilo.

 

 

Rashad Khalifa, alikubalika na baadhi ya watu waliodanganyika na fikra zake hizo, lakini alijenga chuki kubwa kwa Waislam kwa uasi wake na tabia ya ushindani na kuonekana ni mtu anayepotosha katika Uislam kwa fikra zake hizo potofu.

 

 

Rashad Khalifa vilevile alitangaza hadharani kuzipinga aya za 128 na 129 za surah ya At Tawbah na kudai zimepachikwa katika Qur-aan!!

 

 

Rashad Khalifa mwisho wake alidai pia Utume, akisema yeye ni Nabiy aliyeahidiwa na Allaah! Alitumia muundo wake huo wa kuchanganisha namba na maneno ya Qur-aan na kuoanisha jina lake pamoja na Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Pia kuna kadhia maarufu liyochapishwa na magazeti mbalimbali ya yeye Khalifa kuhusishwa na kesi ya kubaka.

 

Wanachuoni wengi wameandika vitabu mbalimbali kuhusu Upotofu na Ubatili wa kundi hilo na Ukafiri wao wa wazi wa kupinga Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kwanza tuangalie hoja ya kukusanywa Qur-aan na Hadiyth kuonyesha ubovu wa madai yao.

 

 

1-Kwanza kabisa inawatosha pekee hoja ya kuwa ikiwa wao wanakanusha Hadiyth kwa kuwa zimekusanywa na 'Ulamaa wa Hadiyth kama Imaam Al-Bukhaariy na Imaam Muslim na kadhalika, baada ya kufa kwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) , inaonyesha dhahiri kuwa hawajui kwamba na  Qur-aan hii tunayoisoma, imekusanywa baada ya kifo cha Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  na kuwekwa katika kitabu nacho ni Mus-haf wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Na kabla ya hapo Qur-aan ilikuwa katika vifua vya waliohifadhi, na kuandikwa katika ngozi au karatasi au mabango ya mti.  

 

 

Ikiwa shaka yao ni katika ukusanyaji wa Hadiyth, ingeliwapasa kwanza wasome wasifu (biographies) za hawa 'Ulamaa wa Hadiyth na njia zao walizokuwa wakizitumia katika kukusanya Hadiyth, ili waone umakini waliokuwa wakiutumia, hasa Al-Bukhaariy na Muslim ambao Hadiyth zao zinatutosheleza kupata mafundisho ya Dini yetu.

 

 

Ukusanyaji wa Qur-aan ulifanyika kwa sababu ya khofu iliyowapata Swahaba    baada ya kuuliwa Swahaba wengi waliohifadhi Qur-aan katika vita vya Yamaamah, kuwa kama haitowekwa katika kitabu itawafikiaje vizazi vijavyo? Karne baada ya karne? Hali kadhalika ukusanyaji wa Hadiyth ulikuwa na lengo hilo hilo.   

 

 

Katika umakini wao Swahaba wa kukusanya Qur-aan wakaweka sharti ya kupatikana mashahidi wawili waliohifadhi Qur-aan kuthibitisha kuwa Aayah ni sahihi na sio ya kuzushwa:

 

 

Ikawa zinakusanywa Aayah baada ya kupatikana katika vifua vya Sahaba wawili. Ikaendelea mpaka mwisho zikamalizika ikabakia ayah moja ambayo ni ya mwisho katika Suwrah At-Tawbah ikawa haikupatikana kwa mtu isipokuwa kwa Abu-Huzaymah Al-Answaariy. Lakini kwa vile sahaba huyu alijulikana kuwa ushahidi wake mmoja ni sawa na mashahidi wawili kutokana na kauli  ya  Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumshuhudia katika kisa cha biashara na Yahudi. Na hii ni moja katika miujiza ya Qur-aan ya   maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika kuhifadhi maneno Yake.

 

 

Na hoja yao ya kuwa Hadiyth ziliandikwa na watu muda mrefu baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki, na kuwa pia aliwahi kukataa Hadiyth zisiandikwe, ni hoja zenye ufinyu wa ufahamu wa kihistoria na ni hoja zinazotumika na Mustashriqiyn (Orientalists) katika kuuhujumu na kuutia kasoro Uislam. Na hoja hizo zapingwa na Hadiyth mbalimbali zenye kuthibitisha kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) karuhusu Swahaba kuandika kutoka kwake, mifano michache ni hii:

 

 

 • Kwamba Sahaba Ibn ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiandika kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 • ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na nyaraka zilizoandikwa Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 • Adhw-Dhwahaak bin Sufyaan aliwahi kumsaidia Khalifa 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  katika fatwa kuhusu malipo ya pesa kwa wajane kutoka katika waraka aliokuwa nao ambao ulitumwa kwa kabila lake na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe wakati wa uhai wake.

