Hofu kutokana kutoweka na kuuawa Waislamu Kenya

 Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la kutoweka na kuuawa Waislamu nchini Kenya na sasa viongozi wa Kiislamu nchini humo wanataka serikali itoe majibu.


Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SUPKEM) linasema tokea Januari hadi Novemba mwaka 2021 Waislamu wasiopungua 40 wametekwa nyara na watu wasiojulikana na ni 10 tu walioweza kurejea katika familia zao. Idadi hiyo haijajumuisha Waislamu wanaotekwa nyara katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya ambalo linapakana na Somalia.


Viongozi wa Kiislamu nchini Kenya wanasema kampeni ya serikali dhidi ya ugaidi sasa imegeuka na kuwa vita dhidi ya Uislamu na Waislamu. “Tunashuhudia kampeni ya makusudi ya kuingiza hofu na wahka miongoni mwa Waislamu ili wasiende misikitini, “ amesema Katibu Mkuu wa SUPKEM, Sheikh Hassan Ole Naado amesema.


“Pamoja na kuwa tumeitaka serikali ichunguze na isitishe ukiukaji wa haki za Waislamu, dola limeamua kubakia kimya,” amesema Ole Naadi.


Taarifa zinasema aghalabu wanaotekwa nyara ni wasomi na wafanyabiashara Waislamu ambapo, wale wanaoachiliwa huru baada ya kutekwa nyara na watu wanaoaminika kuwa ni maafisa wa usalama wanarejea  nyumbani wakiwa na udhaifu mkubwa na msongo wa mawazo.


Kenya imeshuhudia hujuma za magaidi wa kundi la al Shabab la Somalia linalofungamana mtandao wa Al Qaeda. Kufuatia hujuma hizo serikali ya nchi hiyo imekuwa ikitekeleza oparesheni za kuwakamata washukiwa wa ugaidi.


Viongozi wa Kiislamu wanalaani ugaidi vikali lakini wanasisitiza kuwa washukiwa wa ugaidi wanapaswa kufikishwa katika vyombo vya mahakama na mkondo wa sheria kufuatwa kama wanavyofanyiwa wahalifu wengine wote nchini humo.


Miongoni mwa Waislamu mashuhuri waliotekwa nyara na watu wasiojulikana na kisha kuachiliwa huru ni Profesa Hassan Nandwa msomi wa Kiislamu na wakili ambaye alitekwa nyara Oktoba 28 alipokuwa akitoka Msikiti wa Jamia mjini Nairobi baada ya Sala. Nandwa alikuwa wakili wa mshukiwa wa ugaid.


Siku 10 baadaye alipatikana nje ya makaburi ya Waislamu katika mji wa Mwingi ulio kilomita 170 kutoka Nairobi.


Mwezi Septemba pia msomi mwingine wa Kiislamu ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya usalama Profesa Abdiwahab Abdisamad alitekwa nyara na kupatikana siku 12 baadaye.


SUPKEM inasema wiki mbili kabla ya kutekwa nyara Profesa Nandwa, kijana Mohammad Abubakar Said, 22, naye pia alitekwa nyara nje ya msikiti mjini Mombasa na tokea wakati huo hajaonekana tena. Yassin Mahmoud, dereva wa ambulensi Kaunti ya Lamu na mfanya biashara mashuhuri Hassan Dahir Osman, mfanya biashara katika mtaa wa Eastleigh Nairobi nao tokea Juni wametokewa na hawajapatikana hadi sasa.


“Waislamu nchini Kenya wako chini ya mzingiro. Wanalengwa na tunana haki za binadamu zikiwa zinakiukwa kwa kiwango kikubwa,” anasema Sheikh Abdullahi Abdi, mwenyekiti wa Jukwaa la Viongozi wa Kiislamu Kenya. “Tutawahamasisha Waislamu wote kuhakikisha kuwa haki zetu zinalindwa,” ameongeza.


Hivi karibuni viongozi wa jumuiya za Kiislamu, watetezi wa haki na mawakili waliandamana nje ya Mahakama Kuu jijini Nairobi kulaani ongezeko la visa vya kutekwa nyara Waislamu na mauaji ya kiholela.


Akizungumza katika maandamano hayo, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassri alisema: “Hatutakubali mkondo huu uendelee.” Amesema atashirikiana na mawakili kuwakilisha maombo ya kutaka Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai afutwe kazi kutokana na maafisa wa usalama kukiuka sheria.


Naye Bernard Ng’etich, mwanachama mwandamizi wa Chama cha Mawakili Kenya (LSK) amesema wamempa rais Uhuru Kenyata muhula wa mwezi moja kumfuta kazi Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’I kushindwa kuzuia mauaji na utekaji nyara wa Waislamu

0 Comments