Hilaal: Waislamu Wote Duniani Wafuate Mwandamo Mmoja Wafunge Na Kula ‘Iyd Siku Moja ?

  

 

SWALI:

 

nilimskia sheikh mmoja katika kipindi cha televisheni anasema kwamba haiwezekani watu wote duniani kupata sikukuu siku moja kwa sababu kuna nchi zimepishana kwa takribani masaa 24,na kutoa mfano kwamba, Honolulu Marekani jumamosi saa 3 asubuhi, New Zealand ni saa 2 asubuhi Ijumaa. je hii ni kweli na kweli inawezekana ikawa ni sababu ya kutowezekana kufunga na kufungua siku moja dunia nzima??

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ni kweli kuwa zipo sehemu ambazo zimetofautiana kwa masaa takriban 23 kama ulivyosikia  lakini huyo shekhe kachanganya baina ya sehemu. Jua linachomoza Wellington, New Zealand mwanzo kabla ya Hawaii – Honolulu, USA, yaani ikiwa New Zealand ni saa mbili siku ya Ijumaa, Honolulu itakuwa Alkhamisi saa tatu asubuhi. Hata hivyo tofauti hiyo si sababu kabisa kwa Waislamu duniani kutofunga na kutofungua pamoja.

 

Ni hakika isiyopingika kabisa kuwa kuanzia wakati ambao mawasiliano yamekuwa ni sahali kupatikana kote duniani mwezi umekuwa ukionekana Mashariki ya kati. Na kwa sasa kama katika nchi ya Tanzania na Kenya baada ya Waislamu kuchukua umuhimu mkubwa wa kuangalia mwezi ukawa mwandamo wa sehemu hii unakwenda sambamba na ule wa Mashariki ya Kati.

 

Tufahamu kuwa tofauti baina ya sehemu hiyo na sehemu za Mashariki na magharibi ya ulimwengu haizidi masaa 12. Hakika mazungumzo hayo ni watu tu kutafuta vizisababu visivyokuwa na msingi wowote wa kidini.

 

Ni ajabu kuwa mashekhe hao wamejikita kuzungumza kulalamika kuhusu mwezi wa kimataifa pekee wala huwasikii kuzungumza matatizo ya rai kama:

 

1.      Kuzingatia mipaka ya kila nchi.

2.      Kuzingatia umbali wa farsakh 24.

3.      Kuzingatia masafa ya qasri.

4.      Kuzingatia tofauti za matlai.

5.      Kuzingatia usawa wa bahari (sea level).

6.      Kuzingatia maeneo ya mashariki na magharibi.

7.      Kuzingatia kusadifu.

 

Hata hivyo, kuna baadhi ya Wanachuoni wanaoonelea kila mtu afunge na mwezi wa nchi yake au utakaotangazwa na Kiongozi wa Kiislamu wa nchi yake.

 

Kifupi, haya mas-alah yana ikhtilaaf na haipaswi upande mmoja kuwalaumu wengine au kuwabeza.

0 Comments