SHEIKH BARAHIYAN AUTANGAZA MSIKITI MPYA WA TAASISI YA ANSAAR DUGA TANGA.Mudir Markaz kuu Taasisi ya Ansaar Muslim Youth Centre Sheikh Salim Barahiyan ameutangaza msikiti mpya wa Taasisi hiyo uliopo katika kata ya Duga jimbo la Tanga Mjini nchini Tanzania.
Akitoa kalimah fupi ya ufunguzi baada ya kuswaliwa swalah ya kwanza ya Adhuhuri katika msikiti huo leo Alkhamiys Aprili 14 ,2022 amempongeza mjenzi mkuu Abuu Suheyl kwa wema alioufanya na kuukabidhi kwa Taasisi ya Ansaar huku akiwaasa waislamu kuifanya 'ibaadah hiyo ya kujenga misikiti ambayo malipo yake ni pepo.
Kiongozi huyo wa juu katika Taasisi ya Ansaar Muslim Youth Centre ametaja miongoni mwa kazi za misikiti katika jamii ya kiislamu kuwa ni pamoja na kuwaunganisha waislamu katika 'ibaadah ya jamaa'a.
"Ndugu zangu katika Iymaan tujue kwamba wale wenye uwezo wafahamu kwamba hili ni jambo 'adhwiym ,jambo la 'ibaadah (kujenga msikiti) ,kubwa kabisa la lengo la kujenga msikiti ni kuwakusanya watu kwa ajili ya 'ibaadah tena ya Swalah" amesema Sheikh Barahiyan.
Aidha amesema miongoni mwa kazi nyingine za misikiti ni kituo cha kielimu na Da'awah , kuwaelimisha watu mambo ya jamii , kuwa kama vituo vya afya na sehemu ya kuwakaribisha wageni.
"Lakini kubwa vilevile ambalo Bwana mtume alilitumia ilikuwa ni Markaz Ta'alim ,ilikuwa nibMarkaz ya kuelimisha hasa dini ya Allaah Subhaanahu Wata'ala,kwa hiyo Mtume alitumia njia mbalimbali katika madarasa khutbah katika kuwaelilisha waislamu dini yao, msikiti hautokuwa na sifa ya msikiti kama hapaelimishwi hapa"
"Moja ya kazi za msikiti vilevile zama za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wasalam) ilikuwa ni kuwaelimisha waislamu mambo ya jamii jinsi yalivyo,ilikuwa ni kituo cha habari vile ilikuwa misikiti ni vituo vya afya" amesema Sheikh Barahiyan.
Awali akinzungumza kabla ya kalmah ya ufunguzi Naibu Mudir Markaz kuu Ansaar Muslim Youth Centre Sheikh Ally Nassor amewakumbusha waislamu suala la kuitunza na kuimarisha misikiti.
"Tupo katika msikiti huu ambao ni katika masaajid ambazo (zipo kwa lengo la uchamungu) hatusemi tunazindua lakini tunawakumbusha waumini umuhimu wa nyumba za Mwenyezingungu Subhaanahu Wata'ala, Misikiti ni nyumba za Allaah ,na Allaah ametutaka kuimarisha misikiti na kuitunza misikiti" amesema Sheikh Nassor.
Msikiti huo ulioanza kutumika leo ambao una eneo kubwa ,stoo na ofisi ya Imaam unakuwa kati ya misikiti ya Sunnah iliyopo jijini Tanga ambapo kwa mujibu wa Tangazo la leo utaendesha taratibu zake kwa mujibu mafundisho ya Qur'aan na Sunnah kwa ufahamu wa wema waliopita.
IMETOLEWA NA RADIO IHSAAN FM 102.1 TANGA TANZANIA.

0 Comments