UAE yatangaza Ijumaa itakuwa siku ya kazi, Wikiendi ni Jumamosi, Jumapili

Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imetangaza kuwa idara zote za kiserikali nchini humo sasa zitatumia mfumo mpya wa kufanya kazi siku nne na nusu kwa wiki.


Kwa mujibu wa mpango huo Ijumaa itakuwa siku nusu ya kazi ambapo Jumamosi na Jumapili sasa zitakuwa siku kamili za mapumziko ya wikiendi.


Taarifa rasmi zinasema sheria hiyo itaanza kutekeleza kuanzia Januari 1, 2022 na hivyo kufanya wikiendi nchini humo kwenda sambamba na nchi zisizokuwa za Kiislamu.


Katika aghalabu ya nchi za Kiislamu wikiendi ni Alhamisi na Ijumaa au Ijumaa na Jumamosi. Kwa sasa wikiendi UAE imekuwa ni siku za Ijumaa na Jumamosi sawa na nchi zingine kadhaa za Kiarabu. Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wikiendi ni Alhamisi na Ijumaa.


Kufuatia mabadiliko hayo Sala ya Ijumaa kote UAE sasa itakuwa ikisaliwa baada ya saa saba na robo mchana. Kwa mujibu wa utaratibu mpya, saa za kazi nchini UAE kuanzia  Jumatatu hadi Alhamisi zitakuwa ni saa moja na nusu asubuhi hadi saa tisa na nusu mchana na Ijumaa saa za kazi sasa ni kuanzia saa moja na nusu asubuhi hadi saa sita mchana.


Kwa msingi huo hotuba za Ijumaa kote UAE zitaanza saa saba na robo mchana na hivyo wanaotoka kazini watakuwa na wakati wa kutosha kujitayarisha kwa  ajili ya Sala.


UAE sasa imekuwa nchi ya kwanza duniani kuanzisha wiki ya kazi ambayo ni fupi kuliko ile iliozelekea ya siku tano za kazi kwa wiki.


Serikali ya UAE inasema uamuzi huo unalenga kuleta mlingano baina ya kazi na maisha ya kijamii.

0 Comments