Apple yafuta app ya Quran China

Hatua ya kampuni ya Apple ya Marekani ya kuondoa program ya Quran Majeed katika maduka yake nchini China imezua maswali mengi juu ya malengo na sababu kitendo hicho. 


Ni baada ya kampuni hiyo ya Apple kuondoa programu hiyo inayotumiwa sana kwa ajili ya masuala yanayiohusiana na Qur'ani na mafundishi ya Uislamu kuondolewa katika maduka ya App Store nchini Uchina, suala ambalo limewashangaza watumiaji wa programu hiyo na wafuatiali wa masuala ya kidini na teknolojia.


Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, kampuni ya Apple imedai kuwa imechukua hatua ya kuondoa programu ya Quran Majeed katika maduka yake nchini China ili kutiii amri ya serikali ya Beijing. Hata hivyo serikali ya China haijatoa maelezo yoyote kuhusiana na madai hayo.


Programu mashuhuri ya Quran Majeed hutumiwa sana kwa ajili ya qiraa ya Qur'ani na masuala mengine yanayohusiana na Swala kama kujua upande wa kibla, nyakati za Swala, dua, maeneo ya misikiti iliyo karibu na mtumiaji na kadhalika.


Katika miaka ya karibuni China imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji mkubwa kuhusiana na ukiukaji wa haki za Waislamu hususan jamii ya Uighur katika jimbo la Xinjiang.


Mwezi Juni mwaka huu Katibu Mkuu wa Amnesty International, Agnès Callamard amesema jamii ya Waislamu waliowachache ya Uighur inapitia mateso makali, jinai dhidi ya binadamu na ukiukaji mwingine wa kutisha wa haki za binadamu tokea mwaka 2017 na kwamba jinai hizo zinapaswa kuishtua jamii ya mwanadamu.  

0 Comments