Kuchomwa moto kambi ya wakimbizi ya Waislamu wa Rohingya

Polisi ya Bangladesh imetangaza kuwa, moto umetokea katika kambi ya wakimbizi ya Waislamu wa Kirohingya wa Myanmar katika ardhi ya nchi hiyo.


Msemaji wa Polisi ya Bangladesh yenye jukumu la kusimamia amani katika kambi ya wakimbizi ya Waislamu wa Kirohingya amesema kuwa, takribani nyumba 200 zimeungua katika tukio hilo la moto na zaidi ya wakimbizi 5,000 wamebakia bila makazi.


Kambi za wakimbizi za Waislamu wa Rohingya zipo katika mpaka wa pamoja wa Bangladesh na Myanmar huku sehemu ya wakimbizi hao wakiwa wamepelekwa katika kisiwa cha mbali. Kuendelea matukio ya kuchomwa moto kambi za wakimbizi za Waislamu wa Kirohingya nchini Bangladesh ni ishara ya wazi kwamba, kambi hizo za wakimbizi hazina hata usalama mdogo kabisa kama ambavyo hazina suhula za kuzimia moto.


Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao waamekimbilia nchini Myanmar wakikimbia vitendo vya ukandamizaji dhidi yao katika nchi yao huko Myanmar vinavyofanywa na mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka wamekuwa wakiishi katika mazingira mabaya kabisa katika kambi hizo za wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh.


Marzouk Darosman, Kaimu Mkuu wa Timu ya Kutafuta Ukweli anasema kuhusiana na hilo kwamba, idadi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya waliouawa katika hujuma na mashambulio ya jeshi la Myanmar dhidi yao haifahamiki, lakini kuna makumi ya maelfu ya wakimbizi Waislamu ambao ni urithi wa jinai dhidi ya binadamu katika nchi hiyo ambao wanaishi katika kambi za wakimbizi wakiwa katika hali na mazingira mabaya kabisa.

Hatua ya jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ya kupuuza na kutojali hali mbaya wanayokabiliwa nayo wakimbizi Waislamuu wa Kirohingya, imewafanya Waislamu hao siyo tu kwamba, wasiwe na matumaini kabisa ya kurejea kwao huko katika jimbo la Rakhine Myanmar, bali wamo katika hali ya kusahauliwa kabisa.


Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, Waislamu wa jamii ya Rohingya ni jamii ya waliowachache iliyodhulumiwa zaidi ulimwenguni   na hata kueleza kwamba, Waislamu hao wanakabiliwa na dhulma kubwa zaidi na ukosefu wa uadilifu wa hali ya juu nchini Myanmar.


Serikali ya Myanmar imewanyima Waislamu hao haki ya uraia wa nchi hiyo na inawatambua kwamba, jamii iliyohajiri kutokea Bangladesh. Hii ni katika hali ambayo, historia inaonyesha kuwa, uwepo wa Waislamu hao nchini Myanmar katika eneo la Arakan linalojulikana leo kwa jina la Rakhine unarejea nyuma kwa mamia ya miaka. Aidha historia inaonyesha kuwa, jamii hiyo imewahi kuwa hata na utawala wa kifalme katika eneo hilo. Hata hivyo wanajeshi wenye misimamo mikali na mabudha wenye kufurutu ada wakiwa na lengo la kupora ardhi, mashamba na nyumba za Waislamu hao, kwa karibu muongo mmoja sasa wameshadidisha mauaji na kuchoma moto ardhi zao na hivyo kupora mali na milki za jamii hiyo iliyodhulumiwa.

Muhammad Nasim, mmoja wa maafisa wa afya na ustawi wa jamii nchini Bangladesh anaamini kuwa: Waislamu wameendelea kushuhudia jamii ya kimataifa ikiwapuuza, lakini Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetuma vifurushi vya misaada ya kibinadamu na hivyo kuwasaidia pakubwa wananchi hao na hivyo kuweza kukidhi sehemu ya mahitaji yao wakiwa katika maisha ya ukimbizi.


Vyovyote itakavyokuwa, Waislamu wa jamii ya Rohingya wanataraji kuiona Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ikizingatia hali yao na kufanya juhudi za kuyapatia ufumbuzi matatizo wanayokabiliwa nayo. Huko nyuma madola ya Magharibi yalijitokeza na kuonyesha sura ya ubinadamu na kuzungumzia suala la kupatiwa misaada Waislamu hao na hata baadhi ya maafisa wa ngazi za juu waliitembelea jamii hiyo, lakini waliishia kupiga picha za ukumbusho tu, kwani kivitendo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa ya kuyapatia ufumbuzi wa kimsingi matatizo ya wananchi hao.


Kwa msingi huo basi, Waislamu wa jamii ya Rohingya wa Myanmar wanataraji kuziona nchi za Kiislamu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) zikichukua hatua za kivitendo za kutatua matatizo ya Waislamu hao, ili sambamba na kuandaa mazingira ya kurejea makwao kunahitimishwa maisha yao ya kuwa ukimbizini.

0 Comments