Masiyhud-Dajjaal Alikosa Nini? Zipi Alama Zake? Ni Kweli Zimo Katika Noti Ya Dola?

 SWALI:

 

Asalam aleikum, inshaallah nyote wazima, ndugu zangu ningependa kuuliza maswali kuhusu massih dajal; je alikosa nini kwa mwenyezi mungu mpaka ALLAH SWT akampa adhabu hiyo? ni kweli kuwa amefungwa kwenye island ambayo watu wengi wasema kuwa ni bermuda triangle ambayo haipiti kitu chochote karibu yake bila kuungamia? Maana ukifuata historia za Bermuda triangle mambo yote yanaotokea niyakimuijiza hayaeleweki. Je kuhusu hela za marekani ukiangalia kwenye noti ya dola moja nyuma yake kuna triangle na ina jicho moja katikati yake watu wengi wasema kuwa ni jicho lake masih dajal na kuwa hizo ni signs kutoka kwa mwenyezi mungu na kuwa yuko kweli huko Bermuda triangle maana pia ardhi hiyo iko shape ya triangle ni kweli hayo yote? Ndugu zangu niuweni radhi ikiwa nimekosea naomba majibu yenu na pia nielimisheni zaidi kuhusu swala hili wasalam aleikum shukran.

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Masiyhud Dajjaal.

Allaah Aliyetukuka ni Mwelewa wa kila kitu hapa duniani na mbinguni – Hufanya Atakalo wala hakuna wa kumuuliza bali sisi ndio wakuulizwa na Yeye. Anayofanya Allaah Aliyetukuka si majaribio bali ni hakika. Allaah Aliyetukuka Mwenyewe huleta mitihani kwa waja wake kwa njia na aina mbali mbali. Mtihani mmoja ambao wanaadamu watapata ni kuletwa kwa Masiyhud Dajjaal na pia Juuj na Maajuuj.

 

Kuletewa kitu kuwa ni mtihani ili tujulikanwe msimamo wetu sio kuwa kitu kile kimekosea. Saa nyingine yapo mambo ambayo hatuna majibu nayo. Mfano kwa nini punda wa mjini akawa haramu na punda milia akawa halali kwa Muislamu kula. Haya ni mtihani kwetu nasi kama Waumini tunatakiwa tuamini kwani yatoka kwa Allaah Aliyetukuka wala tusiwe kama Mayahudi. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na (Waumini) husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghfira Mola Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako” (al-Baqarah [2]: 285).

Ilhali Mayahudi, msimamo wao ni:

Na tulipochukua ahadi yenu na tukauinua mlima juu yenu (tukakwambieni): Kamateni kwa nguvu haya tuliyo kupeni na sikieni. Wakasema: Tumesikia na tumekataa!” (al-Baqarah [2]: 93).

 

Na Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

Yeye ndiye Aliyekuteremshia Kitabu hichi (Qur-aan). Ndani yake zimo Aayah Muhkam (nyepesi kufahamika, zenye maana wazi). Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine Mutashaabihaat (zinababaisha; zisizo wazi kufahamika kirahisi). Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Allaah. Na wale wenye msingi madhubuti katika elimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipokuwa wenye akili” (Aal-‘Imraan [3]: 7).

Kwa hivyo, mas-ala mengi ya ndani hatujui isipokuwa ni mtihani kwetu, na sisi kama Waumini tunatakiwa tuamini kuwa kama Alivyotueleza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa huyo Masiyhud Dajjaal yupo amefungwa na atafunguliwa mwisho wa dunia.

 

Ama yupo katika Bahari gani hilo linajulikana na Allaah Aliyetukuka peke yake sio sisi wanaadamu. Na haiwezekani kuwa Bermuda kwa kuwa iko mbali na Peninsula ya Arabuni na Abu Ruqayyah Tamiym ad-Daariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipokuja kumueleza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuona kwake Dajjaal akiwa amefungwa na silsila katika kisiwa cha bahari.

 

Ama yanayosemwa na yatakayoendelea kusemwa kutoka kwa watu kuwa Dajjaal ni Marekani na dalili ya noti na Dola moja, si ya sawa kwani katika maelezo ya Dajjaal si nchi bali ni kiumbe. Inawezakana labda kuwa Marekani kuwa mshirika wa kiumbe huyo lakini katika hilo pia hakuna ushahidi bali ushahidi uliopo ni kuwa wafuasi wake wengi watakuwa ni Mayahudi kama alivyoashiria Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na tunachojua kutoka kwa dalili za wazi ni kuwa Dajjaal huyo atauliwa Palestina katika mlango wa kuingilia mji unaoitwa al-Lud na Nabii ‘Iysa (‘Alayhis salaam).

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi

 

Hadiyth Ya Al-Jassaasah

 

Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments