Ikiwa Mume Na Mke Wamekubaliana Kuingiliana Kinyume Na Maumbile, Je, Kuna Ubaya?

  


SWALI:

 

Assalam alaykum warahmatullahi wabarakatu tunashukuru sana kwa jinsi mnavyojitahidi kutujibia maswali yetu kadiri mnavyo weza na ALLAH subhanahu wataala inshaallah atakulipeni ujira ulio bora zaidi. Suala langu ni, nini hukmu ya mume kumtamkia mkewe unyumba lakini kinyume cha maumbile na nini athari zake na jee kama watakuwa wamekubaliana wote wawili kufanya tendo hilo kuna athari zozote na jee ALLAH subhanahu wataala atakuwa radhi kwa hilo?

 

Inshaallah tunategemea majibu yaliokuwa hayana mushkel ndani yake kwani ni suala linlowaumiza vichwa sana waislamu. ASANTE.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako. Hakika swali hilo ni katika maswali ya kushangaza kabisa, na Muislam kufikiria mambo kama hayo ni kuonyesha jinsi gani baadhi ya Waislam walivyo mbali kabisa na mafundisho ya Dini yao.

 

Inatakiwa tufahamu kuwa makubaliano yoyote yanayokwenda kinyume na maagizo ya Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huwa haifai kabisa kwa Muislamu kuyatekeleza.

 

Hakuna utiifu wala kukubali jambo linalopingana na sheria au jambo lolote lile la shari. Kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hilo ni,

"Hakika utiifu ni katika wema". Al-Bukhaariy, Muslim, An-Nasaaiy, na Abu Daawuud.

Na pia,

"Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba". Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, An-Nasaaiy na Ahmad.

 

Ama tendo la ndoa ni lazima litekelezwe kwa mujibu wa tulivyofundishwa na Uislamu. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

 

"Wakishatwaharika basi waendeeeni katika pale Alipokuamrisheni Allaah. Hakika Allaah Huwapenda wanaotubu na Huwapenda wanaojitakasa. Wake zenu ni konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo" (2: 222-223).

 

Na kuziendea konde zenu mpendavyo, si sehemu ya nyuma, bali ni sehemu ambayo inapatikana uzazi na ndio ikafananishwa na konde/ shamba kwa sababu shamba hulimwa na kuota mazao ambayo kwayo hupatikana mavuno.

Kwa hivyo, ni ubaya sana kwa mwanamume kumwendea mkewe kwa nyuma na athari yake ni kubwa kwani inampatia shida sana mwanamke wakati wa kuzaa na matatizo mengine. Pia inaleta madhara ya kiafya, inakwenda kinyume na maadili matukufu na hii ni tabia mbaya sana.

 

Ama katika Dini yetu, hili ni jambo lililokatazwa kwa Aayah tuliyoitaja hapo juu na Hadiyth zifuatazo:

1.      "Allaah Hatomtazama mwanamume mwenye kumuingilia mkewe kwa nyuma" (an-Nasaaiy na Ibn Hibbaan kwa Isnadi nzuri).

2.      "Amelaaniwa mwenye kumjia mwanamke kwa nyuma" (Ahmad, Abu Daawuud na Ibn 'Adiy).

3.      "Mwenye kumuingilia mwenye hedhi au mwanamke kwa nyuma au kumuendea mchawi na kumuamini kwa anayosema basi amekufuru kwa aliyoteremshiwa Muhammad" (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah, na Isnadi yake ni Sahihi).

4.      "Twaawuus amesema: 'Ibn 'Abbaas aliulizwa kuhusu mtu anaye muingilia mkewe kwa nyuma'. Akasema: 'Huyu ananiuliza kuhusu ukafiri'" (an-Nasaa'iy).

Kwa hivyo ikawa mmekubaliana katika hilo mufahamu mnafanya makosa makubwa mbele ya Allaah Aliyetukuka. Kwa hiyo, mnatakiwa mrudi katika njia ya sawa ambayo haina ujongo wa aina yoyote, na kama mlikuwa mnafanya hivyo, basi mtubie haraka sana na msije kurudia kamwe tendo hilo chafu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments