Je' Chanjo (Vaccination) Ni Shirki?

 SWALI:

 

Assalam alaikum, Mungu atawabariki kwa kutufunua macho kwa mengi tunayojielimisha nayo. Twamuomba Allah awalipe mema hapa duniani na kesho akhera. Swali langu nauliza jee hizi chanjo (Vaccination) ni shirki au la? Kwani kuna wanaosema ni shirki ndogo kwa kuwa tumeamrishwa tujitibu tunapo kuwa wagonjwa. Shukran.

 


 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu chanjo na hukumu yake.

 

 

Kutia chanjo si shirki ndogo wala kubwa. Hiyo ni kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamuru tutafute dawa tunapokuwa wagonjwa. Na katika kauli yake nyingine akasema: Allaah Hakuteremsha ugonjwa isipokuwa ameleta na dawa yake basi jitibieni (al-Haakim).

 

Na kuhusu kuambukizwa hata kwa ngamia, alisema (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni nani aliyemuambukiza yule ngamia wa kwanza?” (Al-Bukhaariy na Muslim). Hiyo ni kumaanisha kuwa ngamia mgonjwa alikuwa atenganishwe na wale ngamia wengine walioathirika.

 

Na chanjo ni kumkinga mtoto au wewe mwenyewe na ugonjwa na hasa ikiwa unakwenda katika nchi ambayo ugonjwa kama ule unapatikana kwa kiasi kikubwa. Na hii ni katika kuwalinda wale wasiokuwa nao kuupata au aliye nao kuueneza kwa wasiokuwa nao. Na hilo pia limepatikana katika uongofu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kuelekea katika sehemu yenye tauni. Kwa ajili hiyo, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipozuru al-Quds alikuwa azuru Damascus lakini kwa sababu ya tauni iliyokuwa kule hakwenda. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Itapotokea tauni katika mji nanyi mpo humo basi msitoke na kama ukitokea ugonjwa huo nanyi hampo basi msiingie” (Ahmad).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

0 Comments