Chuki dhidi ya Uislamu ni tishio kubwa kwa Waislamu Ufaransa

Sera rasmi ya serikali ya Ufaransa ya kubana uhuru wa Waislamu sasa imefika kiasi ambacho hakiwezi kustahamiliwa tena.


Misikiti inafungwa moja baada ya mwingine kwa sababu zisizo na msingi, maamuzi  yanayochukuliwa yanakiuka uhuru wa kuabudu wa Waislamu huku kuzuiwa Waislamu katika maeneo ya umma kukiwa ni jambo la kawaida.


Kufanya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) kuwa jambo la kawaida sasa ni sera ya wanasiasa kote Ufaransa. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa sasa imezindua laini maalumu ya simu ambapo imewataka raia kuripoti 'misimamo mikali ya Kiislamu.' Kimsingi ni kuwa hivi sasa kila Muislamu  Ufaransa anatazamwa kama mshukiwa wa uhalifu.


Mwaka jana Taasisi ya Kukabiliana na Chuki Dhidi ya Uislamu Ufaransa, ambayo ilikuwa moja ya asasi kubwa za Waislamu nchini humo, ilifungwa kufuatia uamuzi wa baraza la mawaziri.


Bunge la Ufaransa pia limepitisha   sheria ya 'thamani za jamhuri' ambazo zilipendekezwa na rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na kile alichokitaja ni 'Uislamu wa wanaotaka kujitenga.'


Kwa ujumla katika miaka ya karibuni wimbi la chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa limeshadidi ambapo hasa katika uongozi wa Emmanuel Macron ambapo Waislamu wengi wamekuwa waiandamwa kwa mashinikizo na vitendo vya bughuda na mauadhi na hata wakati mwingine matukufu ya dini yao kutusiwa na kuvunjiwa heshima.


Aidha mwezi MachiMkurugenzi wa Msikiti wa Paris Chems-eddine Hafez, mkurugenzi wa Msikiti wa Lyon Kamel Kapatano na mkurugenzi wa Msikiti wa Evry wametoa taarifa ya pamoja na kusema amri ya Wizara na Kilimo na Chakula Ufaransa ya kupiga marufuku uchinjaji wa kuku kwa misingi ya Uislamu ni jambo ambalo linatoa ishara hasi kwa Waislamu nchini humo  katika kipindi hiki cha kukaribia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


Aidha  katika kitendo kinachoashiria chuki ya wazi dhidi ya Waislamu supamaket moja ya Paris imelazimishwa na wakuu wa mji huo kuuza nyama ya nguruwe na pombe, bidhaa  ambazo ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu. Supamaket hiyo inyojulikana kama 'Good Price' iliyo katika mtaa wa Colombes mjini Paris ilifahamishwa kuwa leseni yake itabatilishwa iwapo haitatii amri ya kuuza pombe na nyama na nguruwe.


Mwaka huu pia maafisa wa serikali za mitaa Ufaransa wametumia visingizio kufunga biashara za Waislamu ikiwa ni katika kutekeleza sera jumla za Rais Emmanuel Macron ambaye ameanzimia kuwadhoofisha Waislamu nchini humo.


Kwa kuzingatia kuwa uchaguzi wa Ufaransa utafanyika Aprili 2020, wanasiasa nchini humo wanajaribu kuvutia kura za wapiga kura wa mrengo wa kulia kwa kueneza chuki dhidi ya Uislamu. Kwa msingi huo hali ya Waislamu inatazamiwa kuwa mbaya zaidi wakati huu wa kkukaribia uchaguzi mkuu nchini humo.


Ufaransa ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016, kuna zaidi ya Waislamu milioni 5.7 Ufaransa ambao ni takribani asilimia 8.8 ya watu wote nchini humo.

0 Comments