Pakistan, Uturuki na Malaysia kuasisi televisheni ya kupambana na chuki dhidi ya Uislamu

Waziri wa Habari na Turathi za Taifa wa Pakistan amesema, nchi hiyo kwa kushirikiana na Uturuki na Malaysia zitaanzisha chaneli ya televisheni kwa lengo la kukabiliana na kampeni za uenezaji chuki dhidi ya Uislamu duniani.


Uamuzi huo umechukuliwa katika kikao cha pamoja cha pande tatu kilichofanyika pembeni ya kikao cha jana cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kilichofanyika katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad.


Imetangazwa kuwa, lengo la kuasisi chaneli hiyo ya pamoja ya televisheni ni kukabiliana na uenezaji hofu na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na kutumia fursa na uwezo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kwa ajili ya kufikia malengo ya pamoja.


Wazo la kuanzisha kanali ya pamoja ya televisheni lilitolewa kwa mara ya kwanza na Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan katika kikao cha pande tatu alichofanya na Rais Recep Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu wa wakati huo wa Malaysia Mahathir Muhammad pembeni ya mkutano mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika Septemba 2017 mjini New York.

Chaneli hiyo ya televisheni itakayorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiingereza italenga kukabiliana na uenezaji chuki dhidi ya Uislamu kimataifa na kuondoa pia mtazamo potofu uliopo kuhusu dini hiyo tukufu.


Katika kikao chao hicho cha pamoja viongozi hao wa Pakistan, Uturuki na Malaysia walisisitiza pia kuchukuliwa hatua madhubuti na athirifu dhidi ya ubaguzi unaofanywa kwa misingi ya kidini, hasa ule wanaokabiliana nao Waislamu katika nchi za Magharibi.../

0 Comments