Waliohifadhi Qur'ani gerezani Dubai wapunguziwa adhabu

Wafungwa 115 mjini Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu wamepunguziwa adhabu zao kwa miezi sita hadi miaka 20 baada ya kuhifadhi Qur'ani.


Taasisi ya Tuzo ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Dubai (DIHQA) imewasaidia wafungwa hao kuhifadhi Qur'ani na hivyo kuwawezesha kupunguziwa vifungo vyao gerezani.


Mkurugnezi wa Teknolojia katika DIHQA Mohammad Al Hammadi amesema kundi la tatu limefanyiwa mtihani kwa ushirikiano na Idara ya Magereza Dubai.


"Wanafanuzi 124 ambao wamepewa mafunzo na waalimu wetu wa Qur'ani wametahiniwa katika taaluma ya kuhifadhi Qur'ani katika robo ya tatu ya mwaka huu," amesema.


Ameongeza kuwa kati ya wanafunzi hao, 115 wamefanikiwa kupunguziwa adhabu yao kwa mujibu wa juzuu za Qur'ani walizoweza kuhifadhi moyoni.


"Wafungwa saba wampunguziwa miaka 20 ya vifungo vyao  kila moja huku wanne wakipunguziwa miaka 15," amesema Al Hammadi.


"Wafungwa wengine 8 wamepunguziwa miaka 10, wengine 20 wamepunguziwa miaka 20 na 35 wamepunguziwa mwaka moja huku wengine 41 wakipunguziwa miezi sita,"amebaini afisa huyo.


Al Hammadi amesema watamaliza taratibu za kisheria za kupunguza vifungo hivyo kwa kushirikiana na Idara ya Mwendesha Mashtaka na Idara ya Magereza.


Ibrahim Mohammed Bu Melha, Mshauri wa Mtawala wa Dubai Katika Masuala ya Kibinadamu na Kiutamaduni amesema mpango huo wa kuwapunguzia adhabu wafungwa waliohifadhi Qur'ani ulizinduliwa mwaka 2002 na mtawala wa Dubai Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum. Amesema mpango huo umewasaidia wafungwa wengi kurekebisha tabia zao na kupata nuru ya muongozo wa Qur'ani Tukufu.


Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2017, wafungwa 2,950, isipokuwa wauaji, wamepunguziwa au kusamehewa kikamilifu vifungo vyao gerezani baada ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu.

0 Comments