Msikiti wahujumiwa Iowa, Marekani, Waislamu wataka uchunguzi

Waislamu nchini Marekani wanataka uchunguzi ufanyike baada ya msikiti kuhujumiwa katika mji wa Waterloo jimboni Iowa.

Kufuatia jinai hiyo,  Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), ambalo hutetea haki za Waislamu Marekani, limetoa wito wa kufanyika uchunguzi hasa kwa kuzingatia tukio hilo limenaswa na kamera za usalama.Kamera hizo zilimnasa mwanamke akihujumu Kituo cha Kiislamu cha Al Noor ambacho pia kinajumuisha msikiti mnamo Disema 28.


Mwanamke huyo alionekana akichora alama za msalaba katika kuta za msikiti na kisha akaandika maneneo yenye kuvunjia heshima Uislamu na kuwatusi Waislamu.


Siku ya Jumatano CAIR imetoa taarifa ikitaka wakuu wa usalama waanzishe uchunguzi.


“Tukio hilo la hivi karibuni la hujuma dhidi ya Msikiti Marekani ni ishara ya hatari ya chuki dhidi ya Waislamu,” amesema Naibu Mkurugenzi wa CARI Edward Ahmed Mitchell katika taarifa.


Imamu wa Msikiti wa Al Noor Sheikh Ahmed Abouzid anasema analenga kuelimisha jamii kuhusu Uislamu.


“Je unadhanu hatumpendi Nabii Issa (Yesu)? Tunampenda na sisi si maadui wenu”, amesema Abouzid.


Katika Uislamu, Nabii Issa-Amani ya Allaah iwe juu yake, anatambuliwa na kuheshimiwa kama Mtume wa Allaah.


 Ripoti iliyotolewa na CAIR mwezi Aprili  mwaka 2021 ilibaini kuwa Marekani kumeshuhudiwa ongezeko la asilimia 9 ya idadi ya malalamiko ya unyanyasaji dhidi ya Waislamu ambayo yalipokewa mwaka wa 2020 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.


Kwa upande wake Baraza la Jumuiya za Kiislamu nchini Marekani limemwandikia barua Rais wa nchi hiyo, Joe Biden likisisitiza kuwa, kuwepo mwakilishi maalumu wa kusimamia na kupambana na chuki na propaganda chafu dhidi ya Uislamu kunaweza kusaidia juhudi za kupata suluhisho la tatizo hilo ambalo linaizonga jamii ya Waislamu nchini Marekani. 

0 Comments