Una Vitamini za Kutosha? Angalia Dalili Hizi

Vitamini ni moja kati ya viini lishe muhimu sana katika mwili wa binaadamu. Umuhimu huu unatokana na shughuli mbalimbali ambazo ufanisi wa kufanyika kwake hutegemea vitamini. Kabla ya kujionea dalili mbalimbali ambazo hutokea katika mwili, ni vyema tukatambua kazi mbalimbali za viini lishe hivi.Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na kuboresha afya ya meno, mifupa, ngozi, kutengeneza damu, kugandisha damu, kutengeneza vichocheo, kuyeyusha baadhi ya sumu mwilini pamoja na kazi nyengine nyingi. Ni muhimu sana kuhakikisha kuwa miili yetu inapata vitamini za kutosha ili kuepuka kupata madhara na magonjwa mbalimbali. Hapa tutataja baadhi ya dalili za kukosa vitamini.


  • Kupata vidonda mdomoni

Pengine hii ni moja ya dalili inayofahamika na wengi. Pia vidonda hivi huweza kutokea kwenye ncha za midomo na huwa na rangi nyeupe na hujulikana kama ‘makinda’. Kitaalamu, vidonda hivi hujulikana kama ‘angular chelitis’ na hutokea tu ikiwa kutakua na upungufu wa vitamini aina ya B1, B2 na B6 pamoja na upungufu wa madini ya chuma.


Ili kuepukana na ugonjwa huu wa vidonda ni lazima kuhakikisha tunapata aina tajwa za vitamini. Vitamini hizi zinaweza kupatikana katika vyakula mbalimbali kama vile samaki, nyama, maziwa na bidhaa zake, maini, mboga za kijani pamoja na mimea jamii ya kunde.


  • Kunyonyoka nywele na kucha

Dalili hizi mara nyingi huwapata watoto wenye utapia mlo, mama wajawazito, watumiaji sugu wa madawa ya kuulia bakteria [antibiotics], wavutaji sigara pamoja na wanywaji pombe kupindukia. Kupata dalili hizi kunaashiria upungufu wa vitamini aina ya B7 ambayo pia upungufu wake huweza kuleta hali ya uchovu, maumivu ya misuli, ganzi miguuni na mikononi.


Kuepukana na tatizo hili wagonjwa wanashauriwa kula kwa wingi vyakula kama vile viazi vitamu, uyoga, nafaka nzima, karanga, korosho na ndizi.


  • Fizi kuvuja damu

Huenda ikawa hali ya kawaida kwa watu wengi kuvuja kiasi kidogo cha damu wakati wa kupiga msuwaki. Kitendo hiki hutokea ikiwa nguvu kubwa itatumika katika kusugua fizi na damu hii huacha kutoka baada ya muda mfupi ila hali huwa tofauti ikiwa kutakua na upungufu wa vitamini C kwani damu hii huendelea kutoka kwa muda mrefu kidogo na muda mwingine hutoka bila ya hata kuwa na sababu maalum.


Tatizo hili linaweza kudhibitiwa kwa kuhakikisha kutumia vyakula vinavyoupatia mwili vitamini hii ambavyo ni mboga mboga na matunda kama vile machungwa, chenza na mengine mfano wa hayo.


  • Uoni hafifu na madoa meupe machoni

Uoni hafifu hasa nyakati za usiku husababishwa na ukosefu wa vitamini A katika mwili. Kama hali hii usipotibiwa, mboni za macho huweza kuathirika zaidi na mwishowe kusababisha upofu. Ili kujikinga na hali hii ni muhimu kuipatia miili yetu vitamini A kwa kutumia vyakula kama vile maini, figo, moyo, mayai, maziwa pamoja na mboga za majani.


  • Kutoka mbalanga na mba

Ingawa ukosefu wa madini ya zinki unaweza kuwa ni chanzo, lakini pia ukosefu wa vitamini B2, B3 na B6 huchangia kwa kiasi kikubwa kupata maradhi haya. Pia maradhi haya huwapata zaidi watoto chini ya miezi mitatu, vijana walio katika umri wa balehe pamoja na vijana wa umri wa kati. Tatizo hili linaweza kuondoka ikiwa wagonjwa watakua na tabia ya kula mboga za majani, karanga, nyama, samaki na vyakula vyengine mfano wa hivyo.


  • Kupata upele mweupe

Mara nyingi upele huu hutokea zaidi nyuma ya viwiko vya mikono. Pia vipele hivi vinaweza kuwa vyekundu na kua na kama kijinywele cheupe katikati. Upele huu huwapata zaidi watoto wenye upungufu wa vitamini A na huondoka wenyewe kadri umri unavyoongezeka.


  • Vipi tukabiliane na tatizo

Kama tulivyojionea katika kila kipengele ya kuwa dawa bora ya kukabiliana na matatizo haya ni chakula bora. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kula chakula bora kinachohusisha mlo kamili ambao unajumuisha vyakula vya wanga, protini, mboga mboga pamoja na matunda.

0 Comments