Nasaha kwa akinamama, dada wa Kiislamu

 


Ndugu zangu, leo hii katika safu hii ya familia naomba nitoe nasaha tu kuhusu kwa wakinadada na wanawake wenzangu.

Akinamama, wote twajua kuwa uhuru ni jambo adhimu ambalo kila binadamu analihitaji. Kwa mujibu wa Uislamu, msingi wa uhuru binafsi wa mtu ni kufikia ukamilifu katika kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kupata radhi zake.

Hata hivyo, kuna ambao hutumia uhuru waliopewa kwa kufanya mambo kinyume. Hawa ni wale wanaoutazama uhuru kama fursa ya kutenda mambo bila mipaka, vizuizi, ukomo wala masharti mithili ya wanyama.

Mtazamo huu batili unawafikiana kwa karibu na ule wa wanafalsafa wengi wa kimagharibi wanaoamini kuwa, chimbuko na msingi wa uhuru ni kutoa haki kwa watu kufanya mambo kwa mujibu wa utashi na matamanio yao kwa sharti la kutokuvunja sheria na taratibu za nchi.

Kimsingi hakuna uhuru wa kufanya mambo machafu na maovu. Uhuru lazima uwe na masharti na mipaka maalum iliyowekwa na Mola Muumba.

Kinamama wenzangu, miongoni mwa wale wanaotumia vema uhuru ni waja wa Allah ambao hutumia fursa ya uhai kutenda mema. Wanafanya hivyo wakitambua fika kuwa kuwepo kwao duniani ni kwa ajili ya kufanya biashara na Mola wao.

Kinyume na hao kuna ambao huwekeza nguvu kubwa katika kustawisha duniana kuisahau Akhera wakiamini furaha yao itakamilishwa kwa burudani na starehe za Dunia. Watu wa aina hii hawawezi kuwa sawa na wale wanaotii amri za Allah Ta’ala ambao mara zote wanapokumbushwa kuwa duniani mahala pa mtihani hujitahidi kufanya mambo ya kheri na kujizuia na haramu.

Allah Ta’ala anatukumbusha akisema: “Je! Wanadhani wanaotenda maovu kuwa tutawafanya kama walio amini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni hukumu mbaya wanayo ihukumu!” [Qur’an, 45:21].

Aya hii ni dalili ya majuto yatakayowapata wale ambao Duniani hawakuishi kwa mujibu wa matakwa ya dini. Hali halisi ni kwamba wengi tumepotezwa na anasa za duniatukitumai kuishi muda mrefu, na hivyo kutumia fursa ya ujana kukithirisha kutenda maasi.

Ndugu kinamama, hivi ulishawahi kujiuliza kwanini hutaki kumuabudu Mola wako ilihali hujui wakati gani utafikwa na umauti? Na je, ni kwa kiwango gani unamkumbuka Mola wako kwa kumdhukuru na kuisoma Qur’an. Na mara ngapi umemuomba msamaha Allah kutokana na mabaya unayotenda kila uchao. Ikiwa ni miongoni mwa watu wa aina hii basi chukua hatua kwa kujilazimisha kusimamisha swala, kuwaheshimu watu, kutoa swadaka na kuwasaidia wahitaji.

Ewe dada/mama wa Kiislamu, ishi kwa kumhofu Allah kwani kufanya hivyo kutabadilisha tabia na mwenendo wako mbaya. Badili maisha yako kwa kuifanya Hijab kuwa kipaumbele cha kwanza.

Hijab haikuja isipokuwa ni kwa ajili ya kuhifadhi na kulinda heshima na utu wako dhidi ya ufisadi wa kimaadili Hakika Mwenyezi Mungu hapendi tabia ya kujidhalilisha kwa kutembea utupu, bali anataka ujitofautishe na wanawake wa Wayahudi na Wakristo kwa vazi la sitara la Hijab ili uthaminike.

Hakuna faida kwa mwenye kuiacha Hijab isipokuwa kupata hasara ya Duniani na Akhera. Kumbuka wanaokupenda na kukusifu kwa sababu ya kuonesha maungo yako watakusahau pindi utakapokufa.

Zinduka ewe mja wa Allah, tubu haraka kabla haujatembelewa na Malaika wa kifo.Uza duniayako kwa kushikamana na Hijab kwani ridhaa ya Allah ni bora kuliko ya wanadamu.Usiwe mwenye fikra potofu kwa kuiona Hijab kama vazi duni, linalokunyima uhuru na maendeleo.

Ewe dada/mama wa kiislamu, tambua Hijab ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwako, basi mtii na utekeleze amri yake ili upate kheri, utukufu na radhi zake.

Allah anasema: “Wala msionyeshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionyesha mapambo yao wanawake wa zama za ujahilia (ujinga). Na simamisheni swala na toeni zaka, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake (katika maamrisho na makatazo yao).” [Qur’an, 33:33].

Bila shaka mwenye kuiuza duniakwa matendo mema basi atakuwa amewekeza rasilimali muhimu mbele ya Mola wake, lakini mwenye kuiuza Akhera kwa kufanya maovu katika Dunia, hakika atakuwa miongoni mwa wenye kufanya bishara yenye khasara mara mbili (Duniani na Akhera). Jua ya kwamba, maisha ya duniani mchezo na starehe za muda mfupi, hivyo tahadhari na kuiga mambo kibubusa kwani kufanya hivyo kunakinzana na wajibu wa kumtii Allah na Mtume wake.

Allah anatuambia ndani ya Qur’an:“…Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kamili siku ya kiyama.Na atakayeepushwa na moto na akatiwa peponi basi huyo amefuzu.Na maisha ya duniasi kitu ila ni starehe ya udanganyifu.” [Qur’an, 3:185].

Tumuombe Allah atuepushie adhabu ya siku ya kiyama, atusamehe madhambi yetu na atuingize peponi kwa rehema zake, Insha Allah.

0 Comments