Wenye chuki wahujumu biashara za Waislamu Marekani

Watu wanaoaminika kuwa na chuki dhidi ya Uislamu sasa wanalenga biashara zinazomilikwa na Waislamu nchini Marekani.


Katika matukio ya miezi ya hivi karibuni migahawa mitatu ya Waislamu ilishambuliwa na watu wenye chuki dhidi ya Uislami katika eneo la Catonsville, jimboni Maryland Marekani.


Katika tukio la karibuni kabisa, Ijumaa asubuhi watu wanaoaminika kuwa na chuko dhidi ya Uislamu walishambulia migahawa ya Champs Pizza na Winge katika barabara ya Reisterstown na kuiba vitu vifaa kadhaa pamoja na pesa taslimu. Taswira za kamera za usalama zinaoneysha mtu aliyejifunika uso akiingia Champs Pizza kutekeleza uhalifu.


Kufuatia hali hiyo, Baraza la Uhusiano wa Uislamu na Marekani (CAIR), ambalo hutetea haki za Waislamu, limewataka Waislamu wachukua tahadahri zaidi katika biashara zao.


Zainab Chaudry, mkurugenzi wa ofisi ya CAIR katika jimbo la Maryland amesema ingawa bado hakuna taarifa kamili kuhusu waliotekeleza hujuma hizo lakini kuna haja ya Waislamu kuchukua tahadhari. "Kuna haja ya kuchukua tahadhari katika mazingira hayo ya ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu kitaifa na kimataifa. Tunawahimiza Waislamu watume ripoti kuhus tukio lolote lisilo la kawaida," amesema Chaudry.


CAIR imewahimiza Waislamu waweke kamera za siri katika biashara zo na kutoacha nyaraka muhimu katika maeneo yao ya biashara.


Ripoti iliyotolewa na CAIR mwezi Aprili ilibaini kuwa Marekani kumeshuhudiwa ongezeko la asilimia 9 ya idadi ya malalamiko ya unyanyasaji dhidi ya Waislamu ambayo yalipokewa mwaka uliopita wa 2020 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.


Kwa upande wake Baraza la Jumuiya za Kiislamu nchini Marekani limemwandikia barua Rais wa nchi hiyo, Joe Biden likisisitiza kuwa, kuwepo mwakilishi maalumu wa kusimamia na kupambana na chuki na propaganda chafu dhidi ya Uislamu kunaweza kusaidia juhudi za kupata suluhisho la tatizo hilo ambalo linaizonga jamii ya Waislamu nchini Marekani. 


Ikulu ya Rais wa Marekani, White House hadi sasa haijatoa jibu iwapo serikali ya nchi hiyo itateuwa mwakilishi maalumu wa kushughulikia chuki na propaganda chafu dhidi ya Uislamu au la. 

0 Comments