Qur'ani ya kidijitali ya maandishi ya nukta nundu yatengenezwa Saudia

Chombo cha kidijitali chenye Qur'ani Tukufu na tafsiri katika maandishi ya nukta nundu au braille kimeundwa Saudi Arabia kwa ajili ya wenye ulemavu wa macho.


Taarifa ya Idara ya Uongozi wa Misikiti Miwili Mitakatifu Saudi Arabia imesema wale wenye ulemavu wa macho sasa wataweza kusoma Qur'ani Tukufu na tafsiri yake kwa njia rahisi kwa kutumi chombo hicho cha kidijitali.


Taarifa hiyo imeongeza kuwa, jitihada za kina zinatakikana ili kuwa na miradi kama hii ya uvumbuzi kwa ajili ya kutumia teknolojia yenye kutoa huduma kwa Uislamu na Waislamu.


Hakuna taarifa zaidi zilizotelewa kuhusu chombo hicho.


Nukta nundu ni muwasilisho wa herufi kwa njia inayoshikika au kutambulika kwa vidole ambapo herufi na namba au hata noti za muziki na alama za kisayansi zinachorwa kiasi kwamba mtu asiyeona au mwenye uoni hafifu anaweza kutambua na kusoma kama kawaida.


Mbinu hii inatokana na mgunduzi wake Louise Braille kutoka Ufaransa ambaye aliigundua karne ya 19.


Matumizi ya nukta nundu huwezesha kundi hilo kusoma vitabu na majarida na hivyo kuimarisha ubobezi wao, uhuru na usawa katika nyanja mbalimbali.


Ibara ya 2 ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu inataja nukta nundu kama mbinu muhimu kwenye elimu, uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, kupata taarifa na mawasiliano mbalimbali.


Halikadhalika nukta nundu inasaidia ujumuishaji kwenye jamii kwa watu wasioona na wenye uoni hafifu kama ilivyobainishwa katika ibara ya 21 na 24 ya mkataba huo wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu, au CRPD.

0 Comments