Mkutano wa OIC kuhusu Afghanistan unafanyika leo Islamabad, Pakistan

 Mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) unafanyika leo Jumapili katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad kwa shabaha ya kujadili namna ya kuisaidia Afghanistan ambayo inajongewa na maafa ya kibinadamu.


Akizungumza kabla ya kuanza mkutano huo Shah Mehmood Qureshi Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan amesema kuwa, lengo la kikao cha Islamabad ni mkusanyiko wa kimataifa kwa ajili ya kuisaidia Afghanistan.


Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan ambaye nchi yake ndio mwenyeji wa mkutano huo amesema kuwa, ajenda kuu na pekee ya mkutano huo ni kuchunguza matukio ya Afghanistan hususan hali ya kibinadamu katika nchi hiyo.


Shah Mehmood Qureshi ameyataka mataifa ya Kiislamu kutoitelekeza Afghanistan na kuongeza kuwa, atautumia mkutano huo kuwakumbusha wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa nchi wanachama wa OIC kuiunga mkono Afghanistan na watu wake licha ya kwamba jumuiya hiyo haijautambua rasmi utawala wa kundi la Taliban.


Tangu wanamgambo wa Taliban waliposhika tena hatamu za uongozi nchini Afghanistan Agosti 15 mwaka huu (2021), Pakistan ndio nchi pekee ambayo imetoa himaya kubwa zaidi ya kisiasa kwa kundi hilo katika eneo na katika uga wa kimataifa. Mkakati muhimu zaidi kwa sasa wa Pakistan kuhusiana na kuliunga mkono kundi la wanamgambo wa Taliban ni kusaidia kuzikinaisha nchi na asasi mbalimbali za kimataifa ili ziutambue rasmi utawala wa kundi hilo.


Pakistan leo ni mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu {OIC} katika hali ambayo, hivi karibuni kundi la Taliban liilitaka jumuiya hiyo kuutambua rasmi utawala wake nchini Afghanistan. Mataifa ya Kiislamu kama ilivyo jamii ya kimataifa nayo yamekuwa na kigugumizi kikubwa katika kuitambua rasmi serikali ya Taliban nchini Afghanistan.

0 Comments