 

 • Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, "Balighisheni kutoka kwangu japo aya moja" n.k.

 

 • Alitoa ruhusa kwa mtu mmoja kutoka Yemen aitwaye Abu Shah aandikiwe Hadiyth zake azipeleke Yemen.

 

 

Hapa chini tutaangalia shahidi mbalimbali kutoka katika Qur-aan kuthibitisha kwa nini tunapaswa kufuata Sunnah za Nabiy wetu Mpenzi (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuonyesha kuwa Sunnah ndio msingi mkuu wa shari'ah ya Dini yetu pamoja na Qur-aan, na bila Sunnah, Qur-aan hii tuliyonayo isingeweza kueleweka na tusingejua maamrisho mengi na mafunzo mbalimbali yaliyomo ndani yake bila kufahamishwa na Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndio maana Allaah Akumtuma Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwetu na kumshushia hiyo Qur-aan ili atufundishe na kutufafanulia. Pia tutaona hukumu ya kukataa na kupinga Sunnah, na hizi ni dalili na uthibitisho wenye kukata kudhihirisha kuwa wanaodai kuwa wao ni 'Watu wa Qur-aan' kuwa hawahusiani hata chembe na Qur-aan. Kwani Qur-aan yenyewe inawasuta na kuwapinga.

 

Anatuambia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾

Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi. [Al-Hijr:9]

 

 

 

2-Bila ya shaka Qur-aaniyyuwn hawafuati hata hiyo Qur-aan wanayodai kuwa pekee wanaifuata kwani humo amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni nyingi za kumtii na kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا آمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي أَنزَلَ مِن قَبْلُ ۚ وَمَن يَكْفُرْ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿١٣٦﴾

Enyi walioamini! Mwaminini Allaah na Rasuli Wake na Kitabu Alichokiteremsha kwa Rasuli Wake na Kitabu Alichokiteremsha kabla. Na atakayemkufuru Allaah na Malaika Wake, na Vitabu Vyake na Rusuli Wake na Siku ya Mwisho, basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali[An-Nisaa:136]

 

 

Pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesema:

 

فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَالنُّورِ الَّذِي أَنزَلْنَا ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ﴿٨﴾

Basi muaminini Allaah na Rasuli Wake na Nuru (Qur-aan) Tuliyoiteremsha, na Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [At-Taghaabun: 8]

 

Vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesema:

 

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٥٤﴾

Sema: Mtiini Allaah na mtiini Rasuli. Mkigeukilia mbali, basi hakika jukumu lake ni lile alilobebeshwa tu nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa. Na mkimtii mtaongoka; na hapana juu ya Rasuli isipokuwa ubalighisho bayana. [An-Nuwr:54]

 

Na Amesma Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا  

Na lolote analokupeni Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم ) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. [Al-Hashr:7]

 

 

 

3-Kukanusha Hadiyth ni kukanusha Siyrah vile vile kwani bila ya Hadiyth tusingeliweza kupata mafundisho ya Siyrah kamili ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

4-Tungelipataje mafundisho ya tabia ya aina mbali mbali bila ya kuwa na mifano kutoka wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?   

 

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا ﴿٢١﴾

Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi. [Al-Ahzaab:21]

 

Kwani vile vile ukamilifu wote wa tabia umetokana naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyosema katika Hadiyth kuwa

 

قال صلى الله عليه وسلم : (إنما بعثت لأتمم مكارم الأخلاق)

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema, "Nimetumwa kukamilisha tabia njema." Imepokewa na [Imam Ahmad].

 

 

5-Qur-aan haikuelezea namna ya kutekeleza ibada mbalimbali, kama vile Swalaah, ingawa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Katuambia tusimamishe Swalaah lakini, Hakutuelezea vipi kuswali Swalaah yenyewe, yaani kama mwanzo tusimame, kisha turukuu, tusujudu n.k.   Wala pia Hakutuelezea idadi za Rakaa kuwa Alfajiri ni mbili, adhuhuri ni nne, alasiri ni nne, magharibi ni tatu na ‘Ishaa ni nne.  Sasa tungelijuwaje bila ya kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?   Naye ametuambia katika Hadiyth yake kuwa

 

"صلوا كما رأيتموني أصلي"  رواه البخاري

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema, "Swalini kama mlivyoniona nikiswali" Imepokewa na [Imaam Al-Bukhaariy.]

