MATUKIO : Ajali ya gari la waandishi habari yaua watu wasiopungua 14 Simiyu, Tanzania

Watu wasiopungua 14 wamefariki dunia baada ya gari ya waandishi wa habari iliyokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Robert Gabriel kugongana na gari ya abiria aina ya Toyota Hiace katika eneo la Nyamikoma wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.


Mkuu wa Wilaya ya Busega, Gabriel Zakaria amethibitisha kutokea vifo hivyo.


Amesema miongoni mwa waliofariki dunia kuna waandishi wa habari wanne na dereva wao, na watu wengine sita walifariki dunia papo hapo


“Ni kweli ajali hiyo imetokea, watu 11 wamefariki dunia kwenye eneo la tukio wakiwemo waandishi wa habari wanne na dereva, na wengine sita waliokuwa kwenye gari lingine” amesema DC Zakaria


Ameongeza kuwa, dakika chache baadaye majeruhi watatu waliopelekwa kwenye kituo cha afya cha Nasa walifariki dunia, wakiwemo wale waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara.


Mapema leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyo, Blasius Chatanda aliahidi kuwa atatoa taarifa zaidi baadaye.


Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa wote waliopeteza ndugu na marafiki na Watanzania kwa ujumla.    


Mwezi uliopita wa Disemba watu tisa walifariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa katika ajali ya gari aina ya hiace ya kubeba magazeti iliyokuwa ikitoka jijini Dar es Salaam kuelekea jijini Mbeya.

0 Comments