Kufichuliwa ujasusi wa kundi la Kizayuni dhidi ya taasisi za Kiislamu nchini Marekani

 Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu CAIR limefichua kuwa, genge moja la maadui wa Uislamu nchini Marekani linashirikiana na mashirika ya kijasusi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na limeunda kanali maalumu ya siri ya kujipenyeza na kufanya ujasusi katika safu za Waislalmu.


Baraza hilo limesisitiza kuwa, limefanikiwa kugundua na kuvunja njama za genge hilo lililo dhidi ya Uislamu na ambalo lilijaribu kujipenyeza na kufanya ujasusi katika ofisi ya Columbus ya baraza hilo katika jimbo la Ohio. 


Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu CAIR ambayo ni taasisi kubwa zaidi ya Kiislamu nchini humo limesisitiza pia kuwa, mwaka jana ilibainika kwamba Romin Iqbal, mkurugenzi wa zamani wa utendaji na wa sheria wa ofisi ya baraza hilo huko Columbus, kumbe alikuwa ni jasusi wa genge moja lenye chuki na uadui mkubwa na Waislamu lijulikanalo kwa jina la Investigative Project on Terrorism.


Whitney Siddiqi, mkurugenzi wa masuala ya jamii ya Waislamu wa Ohio wa baraza hilo anazidi kufichua ukweli huo akisema, mkurugenzi mtendaji wa zamani wa ofisi ya baraza hilo huko Columbus, alivujisha taarifa za siri za baraza hilo ikiwa ni pamoja na email na sauti za vikao vya viongozi wa ngazi za juu wa baraza la CAIR na kuzikabidhi kwa genge hilo la maadui wa Uisalmu.  Ushahidi mbalimbali unaonesha kuwa, genge hilo linaloendesha harakati zake kwa ajili ya kuupiga vita Uislamu, lina ushirikiano wa karibu na shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni ambalo lina ofisi zake katika ofisi ya waziri mkuu wa Israel  ambaye wakati huo alikuwa ni Benjamin Netanyahu.

Kufichuliwa ushirikiano baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na genge linaloeneza chuki dhidi ya Uislamu katika kuwafanyia ujasusi Waislamu wa Marekani, kunazidi kuonesha hali halisi ya genge hilo pamoja na namna utawala wa Kizayuni unavyotumia hila na njama za kila namna kudhihirisha uadui wake kwa Waislamu. Chuki na uadui bali hata vitendo vya kushambuliwa Waislamu vimeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni huko Marekani. Vitendo hivyo vilipamba moto na viliongezeka sana wakati wa urais wa miaka minne wa Donald Trump. Rais huyo wa zamani wa Marekani alikuwa akitoa maneno machafu na makali mno dhidi ya wafuasi wa dini za wachache na kaumu na jamii za watu wachache huko Marekani hasa Waislamu.


Taasisi za Kiislamu likiwemo Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu CAIR mara nyingi zimekuwa zikilalamikia kuongezeka vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu katika kona mbalimbali za Marekani. Hata mwaka jana kuliripotiwa vitendo vingi vya kushambuliwa Waislamu na Misikiti katika maeneo tofauti ya Marekani. Kuvamiwa Misikiti na kuchomwa moto maeneo ya ibada ya Waislamu, kushambuliwa moja kwa moja Waislamu kimwili na kwa maneno ya chuki na kubaguliwa waumini wa dini hiyo takatifu katika sehemu mbalimbali zikiwemo za masomo na ajira, ni baadhi tu ya mifano ya wazi kuongezeka na kukita mizizi chuki dhidi ya Waislamu katika jamii ya Marekani. Ripoti za makundi ya kutetea haki za raia zinaonesha kuwa, kueneza chuki nchini Marekani ni sehemu ya siasa kuu na pana za kupiga vita Uislamu nchini humo na dunia kwa ujumla. 


Ripoti zilizoenea katika vyombo vya habari vya Marekani zinaonesha kuwa, taasisi za usalama za nchi hiyo kama vile polisi wa FBI  zinachochea chuki dhidi ya Uislamu. Ijapokuwa mwanzoni mwa urais wake Barack Obama alijaribu kubadilisha siasa hizo kuu za Washington na aliwaahidi Waislamu kuwalindia haki zao, lakini vitendo vya chuki na uadui dhidi ya Waislamu havijawahi kupungua hata mara moja huko Marekani. Kama tulivyotangulia kusema vitendo hivyo vilipamba moto baada ya urais wa Barack Obama na wakati alipoingia madarakani Donald Trump ambaye alitumia miaka minne ya urais wake kutoa maneno makali na ya kejeli na kuchukua hatua za wazi dhidi ya Waislamu na Uislamu na kuchochea mno chuki dhidi ya dini hiyo takatifu. Tukumbuke pia kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi, rais wa hivi sasa wa Marekani, Joe Biden aliahidi kupambana na ubaguzi na chuki dhidi ya Waislamu lakini hadi hivi sasa ameshindwa kufanya chochote cha maana.


Sasa hivi pia, umefichuliwa ujasusi wa genge moja lenye misimamo mikali na chuki za kupindukia linaloshirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel kujipenyeza na kufanya ujasusi dhidi ya Waislamu wa Marekani, tena wakati huu wa urais wa Joe Biden aliyeahidi kulinda haki za Waislamu nchini humo.

0 Comments