Hatua kali misikitini Saudia kufuatia ongezeko la maambukizi ya COVID-19

Misikiti kote Saudi Arabia imetakiwa kuchukua hatua kali za kuhakikisha kuwa wote wanaoshiriki katika ibada wanatekeleza kanuni za kukabiliana na COVID-19.


Amri imetolewa na Waziri wa Masuala ya Kiislamu Saudia Abdulatif Aal Sheikh kufuatia ongezeko la maambukizi ya COVID-19 katika ufalme huo. Katika dikrii yake, ametaka wasimamizi wa misikiti kuhakikisha wanaoshiriki katika ibada wanazingatia kanuni zote za kiafya hasa uvaaji barakoa na kutokaribiana ili kuzuia maambukizi ya COVID-19.


Agizo hilo limetolewa baada ya kubainika kuwa watu wanapuuza kanuni zilizowekwa misikitini kuhusiana na maambukizi ya COVID-19 na hivyo kuchangia ongezeko la maambukizi.


Siku ya Alhamisi Saudi Arabia iliripoti maambukizi mapya 287 ya corona huku mtu moja akipoteza maisha. Hadi sasa walioambukizwa corona Saudia ni 551,749 na walipoteza maisha ni 8,868.

0 Comments