Rais Putin akosoa wanaomvunjia heshima Mtume Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam

Rais Vladimir Putin wa Russia amewakosoa vikali wanaomvunjia heshima Mtume Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi   wa aalihi wa sallam na kusema kitendo kama hicho cha kutusi matukufu ya wengine hakiwezi kuhalalishwa kwa kisingizo cha uhuru wa maoni.


Akizungumza na waandishi habari Alhamisi, Putin amesisitiza kuwa kuumiza hisia za waumini kwa jina la uhuru wa sanaa maoni na ni jambo lisiloweza kutetewa hata kidogo.


Akijibu swali la mwandishi habari kuhusu tafauti baina ya kuumiza hisia za wengine na haki ya msanii kubainisha maoni yake, Putin amebaini kuwa, “Tutafakari kuhusu jambo hili. Tunapaswa kuwapa watu uhuru kwa ujumla kwani mustakabali hautakuwa mwema bila uhuru. Hatahivyo ifahamike kuwa uhuru utakinzania na malengo yetu iwapo utakiuka uhuru wa mwingine.


Rais wa Russia amehoji kuwa: “Je kumtusi Mtume Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi   wa aalihi wa sallam kunaashiria uhuru wa ubunifu?” Akijibu amesema binafsi haafiki kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi   wa aalihi wa sallam. Putin amesema jamii ya Russia inajumuisha watu wa kaumu na dini mbali mbali na Warussia wamezoea kuheshimiana jambo ambalo katika baadhi ya nchi haliko.


Katika miaka ya hivi karibuni katika nchi za Magharibi kumeshuhudiwa vitendo vya baadhi ya wasanii hasa wachora vibonzo wakimvunjia heshima Mtume Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi   wa aalihi wa sallam kwa kisingizo cha uhuru wa maoni. Vitendo hivyo vimelaaniwa vikali kote duniani na Waislamu pamoja na watetezi wa haki kwa ujumla.

0 Comments