Chunga Unachokituma Kwa Watu

 


ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ

Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema. [At-Takaathur: 8]

 

Tumekuwa tunakutana ndani ya boksi zetu za barua pepe na barua za ajabu ajabu ambazo imefikia Waislam kutuma picha za wanawake walio uchi sehemu za miili yao zikionekana na maumbile yao ya kushtusha. Muislam akituma mambo kama hayo akiweka kichwa cha habari bila staha wala khofu, ‘mambo hayo’ au maneno kama hayo ya kushabikia uchafu. Wengine wakituma picha za mwanamke aliyechorwa Aayah za Qur-aan mgongoni mwake akiwa nusu uchi! Hayo yote ni mambo yanayofanywa na Waislam wakitaka kuonyesha maovu yanayofanywa na huku wakieneza maovu mengine bila kujua au kufikiria kwa undani kabla ya kutuma.

 

Kwa hakika zimefika zama ambazo Waislamu wamefanya ya haramu kuwa ni halali na kinyume chake, zimefika zama ambazo baba wa Kiislamu anatoa chupa ya mvinyo ndani ya friji na mwanawe akimuona, zimefika zama ambazo mzazi anamuachilia bintiye kutoka (kuzini) na mvulana bila ya kuhisi taabu, na zimetufikia zama ambazo Muislamu anatuma mambo yasiyo na kichwa wala miguu akiona kuwa ni sawa tu. Hizi ndizo zama ambazo tunaishi nazo hivi sasa. Zama ambazo Sunnah imesahaulika, na imebadilishwa kuwa ni Sunnah/Fardhi kutuma email hata ikiwa ina madhara ya aina gani.

 

“Nakuusieni kumcha Allaah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrisheni) ni Mtumwa wa Ki-Habashi. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu. Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu” [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy kasema Hadiyth Hasan Swahiyh].

 

Ni vyema mtumaji/mtayarishaji ajitayarishie jibu mbele ya Muumba dhidi ya neema ya wakati, uhai, uzima na nuru alizojaaliwa; kwani bila ya neema hizi katu asingeweza kutuma mambo machafu.

 

Hivi Muislamu anahitaji kuelezwa nini zaidi ya kujua kwamba mwili wa mwanamke wote ni uchi? Ni vitanga vya mikono na uso (full stop!) hakuna kiungo chengine ambacho ni ruhusa kukiona haswa baina ya wenye kuweza kuoana. Leo imefika wakati Muislamu bila ya haya wala kuona vibaya akaiangalia picha kama hizo, akafurahika nayo, akaipenda kidhati hadi kufikia kuwatumia Waislamu wenziwe. Basi kwa hakika hayaa (kuona aibu) imeondoka, kwani amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Ikiwa huna hayaa basi fanya utakalo” [Imesimuliwa na Abu Mas’uud ‘Uqbah Ibn ‘Amr Al-Answaariy Al-Badriy na kupokelewa na Imaam Al-Bukhaariy].

 

Kwa kumalizia, Waislamu ni watu wenye tabia bora na ni wenye kufuata mwenendo ambao umekamilika. Hivyo tunawausia wenye kushikamana na maasi kama haya kutubia kwa Rabb Mwenye Enzi. Pia tunawasihi kuchukua faida ya mambo matano (5) kabla ya matano (5): ujana kabla ya uzee, afya kabla ya maradhi, mali kabla ya ufukara, faragha kabla ya mishughuliko na maisha kabla ya kifo. (Hadiyth iliyopokelewa na Al-Haakim).

 

Kwa faida zaidi, makala ifuatayo inaeleza juu ya sababu kumi za kumtaka Muislamu asitume barua pepe kibubusa:

 

Sababu Kumi Za Kumtaka Muislamu Asitume Barua Pepe (Email/Forward) Kibubusa

 

Tunamuomba Rabb Atusamehe madhambi yetu na Atuongoze njia iliyonyooka.

 

 

0 Comments