 

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) alikwishamueleza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni kazi yake kuifafanua Qur-aan. Yaani kuwa Aayah zake nyingine azifafanue kwa kutuelezea zaidi na kutuonyesha au kutufahamisha zaidi. 

 

 

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ﴿٤٤﴾

44. (Tumewatuma) Kwa hoja bayana na vitabu. Na Tumekuteremshia Ukumbusho (Qur-aan) ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao huenda wakapata kutafakari. [An-Nahl:44]

 

 

Adh-Dhikr ina maana ya ‘Wahy’ na hali pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kasema kuwa japo kuwa yeye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema lakini hakika ni ‘wahyi’ kutoka Kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَى﴿٣﴾

Na wala hatamki kwa hawaa. [An-Najm:3]

 

 

Vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema katika Surat Al-'Imraan:

 

لَقَدْ مَنَّ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ إِذْ بَعَثَ فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْ أَنفُسِهِمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١٦٤﴾

Kwa yakini Allaah Amewafanyia fadhila Waumini pale Alipomtuma kwao, Rasuli miongoni mwao, anawasomea Aayaat Zake na anawatakasa na anawafunza Kitabu na Hikmah (Sunnah); japokuwa walikuwa kabla katika upotofu bayana. [Al-'Imraan:164]

 

Nguzo za Kiislamu ambazo ni muhimu kabisa zimekuja katika Hadiyth ambazo yeye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe imebidi pia atuelelezee zaidi kutimiza hizo nguzo.

 

 

Zifuatazo ni baadhi ya ibada zilokuwa ni fardhi au Sunnah ambazo hazikuelezwa kwa urefu katika Qur-aan bali tumezipata katika Sunnah.

 

Na ibaadah hizi zimekusanyika katika elimu ya FIQH, sasa sijui vipi Qur-aaniyyuwn wanatimiza ibaadah hizo bila ya elimu ya FIQH na sijui elimu yao ya ibada wanaipata kutoka wapi?

 

 

 • Swalaah kama tulivyoelezea hapo juu, ni Swalaah zote, yaani Swalaah ya Ijumaa, Swalaah za Sunnah zote, Du’aa au Adhkaar katika Swalaah, Swalaah ya maiti, Swalaah ya ‘Iyd.

 

 • Swawm za fardhi na za Sunnah, pamoja na fadhila zake.

 

 • Aina zote za kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) yaani Adhkaar za Mchana na usiku ambazo tunazihitaji kila dakika katika maisha yetu.

 

 • Ibada ya Hajj bila ya kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenda Hajj na Swahaba Na kuwapa mafundisho wangelijuaje Swahaba jinsi ya kufanya Manaasik hayo ya Hajj?  Na sisi tungelijuaje bila ya mafundisho kutokana na Hadiyth?

 

 • Baadhi ya mambo yaliyokuwa hayakutajwa katika Qur-aan na tumeyapata kutokana mafundisho ya Sunnah:

 

 • Allaah katukataza kula nyama ya nguruwe, na ingawa kataja kuwa mbwa wana manufaa kwetu kuwa wanawinda lakini hakutuambia kuwa hatufai kula nyama yake.   Sasa bila ya Hadiyth au ‘Qiyaas’ au analojia (analogy) waliyotumia wataalamu kuwa mbwa ni najis tungelijuaje?  Au hawa wenzetu wanakula nyama ya mbwa? 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anesema:

 

يَسْأَلُونَكَ مَاذَا أُحِلَّ لَهُمْ ۖ قُلْ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ ۙ وَمَا عَلَّمْتُم مِّنَ الْجَوَارِحِ مُكَلِّبِينَ تُعَلِّمُونَهُنَّ مِمَّا عَلَّمَكُمُ اللَّـهُ ۖ فَكُلُوا مِمَّا أَمْسَكْنَ عَلَيْكُمْ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ﴿٤﴾

Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa vizuri na mlichowafunza wanyama au ndege wa kuwinda; mkiwafuga kuwafunza uwindaji, mnawafunza katika ambayo Amekufunzeni Allaah. Basi kuleni walichokukamatieni, na mkitajie Jina la Allaah. Na mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mwepesi wa kuhesabu. [Al-Maaidah:4]

 

 

 • Alama za Qiyaamah.

 

 • Sababu za kuteremshwa baadhi ya Aayah.

 

 • Adhabu alizoonyeshwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari ya Israa Wal-Mi'iraaj.

 

 • Hadiyth za watu wa kale na visa ambavo tunapata mafundisho mengi.

 

 • Habari za moto na pepo na kuwa na tamaa na khofu. 

 

 • Bila ya shaka, bila ya Hadiyth kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tusingeliweza kujua yote hayo.

