October 2, 2021

Mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mmoja wa Waislamu wa Rohingya

 Polisi ya Bangladesh imesema Mohibullah alipigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana katika kambi ya Kutupalong huko Cox's Bazar. 


Zaidi ya Waislamu milioni moja wa Rohingya wamekimbia nyumba na makazi yao nchini Manmar kutokana na ukatili na mauaji ya kutisha yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali, na sasa wanaishi katika kambi za wakimbizi katika nchi jirani hususan Bangladesh. Jinai na uhalifu unaofanywa na Mabudha wa Myanmar wakishirikiana na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya hasa katika jimbo la Rakhin ulianza mwaka 2012 na kufikia kileleni mwaka


2017.Rohingya

Waislamu wa jamii hio huko Myanmar ambao wametajwa na Umoja wa Matafa kuwa ndiyo kaumu inayodhulumiwa zaidi duniani, wanaishi katika mazingira na hali ya kuhuzunisha sana katika kambi za wakimbizi hususan huko Bangladesh. Muhammad Mohiibullah ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Warohingya wa Arakan anasema: "Watenda jinai wa Myanmar ni mithili ya wezi ambao kamwe huwa hawakiri makosa yao, lakini viongozi wa jamii ya Waislamu wa Rohingya wamewasilisha nyaraka na ushahidi wa kutosha mahakamani wakiwa na nia ya kuthibitisha uhalifu na jinai zilizofanyika dhidi ya Waislamu, suala ambalo linawatia wasiwasi mkubwa watenda jinai hao."

Kufichuliwa kwa jinai na uhalifu wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali na wanajeshi wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya kumewatia wasiwasi na wahka mkubwa kiasi cha kuanza kuwafuta na kuwamaliza kabisa viongozi wa jamii hiyo. Mauaji hayo kwa maneno mengine ni wenzo wa kuzima sauti ya kupigania haki na kweli na kuwanyamazisha viongozi wa jamii ya Waisalmu wa Rohingya wanaopaza sauti kuieleza dunia yanayofanyika nchini Myanmar. Ripoti zinasema kuwa, Mohibullah alikuwa kiongozi wa wakimbizi karibu milioni moja wa Rohingya nchini Bangladesh, akiandika kuhusu uhalifu wa jeshi la Myanmar dhidi ya Rohingya na kutetea haki za wakimbizi katika majukwaa ya kimataifa. 


Meenakshi Ganguly ambaye ni Mkurugenzi wa Asia Kusini katika Human Rights Watch anasema: "Mohibullah alikuwa sauti muhimu kwa jamii ya Rohingya ambayo inasumbuliwa na mashaka na maumivu yasiyotasawarika tangu walipofika nchini Bangladesh kama wakimbizi ." Mwakilishi huyo wa Human Rights Watch anasema: "Mohibullah daima alitetea haki za Warohingya za kuishi salama na kwa heshima na kuwa na maoni katika maamuzi yanayohusu maisha yao na siku zijazo. Kuuawa kwake ni dhihirisho la hatari zinazowakabili wale wanaoishi katika kambi ambao wanafichua kwa sauti kubwa ukatili unaofanywa dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema kuwa, mauaji ya Mohibullah yanadhoofisha sio tu mapambano ya wakimbizi wa Rohingya ya kupigania haki zaidi na udharura wa kuimarishwa ulinzi katika kambi za wakimbizi, lakini pia juhudi zao za kutaka kurudi salama nchini kwao, Myanmar. Human Rights Watch imesisitiza kuwa, mamlaka ya Bangladesh inapaswa kuchunguza kwa haraka mauaji ya Mohibullah na mashambulizi mengine dhidi ya wanaharakati wa Rohingya katika kambi hizo. 

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only