Maswali magumu kuhusu Taliban wakirejea madarakani

Kundi la Taliban tayari limeshaikamata tena nchi ya Afghanistan ikiwa ni miaka takribani 20 tangu liondolewe katika usukani wa nchi hiyo.Utawala wa Taliban ambao ulianzia mwaka 1996 uliondolewa na Marekani pamoja na washirika wake mwaka 2001 baada ya kuivamia nchi hiyo kijeshi katika harakati za kumsaka aliyekuwa kiongozi wa Al-Qaeda, Osama Bin Laden.


Ikumbukwe yalikuwa ni madola makubwa ya nchi za Magharibi chini ya Umoja wa wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO) yakiongozwa na Marekani, ndio yaliyoivamia Afghanistan kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 katika ardhi ya Marekani.


Kwa sasa kundi hilo baada ya kukaa nje ya utawala kwa miaka hiyo 20 limerejea madarakani.


Muda mfupi tu baada ya Marekani kuwaondoa wanajeshi wake nchi humo, kundi hilo limeweza kutwaa miji mingi na hatimaye kudhibiti nchi takriban nzima.


Tangu kundi hilo lilipojitangazia ushindi Jumapili Agosti 15 mwaka huu, maswali yameibuka juu ya muelekeo wa mpya wa Afghanistan.


Mosi: Ni kwa vipi kundi hilo lina uwezo wa kuiongoza nchi hiyo ambayo kwa sasa ni kama inadondoka kabisa, katika kila nyanja. Wadadisi wa mambo wanajiuliza wapi kundi hilo litapata fedha za kuendesha Serikali na ni kwa kiasi gani viongozi wake wana ujuzi wa masuala ya utawala wa kuikoa nchi iliyo dhooful-hali hususan kiuchumi na kisiasa.


Tayari kundi hilo limefanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa zamani wa Afghanistan akiwemo, Rais mstaafu, Hamid Karzai kuangalia jinsi ya kuliongoza taifa hilo. Hata hivyo kuna wasiwasi kuwa huenda mazungumzo hayo yasizae matunda kwa sababu ya msimamo mkali wa kundi hilo linalofuata itikadi kali za Kiislamu; wakati makundi mengine yanaonekana kuwa na msimamo wa wastani.


Katika kipindi hiki ambapo kundi hilo ndio lina ushawishi mkubwa, endapo mazungumzo hayo yatashindwa, Afghanistan itaendelea kupitia kipindi kigumu.


Viongozi wakuu wa mataifa makubwa akiwemo Waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson wamelitaka kundi hilo kushirikisha makundi mengine katika utawala, la sivyo hawatautambua utawala wa Taliban. Kwa sasa ni China, Urusi na Iran ndio wanaonekana kuwa nyuma ya Taliban.


Wananchi wa Afghanistan na dunia kwa ujumla wanasubiri kuona jinsi kundi hilo litakavyoiendesha Afghanistan. Pili: Fikra zimekuwa zikigongana juu ya jinsi kundi hilo linavyoweza kutorejea ‘makosa’ iliyoyafanya katika utawala wake wa takriban miaka 7 kuanzia mwaka 1996 hadi 2001.


Katika kipindi hicho, Talibna waliiongoza nchi hiyo kwa tafsiri yao kali ya sheria za Kiislamu (sharia).


Kutokana na historia hiyo, mamia ya watu wamekuwa wakiikimbia nchi hiyo wakihofia kurejeshwa kwa sheria hizo kali. Wapo wanaorejea kumbukumbu ya enzi za utawala wa kundi hilo na wapo ambao wamekuwa wakihadithiwa mambo yalivyokuwa.Masuala ya wanawake/wasichana kunyimwa fursa ya kwenda shule, kuwekwa mbali na harakati za utawala na kukatazwa hata kufanya baadhi za shughuli za kiuchumi. Pia, ilidaiwa kulikuwa na uvunjaji wa haki za binadamu na tuhuma kuwa Taliban ilikuwa ikihifadhi magaidi.


Tayari Taliban wameshatangaza kuwa ‘model’ yao ya kuiongoza Afghanistan itakuwa ya sheria za Kiislamu. Hata hivyo, Taliban kupitia kwa msemaji wao, Zabihullah Mujahid, wameiambia dunia kuwa pamoja na kutumia mfumo huo, kwa sasa mambo yatakuwa tofauti.


Msemaji huyo pia alisema kuwa haki za wanawake na wasichana zitaheshimiwa, ikiwemo kushirikishwa kwenye serikali na kuruhusiwa kwenda shule.


“Hatutaruhusu ubaguzi dhidi ya wanawake, lakini maadili ya Kiislamu ndio muongozo wetu,” alisema Mujahid.


Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaona hayo ni maneno tu, kwenye, na kwamba vitendo vitakuwa tofauti. Jambo kubwa zaidi ambalo linaonekana kuibua mijadala ni kauli ya Taliban kuwa safari hii watatawala kwa namna tofauti, hasa kwa upande wa masuala ya wanawake.


Kama kweli Taliban watakuwa tofauti, wataulizwa mafundisho yapi ya Kiislamu waliyatumia kipindi cha utawala wao wa mwaka 1996 hadi 2001 ukilinganishwa utawala wa safari hii?


Tayari baadhi ya watu wakiwemo Waislamu wenyewe wamekuwa wakihoji kama kundi hilo linaakisi kweli mafundisho ya Kiislamu. Hiyo ni kutokana na matendo yao na pia vyanzo vyao vya mapato.


Kwa mujibu wa Gazeti la Arabnews la Agosti 18 mwaka huu, Taliban hupata takribani dola bilioni 1.5 kwa kuwalazimisha kukusanya kodi kibabe na uuzaji wa mihadarati iliyokuwa ikipatikana katika maeneo waliyokuwa wakiyakidhibiti.


Hata hivyo, uwepo wa mihadarati nchini Afghanistan sio suala geni au la kushtusha. Biashara hiyo imekuwa ikitumiwa na mashirika kadhaa ya kijasusi ya nchi za magharibi katika kufadhili operesheni zao za wazi na za siri duniani kote. Profesa Mahmoud Mamdan amelieleza hili vizuri katika kitabu chake, ‘Bad Muslim, Good Muslim, America’s war on terror’.

0 Comments