 

 

       

6. Muumini hasa ni yule ambaye anampenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zaidi kuliko nafsi yake.

 

النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ

Nabiy ana haki zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. [Al-Ahzaab:6]

 

Na mapenzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanapasa yaendelee hata baada ya kufa kwake. Na moja ya dalili ya mapenzi hayo ni kufuata Sunnah zake. Naye katuhadharisha kuwa tusije tukatofautiana baada ya kufa kwake au kugawanyika makundi mbali mbali na akatupa ufumbuzi wa kuepukana na hatari hiyo, kuwa katuachia Qur-aan na Sunnah zake, pindi tukizishikilia hatutafarikiana wala kupotea kabisa kwa kutuambia:

 

    تركت فيكم ما إن تمسكتم به لن تضلوا بعدي أبدا.. كتاب الله وسنتي

"Nimewaachieni ambayo mkishikimana navyo hamtopotea baada yangu abadan; Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu"

 

Makundi kama haya ya Qur-aaniyyuwn ndio yaliyopotea kabisa kwa kukanusha Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

       

 

 

7. Kuhusu hoja zao kuwa kupigwa mtu mawe mpaka kufa haimo katika Qur-aan, kwetu sisi tunaofuata Hadiyth hatuna shaka kabisa kwani jambo hili 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa ameshalitahadharisha na Hadiyth imo katika Al-Bukhaariy:

 

`Umar katika zama zake za Ukhalifa alikumbusha, "Allaah Amemshushia Muhammad Kitabu. Katika kile Alichomshushia, ni Aayah kuhusu kupiga mawe, tuliisoma, na tukafundishwa, na tukaizingatia. Nabiy alipiga mawe (waliostahili adhabu hiyo) na sisi tukawa tunapiga baada yake. Nina khofu huko mbeleni, watu watakuja kusema kwamba hawajakuta pahala katika Kitabu cha Allaah pametajwa kuhusu adhabu ya kupigwa mawe na hivyo wataachana nayo na kupuuza maagizo Aliyoshusha Allaah. Hakika kupiga mawe katika Kitabu cha Allaah ni adhabu inayowawajibikia wale wazinifu ambao ni wanaume waliooa na wanawake walioolewa. [Al-Bukhaariy]

 

Na pia wakisoma ayah Hii ifuatayo watapata majibu ya hayo na zaidi:

 

 وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا﴿٣٦﴾

Na haiwi kwa Muumini mwanamume na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab:36]

    

 

 

Kama wanafuata kweli Qur-aan basi wangelikhofu kufikwa na majuto na adhabu kama zilivyo katika ayah kama hizi zifuatazo zinazotuhadharisha kumkanusha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَىٰ يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلًا ﴿٢٧﴾   يَا وَيْلَتَى لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلَانًا خَلِيلًا ﴿٢٨﴾ لَّقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي ۗ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلْإِنسَانِ خَذُولًا ﴿٢٩﴾

Na siku dhalimu atakapotafuna mikono yake akisema: Laiti ningeshika njia pamoja na Rasuli.  Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki mwandani.  Kwa yakini amenipoteza mbali na Ukumbusho baada ya kunijia. Na shaytwaan kwa insani daima ni mwenye kutelekeza. [Al-Furqaan: 27 - 29].

 

 

Lakini bila ya shaka wao ni vipofu wa moyo na sio wa macho! 

 

أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَتَكُونَ لَهُمْ قُلُوبٌ يَعْقِلُونَ بِهَا أَوْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا ۖ فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾

Je, basi hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo za kutia akilini au masikio ya kusikilizia; kwani hakika hayapofuki macho, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani. [Al-Hajj:46]

 

 

Na tunaona pia jinsi gani Allaah Anavyotuonya vikali sana kumpinga na kwenda kinyume na mafunzo ya Rasuli wetu:

 

 فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾

Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo. [An-Nuwr: 63]

 

 

Baada ya haya machache, ndugu zangu, imetubainikia kuwa wanaodai kuwa ni watu wa Qur-aan na hawana uhusiano wowote na Hadiyth na Sunnah za Rasuli wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni watu waliofuata njia ya shaytwaan na mwisho wao ni ule mwisho wa shaytwaan.

 

 

Tunamuomba Allaah daima Aithibitishe Mioyo yetu katika Iymaan na Atupe mwisho mwema. Atuepushe na Upindukwaji Moyo kama wa hao waliokhitari hawaa zao kuliko aliyokuja nayo Mtukufu Mpenzi Mbora wa Viumbe, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

0 Comments