Imamu wa Msikiti Columbus Marekani auawa, uchunguzi waanza

Polisi katika mji wa Columbus jimboni Ohio Marekani wameanzisha uchunguzi kufuatia mauaji ya Imamu wa msikiti mmoja katika mji huo.


Polisi wametangaza Ijumaa kuwa Mohamed Hassan Adam, mwenye asili ya Somalia, aliuawa lakini haijulikani ni nani aliyetekeleza mauaji hayo na uchunguzi umeanzishwa.


Watu wa jamii ya Wasomalia wanasema mwili wa Imamu huyo ulipatikana katika eneo lenye miti mingi katika Barabara ya Windsor Ijumaa.  Adam alikuwa hajaonekana tokea Jumatano na ripoti ya kutoweka kwake ilifikishwa kwa polisi Alhamisi.


Kaimu Mkurugenzi wa Tawi la Ohio la Baraza la Uhusiano wa Marekani-Kiislamu (CAIR), Amina Barhumi amesema Adam alikuwa nguzo katika jamii ya Waislamu mjini Columbus. Amesema kifo cha Adam ni pigo kubwa kwa Waislamu wote Ohio na ametaka  vyombo vya sheria kufanya uchunguzi kamili na wa wazi wa mauaji ya kiongozi huyo wa jamii ambaye pia alikuwa ni mume na baba.


CAIR imetangaza zawadi ya dola elfu 10 kwa yeyote atakayetoa taarifa kuhusu mauaji ya Adam.


Meya wa Columbus Andrew Ginther ametuma salamu zake za rambi rambi kwa jamii, familia na marafiki wa Mohamad Hassan Adam na kumtaja kuwa kiongozi wa kidini aliyejitolea kuwongoza Wasomali mjini Columbus. Aidha amesema polisi wanachunguza mauaji hayo.

0 Comments