Wito wa Wahindu wa kutekelezwa mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu waibua hasira

 Video zinazowaonyesha viongozi wa kidini wa Kihindu nchini India wakitoa wito wa mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu zimezua hasira na wito madai ya kuchukuliwa hatua dhidi ya wahusika.


Polisi ya India jana Ijumaa ilieleza kuwa, imeanza kuchunguza hotuba za chuki zilizotolewa na viongozi wa Kihindu katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki huko Haridwar kaskazini mwa jimbo la Uttakakhand; ambapo washiriki walitoa wito wa kutumiwa silaha na kuwaua kwa umati Waislamu.  


Kiongozi mmoja wa Kihindu ambaye alihutubia mkutano huo amenukuliwa akisema kuwa, watu hawapaswi kuwa na wasiwasi wa kwenda jela kwa kuua Waislamu. Hiyo ni kwa mujibu wa video zilizorushwa katika mitandao ya kijamii.


Mshiriki mmoja aliyehudhuria mkutano huo wa Waqhindu amesikika akisema: "Hata kama mia moja kati yetu tutakuwa wanajeshi na kuua milioni mbili kati yao, tutashinda.."


Mkutano huo ulihudhuriwa na baadhi ya wanachama wa chama cha Bharatiya Janata (BJP) kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi. Chama tawala India BJP kimekuwa kikituhumiwa kuwachochea Wahindu wenye misimamo mikali wa nchi hiyo kuwauwa Waislamu na jamii nyingine za walio wachache nchini humo, tangu kiingie madarakani mwaka 2014.


Asaduddini Owaisi mbunge mashuhuri Muislamu wa India ameandika katika ukurasa wake wa Twitter baada ya kusambaa mkanda huo wa video wa chuki dhidi ya Waislamu kwamba: "Video hii ni kesi ya wazi ya uchochezi wa mauaji ya kimbari." Hadi sasa serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi haijatoa taarifa yoyote kuhusu kadhia hii.

0 Comments